HABARI: “Tumeridhishwa na Uwekezaji Kiwanda cha Chai MPONDE”-Kamati ya Bunge ya PIC. - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


17 Oct 2022

HABARI: “Tumeridhishwa na Uwekezaji Kiwanda cha Chai MPONDE”-Kamati ya Bunge ya PIC.

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID

WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wameridhishwa na uwekezaji uliofanywa katika kiwanda cha Chai Mponde kilichoko Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.

Wameyasema hayo baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichoko Kata ya Mponde, jimbo la Bumbuli Oktoba 15, 2022 ili kuona uwekezaji huo uliofanywa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

“Kwa niaba ya Kamati nichukue fursa hii kuwapongeza sana, nadhani nyuso zetu mmeziona tumeridhika na kile tulichoona, naomba spirit hii mliyoanza nayo msiipunguze muendelee nayo.”Alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. George Malima ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mpwapwa.

Alisema kazi ya Kamati yake ni kuangalia pale ambako serikali imeweka mitaji.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameruhusu fedha nyingi kuja kwenye kiwanda hiki ili muweze kuwekeza na hivyo kutoa ajira za kutosha na kuinua maisha ya Watanzania, hiyo ndiyo hasa nia ya Mheshimiwa Rais.” Alibainisha.

Naye Dkt. Julius Chaya ambaye ni Mbunge wa Manyoni na Mjumbe wa Kamati hiyo ya PIC alisema wakati wawekezaji hao walipokutana na Kamati hiyo jijini Dodoma, waliona wazo hilo la uwekezaji ni zuri sana kwani uwekezaji ndio umeweza kukuza ajira kwenye maeneo mbalimbali duniani.

“Tunawapongeza mnapofufua hivi viwanda, wananchi wanapata ajira, wakulima nao wanapata mahala pa kuuza mazao yao kwakweli tunaishukuru serikali lakini pia tunaishukuru Mifuko yote kwa kazi nzuri.” Alisisitiza Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar na Mjumbe wa Kamati, Mhe. Mariam Mwinyi.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe wametoa ushauri kuwa ni lazima uongozi wa kiwanda uhakikishe wamejipanga vizuri katika eneo la masoko hususan yale ya nje, kwani wanunuzi wakubwa wa bidhaa za kilimo licha ya kusisitiza ubora lakini pia hupenda hakikisho la kupata bidhaa kwa mwaka mzima bila kusitisha.

Akiwakaribisha kiwandani hapo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Emmanuel Humba alisema wamefarijika sana na ujio wa Kamati kwani ni ishara ya kutambua juhudi zilizofanywa na wawekezaji hao watatu.

“Kiwanda hiki kama mlivyoona kinawahusu wananchi, wawekezaji tunaongeza nguvu tu, lakini watakaofanya kiwanda hiki kifanye kazi ipasavyo ni wananchi wenyewe.” Alisema.

Alitoa mfano kuwa wakati akiwa pale kiwandani alikutana na mkulima mmoja aliyeleta majani yake ya Chai kilo 15 na alionyesha furaha sana kwani alisema baada ya kuuza anauhakika wa kupata mahitaji mbalimbali ya nyumbani.

Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema, kusudio kubwa la kukifufua kiwanda ni kuwawezesha wananchi wa Lushoto, Bumbuli Korogwe na maeneo jirani kupata kipato na hivyo kuwainua kiuchumi kwani wengi wanategemea zao hilo.

“Tunategemea kwamba kiwanda kitanufaisha takriban asilimia 70 ya wakulima wa chai kutoka Lushoto, Bumbuli Korogwe na maeneo jirani," alifafanua Dkt. Mduma.

Akizungumzia hatua za utekelezaji wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya kiwanda hicho, Bw. Anselim Peter alisema awamu ya kwanza ya kufufua kiwanda hicho ilikuwa ni kukarabati majengo na mitambo ambayo ilikufa kabisa, wakati awamu ya pili ilikuwa ni kuboresha kiwanda kwa ujumla wake na kutengeneza menejimenti.

“ Karibu asilimia 100 kiwanda kimekamilika, tumeshaanza mchakato wa kuajiri wafanyakazi ili kusudi tunapoanza uzalishaji kamili tuweze kutekeleza majukumu ya kiwanda ipasavyo.” Alisema.

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mitaji ya Umma, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. George Malima (mwenye shati jekundu) wakiangalia hatua mbalimbali za uchakataji chai kwenye kiwanda cha Chai Mponde kilichoko Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga Oktoba 15, 2022

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mitaji ya Umma, wakipewa maelezo na Mwenyekiti w aBodi ya Kiwanda cha Chai Mponde, Bw. Anselim Peter kuhusu hatua mbalimbali za uchakataji chai kwenye kiwanda cha Chai Mponde kilichoko Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga Oktoba 15, 2022

Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Chai Mponde, Bw. Anselim Peter (kushoto) akitoa ufafanuzi mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mitaji ya Umma na Menejimenti za Mifuko ya WCF, PSSSF na Ofisi ya Msajili wa hazina kuhusu namna Boiler linavyofanya kazi wakati wa ziara ya Kamati kutembelea kiwanda cha Chai Mponde Oktoba 15, 2022

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini WCF, Bi. Rifai Mkumba (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma (wapili kulia) wakiwa na viongozi wa Kata ya Mponde.
 Meneja wa Kiwanda cha Chai Mponde, Bi.Sane Kwilabya (kulia) akionyesha jinsi ya kuyatambua majani ya chai yenye ubora mbele ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji, Mhe. George Malima (kushoto),  Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Kalist Lazaro (wapili kulia) na baadhi ya wajumbe wa kamati. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mponde, Bw. Anselim Peter.
Kutoka kulia, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini WCF, Bw. Emmanuel Humba, Msajili wa Hazina (TR) Bw. Mgonya Benedicto, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mitaji ya Uwekezaji wakiwa mbele ya boiler.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini WCF, Bw. Emmanuel Humba (aliyenyoosha mkono) akiwa na Makamu Mwenyekiti Bi. Rifai Mkumba (kushoto) Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma na watendaji wa WCF.
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma (mwenyekoti jeupe) na watendaji wengine wa Mfuko huo wakionyeshwa kitu na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Chai Mponde Bw. Temba Msemo 
Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Chai Mponde, Bw. Anselim Peter (kulia) na Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar (kushoto) wakimsikilzia Mkurgenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji WCF, Bw. Bezil Ewala.
Wakulima wakileta Chai kiwandani
Wakulima wakileta Chai kiwandani

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad