Matukio : Siku Moja na Sir Andy Chande - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Sunday, 9 April 2017

Matukio : Siku Moja na Sir Andy Chande



Marehemu Sir Andy Chande

Na Mohamed Said - April 07, 2017
Ilikuwa katikati ya miaka ya 1990 nikiwa afisa mdogo Makao Makuu ya Tanzania Harbours Authority (THA) katika Idara ya Masoko iliyokuwa ikiongozwa na Dr. Ramadhani Kitwana Dau. Idara hii ilikuwa idara ndogo kwa maofisa ndani yake na ndiyo kwanza imeanzishwa.

Mimi nilipewa uhamisho kutoka Idara ya Biashara kwenda Idara ya Masoko kwa kile nilichoelezwa kusaidia kuanzisha idara mpya.

Lakini ukweli ulikuwa mkurugenzi alikuwa anasafiri sana nje ya nchi na pakawa hapana mtu idarani angalau wa kuishikilia idara kwa muda. Lakini palikuwa na sababu nyingine. Ala kuli hali Dr. Dau alikuwa tukifahamiana. Kipindi hiki Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi alikuwa Sir Andy Chande na Mkurugenzi wa Bandari wenyewe tukipenda kumuita DG yaani Director General, alikuwa Mzee Athmani Janguo.




Ikasadifu kuwa Bodi ya Wakurugenzi inakutana chini ya Mwenyekiti Andy Chande wakati Mkurugenzi wa Masoko Dr. Dau yuko nje ya nchi na ametoa ‘’notice,’’ kuwa nafasi yake atakaimu Mohamed Said. Yote yaliyotakiwa kutolewa taarifa kwa Bodi alikuwa kayatekeleza hivyo kazi yangu itakuwa kufanya, ‘’short presentation.’’




Bandarini walipita wenyeviti wengi wa bodi lakini ukurugenzi wa Andy Chande ulikuja na habari nyingine. Taarifa zilikuwa zikivuja na kutufikia maofisa wadogo ilikuwa mabosi wetu walikuwa wakihenyeshwa na Chande kiasi cha kulowesha vitambaa kwa kufuta jasho. Nikiri kwa kusema kuwa habari hizi wakati mwingine zikitufurahisha maofisa wadogo kwa kusikia kuwa wale waliokuwa wanatufanya sisi katika viti vyetu tuone kama moto umewashwa chini yake Mungu katulipia na sisi kwa wao kupata saizi yao wa ‘’kuwanyanyasa.’’




Tukisikia habari kuwa Chande alikuwa hachukui posho ya kikao. Tukipata habari kuwa mkurugenzi akichelewa kikao hamruhusu kuingia. Yaani yeye mwenyekiti akiingia Board Room na kukalia kiti chake cha enzi haingii tena mtu. Ilimuradi madereva wakikaa katika magari yao kusubiri mabosi wao habari zilikuwa Chande hivi Chande vile.




Bila shaka hawa madereva walikuwa wanazinasa habari hizi kwa kuwasikia mabosi wao wakizungumza wakati wakiwaendesha. Juu ya hayo yote kila mfanyakazi wa bandara alikuwa anajua kitu kimoja kuhusu Chande nacho ni kuwa alikuwa tajiri kufru.




Haya mambo ya Freemasons wakati ule yalikuwa bado siri kubwa ila mimi nikijua kuwa Chande alikuwa Freemason na nilijua kwa sababu mzee wangu mmoja na yeye alikuwemo kwenye ‘’club,’’ hiyo kama mwenyewe alivyopenda kuiita na hakuwa akimpenda sana Chande. Alikuwa akinambia,




‘’Natamani nimfanyie ugomvi Chande lakini siwezi kwa kuwa tuko ‘’club,’’ moja na sheria zetu zinatukataza kugombana wenyewe kwa wenyewe.’’

Huu ugomvi wao haukuwa wa leo ulianza miaka mingi nyuma toka enzi za kupigania uhuru wao wakiwa TANU na siasa zao za Afrika kwa Waafrika. Siasa ambazo Nyerere na TANU walizishinda. Ikawa sasa kila Chande akichaguliwa katika nafasi na Nyerere nikifika ofisini kwa mpashaji wangu habari itakuwa hiyo.

Ikawa sasa nimemfahamu Chande kutoka kwa mwanachama mwenzake wa hiyo ‘’club,’’ yao. Siku moja nikamuuliza mzee wangu, ‘’Hii ‘’club,’’ yenu ni ‘’club,’’ gani?’’ Akanitazama usoni huku kakunja uso akaniuliza, ‘’Wewe unaitakia nini?’’




Sikuuliza tena hilo swali lakini iko siku akanitajia.




Nikiwa nimeelemewa na habari za Chande nikawa sasa najitayarisha kuingia katika kikao cha Bodi ya Mamlaka ya Bandari Chande akiwa Mwenyekiti wake.




Bandari maofisa tukishonewa Kaunda Suti kama sare ya kazi. Haikuwa lazima uvae kila ukija kazini lakini kwa yale niliyosikia kuhusu Chande siku ile ya Bodi nilikuwa katika sare kwa kuzingatia kuwa kamba hukatikia pabovu.




