Utalii : Hifadhi ya Mikumi Yaiomba Serikali Kuchepusha Barabara ya Lami Inayopita Ndani ya Hifadhi Hiyo - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


15 Feb 2018

Utalii : Hifadhi ya Mikumi Yaiomba Serikali Kuchepusha Barabara ya Lami Inayopita Ndani ya Hifadhi Hiyo



Na Hamza Temba-WMU-Morogoro
................................................................
Serikali inafikiria namna bora ya kubadilisha uelekeo wa eneo la kilometa hamsini za barabara ya lami inayopita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi au kutoza kodi ya utalii kwa watu wanaotumia barabara hiyo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazosabishwa na barabara hiyo kwenye uhifadhi.

Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kufuatia ombi la uongozi wa hifadhi hiyo la kuiomba Serikali kuchepusha barabara hiyo kutokana na athari mbalimbali za kimazingira zinazosabishwa na uwepo wa barabara hiyo ndani ya hifadhi hususan vifo vya mara kwa mara vya wanyamapori, ujangili na ukosefu wa mapato ya Serikali.

Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo mbele ya Waziri Kigwangalla, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald Mono alisema licha ya barabara hiyo kuwa na fursa nyingi za kimaendeleo imekuwa na changamoto nyingi kwenye uendeshaji wa shughuli za uhifadhi.

Alisema wastani wa mnyamapori mmoja hugongwa na gari kila siku katika barabara hiyo ambapo takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2014 idadi ya wanyamapori waliogongwa walikuwa 351, mwaka 2015 walikuwa 361 na mwaka 2016 walikuwa 218.

Alisema changamoto nyingine ni uchafuzi wa mazingira ambapo wastani wa taka ngumu zisizopungua kilo 138.3 huzalishwa kila siku na watumiaji wa barabara hiyo.

Mbali na changamoto hizo alisema nyingine ni ukosefu wa mapato ya Serikali kufuatia kukosekana kwa mageti ya kulipia tozo za utalii kwa watumiaji wa barabara hiyo ambao hufaidi utalii wa bure na kuikosesha Serikali mapato.

Alisema Changamoto nyingine ni ujangili ambao huchochewa na uwepo wa barabara hiyo ambayo hutoa fursa kwa majangili kuingia katika hifadhi hiyo kiurahisi kwa njia mbalimbali ikiwemo magari na pikipiki.

“Hifadhi inaiomba Serikali kuchepusha barabara hii ili kupunguza changamoto hizi zinazotokana na uwepo wa barabara husika na kuongeza mapato ya Hifadhi kwa kuzuia utalii a bure unaofanywa na watumiaji wa barabara wa ndani na nje,”. Alisema Kaimu Mhifadhi Mkuu huyo wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema changamoto kubwa aliyoiona katika hifadhi hiyo ni namna ya watalii kufika na kufanya shughuli za utalii katika hifadhi hiyo.

Alisema licha ya uwepo wa barabara ya lami inayokatiza hifadhini hapo, barabara hiyo sio rafiki kwenye uhifadhi. “Kuna hiyo barabara ambayo inaleta watalii hapa, ni barabara ambayo iko bize sana, ni barabara ya kitaifa na kwa vyovyote vile hii sio barabara mahsusi kwa ajili ya shughuli za utalii.

“Sisi (Serikali) tunatafakari namna ya aidha kuiondoa hiyo barabara au namna ya kuwachaji watu wanaokatiza hizi kilometa hamsini ambazo zipo ndani ya hifadhi ya Mikumi,” alisema Dk. Kigwangalla.

Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla amemtaka muwekezaji aliyepewa hoteli ya kitalii ya Mikumi Wildlife Lodge iliyopo ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ukarabati na uendelezaji kuhakikisha anakamilisha makubaliano hayo ndani ya muda aliyopewa kwa mujibu wa mkataba aliosaini na TANAPA ama sivyo atanyang’anywa kibali hicho.

Akizungumzia jitihada za kuimarisha ulinzi wa hifadhi hiyo, Dk. Kigwangalla amesema Serikali inakusudia kuharakisha mchakato wa kuanzishwa kwa jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Kidoma itakayojumuisha vijiji vya Kilangali, Doma na Maharaka ili kutengeneza buffer na hatimaye kuimarisha uhifadhi shirikishi.

Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ilianzishwa mwaka 1964 kwa Tangazo la Serikali Na. 465 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 1,070. Mwaka 1975 Serikali iliona umuhimu wa kuongeza eneo upande wa kusini na kaskazini mwa Hifadhi na kufikia ukubwa wa kilometa za mraba 3,230 kwa tangazo la Serikali Na. 121.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongea na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro. Uongozi wa hifadhi hiyo umeiomba Serikali kuchepusha barabara ya lami inayopita ndani ya hifadhi hiyo kutokana na athari mbalimbali za kimazingira zinazosabishwa na barabara hiyo ikiwemo vifo vya wanyamapori, ujangili na ukosefu wa mapato ya Serikali unaotokana na watu kufaidi utalii wa bure. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua maziringira ya jengo lililoungua moto la Mikumi Wildlife Lodge ambalo linalofanyiwa ukarabati wakati wa ziara yake ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi jana mkoani Morogoro ambapo amemtaka muwekezaji aliyepewa hoteli hiyo kuikarabati ndani ya muda aliopewa ama sivyo atanyang’anywa kibali alichepewa. Kushoto kwake ni Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald Mono. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa  na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono kukagua mazingira ya hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo  kutoka kwa Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia mazingira mwanana ya  Hifadhi ya Taifa ya Mikumi wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro.
Picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad