Matukio : Wananchi Waliopewa Uraia Watakiwa kuheshimu Sheria za Nchi - Waziri Mkuu Majaliwa - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


12 Aug 2017

Matukio : Wananchi Waliopewa Uraia Watakiwa kuheshimu Sheria za Nchi - Waziri Mkuu MajaliwaWaziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa CUF Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya Agosti 11. 2017, Waziri Mkuu yupo wilayani Kaliua kwa ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo katika Mkoa wa Tabora

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea na wananchi wa kitongoji cha Mwamnange kilichopo Wilaya ya Kaliua leo Agosti 11, 2017 .Wananchi hao walisimamisha msafara wake ili kumuomba serekali iwasaidie kupata umeme.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihotubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Veta Jimbo la Ulyankulu wilayani Kaliua mkoani Tabora leo August 11, 2017, ambapo amewataka wananchi waliopewa uraia kuheshimu sheria za nchi vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu waache kujihusisha na matukio ya uhalifu.

Ametoa onyo hilo leo mchana (Ijumaa, Agosti 11, 2017) wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa tarafa ya Ulyankulu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya VETA, wilayani Kaliua mkoani Tabora.

Amesema matukio ya ujambazi, mauaji na umiliki wa silaha yanayofanyika kwenye tarafa hiyo ni mengi ikilinganishwa hali ilivyo kwenye maeneo mengine ya mkoa huo.

"Taarifa nilizonazo zinaonyesha katika kipindi cha miaka miwili kumekuwa na matukio ya mauaji 35, ujambazi matukio 12, umiliki wa silaha nao unatisha. Yamekamatwa magobole 11, bunduki aina ya SMG saba na Mark Four mbili."

"Tulikamata pia risasi 714 za SMG zikiwa kwenye ndoo za mafuta na juu yake wamepaka mafuta ya mawese. Pia risasi mbili za Mark Four zilikamatwa," amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amewataka wakazi hao ambao baadhi yao wamepewa uraia na wengine bado ni wakimbizi waonyane wanapokutana kwenye vikao vyao kwa sababu matendo yao yanaikwaza Serikali ambayo iliamua kuwapa hifadhi. "Ni vema mkikutana kwenye vikao vyenu muelezane na kuonyana," amesema Waziri Mkuu.

"Ninawasihi matukio haya myadhibiti la sivyo mtaharibu nia njema iliyoleta uwepo wenu. Bunduki na risasi zinakuja kufanya nini wakati nyie mko maeneo salama? Mauaji ya nini? Kama kuna tatizo limekupata, muone mwenyekiti wa kijiji, atakusaidia," alisisitiza.

Alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi yao ambao wamegeuka mawakala na wameanza kuwaleta ndugu zao bila kufuata utaratibu. "Hatuzuii mtu kutembelewa na ndugu yake, lakini ni lazima mfuate taratibu. Tunataka tudumishe amani iliyopo nchini lakini pia tudumishe urafiki wa nchi zetu mbili za Burundi na Tanzania," aliongeza.

Mapema, Mbunge wa jimbo la Ulyankulu, Bw. John Kadutu alimuomba Waziri Mkuu afuatilie suala la upatikanaji wa maji kwenye tarafa hiyo, pia aliomba wasaidiwe ili kata tatu za Kanindo, Igombenkulu na Milambo ziwezeshwe kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Post Top Ad