Mahakamani : Mabishano makali yaibuka kesi ya Sabaya - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Saturday, 3 July 2021

Mahakamani : Mabishano makali yaibuka kesi ya Sabaya


Lengai Ole Sabaya akipelekwa kwenye chumba cha mahabusu kilichopo mahakama ya hakimu mkazi Arusha.

Na Grace Macha, Arusha.

KESI inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne imeshindwa kuendelea baada ya ya shahidi wa upande wa jamhuri kupata udhuru.
Aidha washitakiwa wawili, Jackson Macha, (29), na Nathan Msuya, wameongezwa kwenye shauri hilo la jinai namna 66 la unyang'anyi wa kutumia silaha.
Pia, yameibuka mabishano ya kisheria baina ya mawakili wa pande zote baada ya mawakili wa utetezi kutaka wapatiwe idadi ya mashahidi na vielelezo.
Mabishano hayo yaliibuka Junai 2,2021baada ya wakili wa Serikali,  Tarsila Gervas kuiomba  mahakama ya hakimu mkazi Arusha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mshasha anayesikiliza shauri  kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza kesi  kwani shahidi waliyemtegemea asingeweza kufika.

"Mheshimiwa shauri hili lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini nipende kuitaarifu mahakama hii upande wa jamhuri utashindwa kuendelea na shauri hili kwa sababu shahidi tuliyekuwa tunamtegemea kidogo amepata udhuru," wakili Tarsila aliiomba mahakama.
Hoja hiyo iliwaibua mawakili wa utetezi, Mosses Mahuna akiomba kupatiwa maelezo ya walalamikaji wengine kwemne shauri hilo huku wakili, Dancan Oola, akiomba wapatiwe idadi ya mashahidi na vielelezo.
"Kwa nini hakuomba samasi siku waliposoma maelezo ya awali? Mheshimiwa hakimu nachotaka kuomba tusipotezeane muda mapema hivi. Tumejiandaa kwa ajili ya kusikiliza kesi halafu tunaambiwa shahidi tuliyetegemea ina maana mtu mmoja anaweza kukwamisha kesi? tunaomba kitu kama hiki kisijirudie," aliomba wakili Oola.

Akijibu hoja hizo wakili wa serikali, Tarsila alisema kuwa amesikia malalamiko na madukuduku ya mawakili wa utetezi ambapo aliwahakikishia kuwa Julai 16, mwaka huu watakuwa na mashahidi na kesi itaendelea.
"Kuhusiana na mashahidi ni namna gani tuwalete ni jukumu letu sisi ndiyo wenye kesi ndiyo tunajua ni yupi aje hata tukiwa nao 20 hawawezi wakatueleza namna gani tuwalete wote kwa namna wanavyotaka wao," alisisitiza wakili Tarsila.

Alisema kama ni haki inapaswa kutendeka kwa washitakiwa na kwa jamhuri huku akisisitiza sheria haiwalazimishi kuwataja mashahidi ambapo amenukuu vipengele mbalimbali vya kisheria. 

Wakili Tarsila akijibu hoja ya wakili wa utetezi Mahuna aliyetaka kupatiwa nakala za maelezo ya walalamikaji wote kwenye shauri hilo alisema kuwa shauri hilo lina mlalamikaji mmoja tu, Bakari Msangi ambaye maelezo yake aliyoandika polisi walishampatia wakili wa utetezi hao wengine wanaoonekana kwenye shauri hilo walijitokeza wakati wa upelelezi.

 Hakimu aliingilia kati pale wakili wa utetezi, Mahuna alipotaka kusimama ili kujibu hoja hizo kwa kumweleza kuwa wote hapo ni wanasheria hakuna sababu ya kuwa na maneno mengi juu ya suala hilo hivyo kesi iendelee.
Lengai Ole Sabaya na washitakiwa wenzake wakielekea kwenye basi la magereza tayari kurejea mahabusu kwenye gereza la Kisongo

Shauri hilo limeahirishwa mpaka Julai 16, mwaka huu litakaporudi kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa ambapo washitakiwa wote wamerudishwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo.
Awali juni 18, mwaka huu washitakiwa hao walisomewa maelezo ya awali ambapo mahakama hiyo ilielezwa namna Sabaya na washitakiwa wenzake walivyotumia bunduki kuwatisha watu waliokuwa kwenye duka la Shaad  kisha wakamfunga pingu Diwani wa Sombetini, Bakari Msangi, (CCM) na kumuibia shilingi 390,000.

Aidha inadaiwa kuwa waliwatisha watu hao kuwa watawavyatulia  risasi endapo wangeshindwa kueleza alipo mmiliki wa duka hilo, Mohamed Saad.

Wakili wa Serikali, Tarsila aliieleza mahakama hiyo kuwa Februari 9, mwaka huu washitakiwa hao Sabaya, Sylvester Nyengu, Daniel Mbura, Jackson Macha, (29), na Nathan Msuya,  walivamia duka la Shaad lililopo mtaa wa biashara jijini Arusha.

"Walipofika waliwalazimisha watu wote kulala chini kwenye sakafu huku wakiwapiga kwa kutumia mateke, ngumi pamoja na makofi," Wakili wa Serikali Tarsila aliieleza mahakama nankuongeza. 

...Mshitakiwa wa kwanza, (Sabaya) aliwanyooshea bunduki wote huku akiwatisha kwamba atawafyatulia risasi kama wakishindwa kumweleza anayemiliki duka hilo yuko wapi...

..Lakini hawakumpatia jibu na badala yake mshitakiwa namba moja alimfunga kwa pingu mmoja wa watu waliokuwa katika duka hilo ambaye anaitwa Bakari Rahibu Msangi ambaye ni diwani wa kata ya Sombetini...

