Teknolojia : Tanzania Yavutia nchi za Afrika Mashariki kwa Mifumo ya Kidijitali ya Posta - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Friday, 16 October 2026

Teknolojia : Tanzania Yavutia nchi za Afrika Mashariki kwa Mifumo ya Kidijitali ya Posta

 





Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya mifumo ya kidijitali ya huduma za posta, ikiwemo mfumo wa anwani za makazi na Posta Kiganjani, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuvutia mataifa mengine kujifunza kutoka nchini humo.


Hayo yameelezwa na Caroline Kanuti, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta na Usafirishaji kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakati akizungumza leo jijini Arusha kwenye Kongamano la Tano la Wasimamizi wa Huduma za Posta Afrika Mashariki.


Kanuti alisema mfumo wa anwani za makazi nchini Tanzania umekuwa kivutio kikubwa, kiasi cha watalii kuuona kama sehemu ya vivutio vinavyoweza kutembelewa na kujifunzwa kutokana na namna ulivyowezesha utambuzi wa maeneo na kurahisisha utoaji wa huduma.


Alisema kongamano hilo litajadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta ya posta katika Afrika Mashariki, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, hali ya sekta hiyo katika ukanda huo pamoja na mifumo ya kidijitali inayoweza kuboresha huduma kwa wananchi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Shirika la Posta Tanzania, Maiko Njau, alisema Tanzania imepiga hatua katika mifumo ya manunuzi ya kidijitali, ambayo imeendelea kuonesha fursa za matumizi ya teknolojia katika kurahisisha upatikanaji wa huduma.


Njau alisema nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya zinaendelea na mazungumzo kuhusu namna ya kutumia mifumo hiyo ili huduma zinazotolewa kupitia teknolojia ziweze kuwafikia wananchi wao.


Aliongeza kuwa mfumo wa Posta Kiganjani una mchango mkubwa katika kurahisisha huduma za posta, akieleza kuwa una viwango vya usalama vinavyolenga kulinda watumiaji na taarifa zao.


“ Mfumo wa Posta Kiganjani ni mfumo bora sana kwani una usalama wa kutosha, na sisi kama nchi hii ni hatua kubwa sana mpaka majirani zetu wameutamani,” alisema Njau.


Kongamano hilo la Tano la Wasimamizi wa Huduma za Posta Afrika Mashariki limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo kwa lengo la kujadili mikakati ya kuboresha huduma za posta, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wananchi katika ukanda huo.

No comments:

Post a Comment