Na Mwandishi wetu,Manyara
Wafanyabiashara na wadau wa sekta mbalimbali wanatarajiwa kukutana mkoani Manyara katika Maonesho ya Biashara ya Tanzanite Manyara Trade Fair yanayotarajiwa kuanza Oktoba 15 hadi 21, mwaka huu, katika viwanja vya Tanzanite Kwara, Babati, huku washiriki 500 wakithibitisha kushiriki.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya maonesho hayo, Lairumbe Laizer, Meneja wa Chemba ya Biashara ya Taifa mkoa wa Manyara, alisema maonesho hayo ni sehemu ya majukumu ya taasisi hiyo katika kukuza biashara na kuimarisha shughuli za kiuchumi nchini.
Laizer alisema maonesho hayo yanalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau wa sekta mbalimbali kukutana, kuonyesha bidhaa zao na kubadilishana uzoefu utakaosaidia kukuza biashara zao.
Alisema kuwa washiriki wa maonesho hayo wanatarajiwa kutoka katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta binafsi, kilimo, madini na ufugaji, ambazo ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yatatoa nafasi kwa wafanyabiashara kutangaza bidhaa na huduma zao kwa wananchi pamoja na kutafuta masoko mapya yatakayowawezesha kupanua shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, Laizer alisema maonesho hayo yatapambwa na wanyama mbalimbali, jambo litakaloongeza mvuto kwa wageni na wananchi watakaotembelea viwanja hivyo wakati wa maonesho.
Alisema kuwa kupitia maonesho hayo, washiriki watapata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za biashara, kubadilishana mawazo na kujenga mahusiano yatakayoweza kuwasaidia kuboresha shughuli zao.
Laizer alitoa wito kwa Watanzania na wadau wengine wa biashara kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo ili kutumia fursa zitakazopatikana katika kukuza biashara na shughuli zao za kiuchumi.
Alisema ushiriki wa wadau mbalimbali utasaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kuchochea ubunifu katika sekta zinazoshiriki, hivyo kuongeza nafasi za maendeleo ya kiuchumi.
Alisisitiza kuwa maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kuonyesha uwezo wao, kutangaza bidhaa zao na kujifunza mbinu mpya zinazoweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto za soko.

No comments:
Post a Comment