Habari : Kikwete Aihimiza Umoja wa Afrika na Maendeleo ni Zaidi ya Uchaguzi Katika Chuo cha Ulinzi cha Nigeria - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

21 Aug 2024

Habari : Kikwete Aihimiza Umoja wa Afrika na Maendeleo ni Zaidi ya Uchaguzi Katika Chuo cha Ulinzi cha Nigeria

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatatu, alitoa mhadhara wa kusisimua katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Nigeria huko Abuja, akisisitiza juu ya uelewa mpana wa demokrasia na akitoa msisitizo mkubwa juu ya umuhimu wa umoja kwa maendeleo ya Afrika.


Akiongea na viongozi wa kijeshi, maafisa wa serikali, na wageni wengine mashuhuri, Dkt. Kikwete amesema demokrasia ni zaidi ya kitendo cha kupiga kura, akizisihi nchi za Afrika kuzingatia umoja na maendeleo kama nguzo za mustakabali wa bara hili.

Mhadhara wa Dkt. Kikwete, uliopewa jina "Demokrasia Zaidi ya Masanduku ya Kura: Njia ya Umoja na Maendeleo ya Afrika," uligusia pia uhusiano kati ya demokrasia, uchaguzi, na maendeleo barani Afrika.

Alisema kuwa ingawa uchaguzi ni sehemu muhimu ya utawala wa kidemokrasia, lakini haupaswi kuonekana kama kiashiria pekee cha demokrasia. Badala yake, alitoa wito wa kuwepo na mtazamo mpana zaidi unaozingatia michakato na matokeo ya utawala kama vipimo muhimu vya mafanikio ya demokrasia.

"Demokrasia ni zaidi ya kitendo cha kupiga kura," alisema Dkt. Kikwete. "Ni kuhusu kuunda mazingira ya kisiasa ambapo maoni mbalimbali yanakusanywa, maamuzi yanachukuliwa kwa pamoja, na mahitaji ya jamii yanashughulikiwa kwa ufanisi. Kujikita tu kwenye uchaguzi ni kuwa na mtazamo finyu ambao unahatarisha kupuuza kazi na majukumu mengine ya serikali ya kidemokrasia."

Kuhusu uhusiano kati ya umoja na maendeleo, Dkt. Kikwete alisisitiza umuhimu wa umoja wa Afrika ni muhimu sana kama nguvu ya mabadiliko ya maendeleo endelevu.

Akikumbushia Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, alisisitiza kuwa umoja ni muhimu kwa kushinda changamoto za utandawazi na kuhakikisha kuwa Afrika inaibuka kama nguvu kubwa ya kiuchumi na kisiasa duniani.

Alipongeza juhudi kama vile Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kama hatua muhimu kuelekea kutimiza maono ya Afrika iliyo na umoja na yenye mafanikio.

"Umoja ulikuwa muhimu wakati wa mapambano yetu ya uhuru, na unabaki kuwa muhimu hadi leo," alisema Dkt. Kikwete. "Ili kuhakikisha maendeleo, lazima tuwe na umoja. Uwezo wa Afrika kama mchezaji wa kimataifa ifikapo mwaka 2050 unategemea uwezo wetu wa kufanya kazi pamoja, ndani ya mataifa binafsi na katika bara lote."

Akigusia kuhusu maendeleo na changamoto zinazokabili mataifa ya Afrika, Dkt. Kikwete alikiri kujwapo kwa hatua kubwa zilizopigwa katika kuboresha utawala na demokrasia barani Afrika.

Hata hivyo, alionya dhidi ya kujisahau, akibainisha kuwa uhusiano kati ya demokrasia na maendeleo si rahisi kila mara, na kwamba kuna matokeo mseto yaliyoonekana katika nchi za Afrika ambapo ukuaji wa kiuchumi hauendani sana na maboresho katika utawala.

"Utawala bora ni muhimu kwa maendeleo endelevu, lakini pia tunapaswa kutambua kuwa maendeleo yanaweza kutokea katika muktadha tofauti," alibainisha. "Njia ya Afrika kuelekea maendeleo inapaswa kuongozwa na hali zetu, na viongozi wetu wanapaswa kutilia maanani demokrasia na umoja ili kufikia uwezo kamili wa bara hili."

Akihitimisha mhadhara wake, Dkt. Kikwete alisisitiza umuhimu wa kuona demokrasia, umoja, na maendeleo kama vipengele vilivyounganishwa ambavyo ni muhimu kwa mustakabali wa Afrika.

Aliwatia moyo viongozi wa Afrika na watunga sera kwa kuchukua mtazamo mpana wa demokrasia unaozidi uchaguzi, na kuendeleza mazingira yanayounga mkono ukuaji jumuishi, maelewano ya kijamii, na utulivu wa kisiasa.


Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Nigeria Mheshimiwa Mohammed Badaru Abubakar katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Nigeria huko Abuja, Jumatatu, wakati wa Mahafali ya Mhadhara wa Kozi ya 32 ambapo Dkt. Kikwete alikuwa mgeni rasmi.

Wahitimu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Nigeria huko Abuja wakitoa heshima kwa kusaluti wakati nyimbo za taifa zikipigwa, Jumatatu, wakati wa Mahafali ya Mhadhara wa Kozi ya 32 ambapo Dkt. Kikwete alikuwa mgeni rasmi.

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri wa Ulinzi wa Nigeria Mheshimiwa Mohammed Badaru Abubakar wakipiga picha na wahitimu na wakuu wa taasisi katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Nigeria huko Abuja, Jumatatu, wakati wa Mahafali ya Mhadhara wa Kozi ya 32 ambapo Dkt. Kikwete alikuwa mgeni rasmi.

No comments:

Post a Comment


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633