Matukio : Mabaraza ya Madiwani Simiyu Yaridhia kukopa Bilioni 17.1 Kutekeleza miradi ya Maendeleo - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Monday, 23 October 2017

Matukio : Mabaraza ya Madiwani Simiyu Yaridhia kukopa Bilioni 17.1 Kutekeleza miradi ya Maendeleo



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (katikati) akizungumza na Madiwani na baadhi ya wakulima Bonde la Mwamanyili wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega (hawapo pichani) katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika Nyashimo kwa lengo la kujadili suala la maombi ya mkopo kwa ajili kutekeleza Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili Wilayani humo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mhe.Vumi Magoti(wa pili kulia)akizungumza na Madiwani na baadhi ya wakulima wa Busega(hawapo pichani) katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Nyashimo kwa lengo la kujadili maombi ya mkopo kwa ajili kutekeleza Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili Wilayani humo
Madiwani na baadhi ya Wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu wakifuatilia mjadala kuhusu suala la maombi ya Mkopo kwa ajili ya Upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa Wilayani Meatu katika kikao cha dharura cha Baraza kilichofanyika Mjini Mwanhuzi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Busega (meza kuu) na baadhi ya wakulima baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwa lengo la kujadili suala la maombi ya mkopo kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili wilayani humo.

Na Stella Kalinga, Simiyu
Mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Meatu Mkoani Simiyu yameridhia Halmashauri hizo kukopa shilingi bilioni 17.1 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kwa ajili ya kutekeleza Miradi mikubwa miwili ya Maendeleo.

Maridhiano hayo yamefikiwa katika Vikao vya dharura vya mabaraza ya madiwani vilivyofanyika kwa nyakati tofauti, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Busega imepanga kukopa shilingi bilioni 10.7 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili (eneo la ekari 2050) na Meatu shilingi bilioni 6.4 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha maziwa(MEATU MILK).

Akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Mpango wa Kilimo cha Umwagiliaji Wilayani Busega, Afisa Mipango wa Wilaya hiyo Josephat Joseph, amesema hadi sasa kazi za upimaji wa mashamba na njia ya kupita bomba la maji, kupima udongo, kusanifu mfereji mkuu kwenye chanzo, sehemu ya kuchukulia maji, nyumba za pampu, mifereji ya kuingiza na kutolea maji,kuandaa michoro na gharama za mradi zimeshakamilika.

Aidha, amesema katika utekelezaji wa mradi huu Halmashauri ndiyo msimamizi mkuu wa mradi na itajenga miundombinu yote ya umwagiliaji, hivyo itaingia makubaliano na wakulima wa Mwamanyili kupitia umoja wao watakaounda katika kutekeleza shughuli za mradi.

Nao wakulima wa Bonde la Mwamanyili wamesema wameupokea mradi huo kwa mikono miwili na kwa sasa wamesitisha shughuli zote za Kilimo katika bonde hilo, ili kupisha shughuli nyingine za maandalizi ya ujenzi wa miundombinu ya mradi huo.

“ Tunawashukuru viongozi wetu kwa kutusaidia kupata mkopo wa kutekeleza mradi huu naupokea kwa mikono miwili tena natamani uanze haraka, sasa hivi hatutalima maeneo yetu tunapisha wataalam waendelee na shughuli za maandalizi ya mradi ili wakikamilisha tu tuanze ” alisema Joseph Mayala.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema kutekelezwa kwa mradi huo, kutaiandikia historia wilaya ya BUSEGA kwa kuwainua wananchi kiuchumi na kuondokana na aibu ya kuomba chakula cha msaada Serikalini, ambapo amesisitiza kuwa utakuwa mradi wa pekee ambao mnyororo wake wa thamani utaonekana kupitia mazao yatakayolimwa hususani mpunga.

Kwa upande wa Mradi wa Upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa Meatu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza amesema kuelekea upanuzi wa kiwanda hicho, Halmashauri imekusudia kuongeza idadi ya wafugaji wanaopeleka maziwa kiwandani kutoka 45 wa sasa na kufikia wafugaji 400 wakubwa ambao wanafuga ng’ombe wa kisasa.

Mikakati mingine ni kununua mtambo mpya wa kuchakata maziwa wenye uwezo wa kuchakata lita elfu 15,000 kwa siku, kununua Mitamba 1000 na kuandaa shamba la malisho lenye miundombinu muhimu pamoja na kuongeza soko la MEATU MILK kwa kuingia mikataba na mawakala na kuweka maduka katika baadhi ya miji mikubwa.

Wafugaji wa Wilaya ya Meatu wamesema wameupokea mradi wa upanuzi wa kiwanda cha maziwa wilayani humo kwa furaha, kwani utawasaidia kuongeza upatikanaji wa soko la uhakika la maziwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe.Pius Machungwa ametoa wito kwa wafugaji kukubali kubadilika na kuanza kufuga kisasa kulingana na jinsi wanavyoshauriwa na wataalam ili kuongeza tija
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Serikali mkoani humo imejipanga kutafuta majawabu ya changamoto za wafugaji kwa kuwasaidia kufuga kisasa, ikiwa ni pamoja na kuwashauri kupima maeneo yao na kuyawekea miundombinu muhimu kama mabwawa, visima, majosho na mashamba ya malisho.

“Kiwanda mnachokihitaji hapa kitatumia lita 15,000 kwa siku, mnapaswa kuweka mikakati mizuri ya ng’ombe wenu ili muwe na uhakika wa maziwa, nayazungumza haya ili kila mmoja aone umuhimu wa kiwanda; tuwasaidie wafugaji wafuge kisasa na kwa tija” alisema Mtaka

Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Meatu zinatarajia kupata Mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambayo imekubali kutoa mikopo hiyo ili kuunga mkono juhudi za Viongozi na wananchi wa mkoa wa Simiyu katika kuleta maendeleo.

No comments:

Post a Comment