Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, ameingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 20 katika Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Monduli, baada ya wananchi kuvamia eneo la mwekezaji lenye ukubwa wa ekari 200 na kuanzisha makazi pamoja na shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Zaburi, Novemba 6, 2026, Mhe. Makalla amebainisha kuwa kampuni ya Rhino Equipment & Transportation ndiyo mmiliki halali wa eneo hilo, huku Serikali ikipendekeza mwekezaji huyo kutenga ekari 100 kwa ajili ya wananchi wa kitongoji hicho ambacho tayari kimesajiliwa na kuwa na miundombinu ya kijamii ikiwemo msikiti, kanisa, shule ya awali, maji na umeme.
Aidha, Mhe. Makalla ameuagiza uongozi wa kampuni hiyo kukaa na wananchi walioingia katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa ekari 100 ili kujadiliana na kufikia makubaliano yatakayowezesha matumizi sahihi ya ardhi hiyo na kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu.
Amewataka wananchi kuwa watulivu na kusitisha uvamizi pamoja na uendelezaji wa maeneo hayo hadi pale makubaliano yatakapokamilika. Pia, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo na kuhakikisha kunakuwa na mpango mzuri wa matumizi ya ardhi itakayotengwa kwa ajili ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mzee,Leng’ida , amesema busara na hekima zilizotumiwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na timu yake katika kutafuta suluhisho la mgogoro huo zitarejesha matumaini na kuleta tabasamu jipya kwa wakazi wa Kitongoji cha Zaburi.
“Busara nyingi ambazo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa umetumia, pamoja na timu yako, zitasaidia kuleta tabasamu jipya kwetu wananchi wa Kijiji cha Zaburi. Tunakushukuru kwa hatua hii,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makuyuni,Ngayoki amesema atahakikisha anasimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa katika ngazi ya kijiji na kata kwa kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha suluhisho lililopatikana linatekelezwa.
Naye mkazi wa Kitongoji cha Zaburi, Bi. Naserian Saitabau , amesema kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakiishi katika hali ya taharuki kutokana na mgogoro huo, huku wakikosa matumaini ya kupata suluhisho la kudumu.
Amesema hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa imewapa matumaini mapya, huku akiahidi kuwa wananchi wataendelea kumuombea na kuamini kuwa mazungumzo yake na mwekezaji yatatoa majibu ya kudumu kwa changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa wananchi wana matumaini makubwa kuwa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa utamaliza mgogoro huo na kuwawezesha kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.




.jpeg)





.jpeg)
No comments:
Post a Comment