TAASISI ya
Bloomberg Media Initiative Africa (BMIA)
imetangaza kuanza kwa awamu ya
pili ya programu ya mafunzo ya uandishi wa habari za fedha (FJT) kwa waandishi
wa Tanzania. Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha waandishi wa habari wa fedha na
biashara kuandika habari za kina zinazohusu sekta hiyo.
Awamu hiyo ya pili inafanyika baada ya mafunzo hayo kusimama
kwa mikaa miwili kutokana na changamoto za ugonjwa wa Covid-19.
Mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shule Kuu
ya Biashara ya Strathmore(Strathmore Business School), Shule Kuu ya Biashara ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dar es Salaam Business School) na Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano ya Umma
ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (University of Dar es Salaam School of
Journalism and Mass Communication). Kurejewa kwa mafunzo hayo kunatokana na
mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu ya kwanza iliyofanyika 2019
ambapo waandishi wa habari 40 walipata taaluma mbalimbali kuhusiana na uandishi
wa habari za fedha na biashara.
Katika awamu ya pili kutakuwa na waandishi wa habari 50
kutoka vyombo vya serikali, sekta binafsi,taasisi zisizokuwa za kiserikali na
vyombo vikubwa vya habari. Imeelezwa kuwa mafunzo hayo ya miezi sita
yatazingatia mada mbalimbali zikiwamo uchambuzi wa data,soko la hisa,
uhasibu,sera, uchumi na hivyo kuwezesha mabadiliko ndani ya vyombo vya habari
ya namna ya kuandika habari za fedha na biashara.
Mafunzo hayo yatatolewa na waandishi wa habari wa Bloomberg
News na shule zilizotajwa.
Mafunzo kuhusu uandishi wa habari za fedha na biashara
nchini Tanzania yamelenga kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwajibikaji, uwazi na
utawala bora. Mafunzo hayo ni sehemu muhimu
na ya msingi kwa BMIA kuchangia maendeleo katika uandishi wa habari za
fedha na biashara barani Afrika, kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari
katika kuleta uwazi, uwajibikaji na utawala bora.
Akizungumzia taarifa hiyo Mkurugenzi BMIA, Erana Stennett, anasema:
“Tumefurahishwa na kurejea tena katika kutoa mafunzo ya programu baada ya miaka
miwili. Tunaamini kwa kuwapa waandishi wa habari ujuzi na maarifa ili kuripoti
vyema masuala ya biashara na fedha tunachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
Tanzania.”
Akizungumza katika uzinduzi huo, Gavana wa Benki Kuu (BoT)
Profesa Florens Luoga alisema: “Katika kipindi hiki kigumu baada ya janga la
corona, uandishi thabiti wa habari za kibiashara na kiuchumi ni msingi mkubwa
wa kuweza kuwafahamisha wadau ili kuweza kuwa na msukumo mkubwa wa ukuaji wa
uchumi. Kwa kutoa mafunzo kwa wanahabari zaidi, BMIA inachangia maendeleo ya
kiuchumi ya Tanzania.”
Kuzinduliwa kwa awamu ya pili nchini Tanzania kunafuatia
kuwapo kwa mafanikio makubwa ya programu hiyo kwa nchi za Kenya, Nigeria,
Afrika Kusini, Ghana, Zambia, Côte d’Ivoire na Senegal, ambapo zaidi ya
waandishi 600 wamekamilisha mafunzo hayo.
Tangu kuzinduliwa kwa programu hiyo mwaka 2014, BMIA
imewafikia wadau 1,000 barani Afrika. BMIA pia imedhamini mikutano minne
iliyokutanisha wamiliki wa vyombo vya habari na viongozi waandamizi mkatika
masuala ya biashara, serikali na vyama vya kiraia.
No comments:
Post a Comment