Kichekesho kikibwa katika hili ni kuwa mimi nilikuwa ofisa mdogo mno na naamini hajapatapo ofisa wa ngazi yangu kukaimu nafasi ya kubwa ya ukurugenzi. Ilikuwa hakuna mantiki na ni jambo lisilowezekana. Lakini kwa kuwa nilikuwa idarani hapakuwa na jinsi ila nikaimu nafasi ya ukurugenzi na hivi ndivyo nikajikuta nimeingia katika bodi pamoja na wakurugenzi wa idara mbali mbali ambao kwangu ni mabosi wakubwa na hata umri wamenipita kwa mbali sana.




Nimetulia kwenye kiti na wakurugenzi wenyewe na mara Chande akaingia Board Rom kafatana na Mkurugenzi Mkuu Athmani Janguo.




Kikao kikaanza.




Ikawa Mwenyekiti Chande na Athmani Janguo wananong’ona sauti ziko chini lakini aliyekuwa anazungumza ni Chande.




Wakurugenzi wametulia tuli.




Baada ya mazungumzo yao kule mbele Mkurugenzi Mkuu akatuamuru sote tutoke tusibiri hapo nje. Naam. Si bure liko jambo niliiambia nafsi yangu. Wakurugenzi wote wakawa wamesimama nje wamewaacha Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wako ndani bila shaka wanaendelea mazungumzo muhimu.




Pale nje tukisubiri nawaangalia wazee wangu. Walikuwako waliovuta sigara na kupuliza moshi juu hewani na walikuwapo pia waliokuwa wanauma meno kwa ghadhabu.




Ilikuwa wazi wamefedheheshwa kwa kutolewa ndani ya Board Room na kusimamishwa nje kwenye, ‘’corridor.’’ Kwangu mimi hii ilikuwa mfano wa wanafunzi watukutu wakiotokewa darasani na mwalimu. Madirisha yalikuwa wazi yakiingiza upepo wa Bahari ya Hindi lakini wazee wangu naona walikuwa wanahisi joto maana wakijongea madirishani na kuchungulia nje kuiangalia Dar es Salaam Port.




Haukupita muda mrefu tukaitwa ndani. Kilichokosewa kikaelezwa kwa wakurugenzi na Mkurugenzi Mkuu akaahidi kuwa kitarekebishwa na kurejeshwa kwenye kikao siku ya pili.




Ilipofika zamu ya Idara ya Masoko kufanya ‘’presentation,’’ Mkurugenzi Mkuu Athmani Janguo akamwambia Mwenyekiti wa Bodi Andy Chande kuwa yeye ndiye atawasilisha.




Allah alikuwa kapokea dua zangu.




Vibweka vya Chande vilikuwa havijesha.




Kwa kawaida posho ya Wakurugenzi huwa inatolewa wakati kikao kinaendelea. Mgawaji anapita kwa wakurugenzi mmoja mmoja anagawa bahasha.




Chande pale mbele alipokuwa amekaa akaona bahasha zinatolewa akasema, ‘’Hapana kutoa fedha tunatoa fedha kwa watu wanaofanya kazi. Acha kugawa.’’
Sikuweza kuamini masikio yangu.




Ikanidhihirikia kuwa kumbe yote niliyokuwa nayasikia kuhusu Mwenyekiti Chande kumbe kweli.
Lakini baada ya kikao tuko ofisini tunaendelea na kazi mgawaji akatuletea bahasha zetu. Siku ya pili Bodi inaendelea lakini Mkurugenzi wa Masoko Dr. Dau akawa kesharudi safari.




Bismillah kuona sura yake tu baada ya salamu nikampa taarifa ya kikao cha bodi jana na yote mengine ya biashara mpya na nengineo[MS1] kwangu yalikuwa hayana umuhimu.
Dr. Dau akanambia,’’Hivi asubuhi hii wakurugenzi wote tumeitwa kwa DG kuna kikao kabla ya kikao cha bodi.’’




Baadae Dau alinambia kuwa Mkurugenzi Mkuu aliwaambia kuwa hajapata kuhisi vibaya kama alivyohisi jana.




Tulipokuwa wadogo nilikuwa nikimsikia mama yangu akisema kila anapomhadithia mtu aliyekuwa na mengi ya kueleza kuhusu yeye, ‘’Chini kunakwenda watu.’’




Siku yangu moja na Andy Chande ilitosha kumwelewa na kujua kwa nini juu ya yeye mali yake Kengele Tatu (sasa National Milling Corporation) kutaifishwa bila ya fidia hakutetereka, hakukimbia nchi wala hakugombana na Mwalimu Nyerere wala na serikali akabaki nchini na akaanza biashara nyingine na akatajirika pengine kupita pale mwanzo. Huku akifanya biashara zake alikuwa pia akitumikia bila kinyongo nafasi kadhaa alizokabidhiwa na nchi.




Hakika chini kunakwenda watu.

No comments:

Post a Comment