....Na akiwa ameshika silaha, bunduki ameshika mkononi alimtesa na kumtisha kumuua (Msangi) kwa kuwa alikuwa akitishia kuingilia biashara zake alizokuwa akifanya mahali hapo,". 

Wakili Tarsila aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa washitakiwa wote kwa pamoja waliwapekua watu waliokuwa kwenye duka hilo huku wakiwa wamewashikia silaha ambayo ilikuwa ni bunduki na waliweza kuchukua fedha taslimu kutoka kwa Bakari Rahibu Msangi kiasi cha shilingi 390,000.

Pia walichukua simu aina ya tecno moja  na fedha taslimu shilingi 35,000 kutoka kwa Ramadhani Ayoub Rashid ambaye pia alikuwa ni mhanga aliyekuwa katika duka hilo.
"Baada ya kufanya unyang'nyi wa kutumia silaha waliondoka tukio hilo lilitolewa taarifa kwenye kituo cha polisi upelelezi ulifanyika kutokana na vitendo hivyo vya kifedhuli walivyofanya dhidi ya wahanga na watuhumiwa hawa waliweza kukamatwa maeneo tofauti ndani mkoa wq Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam," wakili huyo wa serikali aliieleza mahakama.

Alidai kuwa  wakati washitakiwa hao wanafanyiwa mahojiano na polisi walikubali siku hiyo ya tarehe 9, februari, 2021 walikuwa kwenye duka hilo la Mohamed Saad ambapo baadaye waliletwa mbele ya  mahakama hiyo kwa makosa yanayowakabili.

Washitakiwa wote walikana maelezo hayo isipokuwa walikubali kuwa waliletwa mbele ya mahakama shauri hilo limeahirishwa mpaka Julai 16, mwaka huu litakaporudi kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

KESI YA UHUJUMU UCHUMI

Kesi ya  inayomkabili  Ole Sabaya wenzake wanne ilishindwa kuendelea mahakamani hapo baada ya upande wa jamhuri kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Wakili wa Serikali,  Tarsila Gervas aliiomba  mahakama ya hakimu mkazi Arusha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mshasha kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo la uhujumu uchumi namba 27/2021 ambapo litarudi kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa wengine ni msaidizi binafsi wa DC Sabaya, Sylivester Nyengu, (26) maarufu kama Kicheche, Enock Mnekeni, (41), Watson Mwahomange, (27) maarufu kama Maliamungu, John Aweyo maarufu kama Mike one na Daniel Mbura, (38).

Wakili wa Utetezi, Mahuna alieleza mahakama hiyo kuwa hana pingamizi na ombi hila isipokuwa anaomba apatiwe nakala ya hati ya mashitaka kwani hiyo ni mara yake ya kwanza amefika mahakamani kwa ajili ya kuwawasikilisha wateja wake.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Chavula alisema watampatia ila akaiomba mahakama kama inayo nakala wampatie jambo ambalo hakimu aliridhia hivyo akampatia nakala hiyo.
Awali Juni 4,mwaka huu Sabaya na wenzake watano walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa saba mchana chini ya ulinzi mkali kisha wakasomewa mashitaka yao mbele ya mahakaimu wawili tofauti kisha wakarudishwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo kutokana na kesi zinazowakabili kutokuwa na dhamana.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mashitaka, Kweka aliieleza mahakama hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Martha Mahumbuga kuwa shitaka la kwanza ilidaiwa Ole Sabaya kuongoza genge la uhalifu kinyume cha sheria akishirikiana na washitakiwa wengine ambao si mtumishi wa umma 

ilidaiwa kuwa  mnamo Januari 20, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha Sabaya akiwa ni ofisa wa umma, mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro alikiuka majukumu yake ya kiofisi kwa pamoja akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu.
 
"Kwa kujua na kwa malengo ambayo si halali kwa kutumia mamlaka yake kama afisa wa umma huyu mshitakiwa wa kwanza walijipatia manufaa ambayo ni kinyume cha sheria," Kweka aliieleza mahakama.

Katika shitaka la pili na tatu yanamkabili Sabaya peke yake ambapo anadaiwa kushiriki matukio ya rushwa ambapo mnamo Januari 20, mwaka huu katika maeneo ya jiji la  Arusha alishiriki vitendo vya rushwa kwa kumshawishi Francis Mrosso ampatie fedha kiasi cha shilingi milioni 90 kwa kumahidi kwamba atamsaidia kuweza kuepuka vitendo vya jinai vilivyokuwa vinamkabili ambavyo vilikuwa ni vya ukwepaji wa kodi.

Kweka aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa katika shitaka la tatu Sabaya anadaiwa kuwa mnamo Januari 20, mwaka juu kwenye maeneo ya Mrombo jijini Arusha alipokea rushwa ya kiasi cha shilingi milioni 90 kutoka kwa Mrosso kwa maelezo kuwa angemsaidia kukwepa vitendo vya kijinai alivyodaiwa kukabiliwa navyo vya ukwepaji kodi .

 Katika shitaka la nne  linalowalabili washitakiwa wote watano ni la utakatishaji wa fedha haramu ambapo Ole Sabaya akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu ambapo wanadaiwa januari 20, mwaka huu huko maeneo ya Kwamorombo, Jijini Arusha walijipatia kiasi cha shilingi milioni 90 wakati wakijua kuwa kujipatia fedha hizo ambazo ni mazalia ya uhalifu ilikuwa ni mwendelezo wa kosa la vitendo vya rushwa.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo ambapo upande wa jamhuri uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo kwani upalelezi bado haujakamilika.

Shauri hilo limeahirishwa mpaka Julai 16, mwaka huu litakapokuja kwa ajili ya kutajwa washitakiwa wote wamerejeshwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo.

No comments:

Post a Comment