Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Diwani wa kata ya Murriet kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kredo Kifukwe ametangaza kujiuzulu rasmi katika Nafasi ya Udiwani wa kata hiyo iliyoko Wilaya ya Arusha mkoani Arusha .
Kredo ameeleza kuwa ameamua kuchukua uamuzi huo ili aweze kutumikia jamii kama raia mwema bila kuegemea upande wowote kisiasa lakini pia amesema kuwa juhudi zinazofanywa na Raisi John Pombe Magufuli zimemfanya ajiuzulu kwani haoni sababu ya kuendelea kumpinga kutokana na kazi nzuri anayoifanya ya kulitumikia taifa bila kujali itikadi za kisiasa.
Diwani huyo aliyejiuzulu amesema kuwa kwa sasa hana mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa kwani ataendelea kuwa raia mwema na kuitumikia jamii yake pamoja na taifa huku akiendelea kuunga mkono juhudi za Rais.
Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Arusha Injinia Gaston Pascal amethibitisha kupokea taarifa za kujiuzulu kwa diwani huyo ambaye aliwasilisha barua ya kujiuzulu katika Ofisi za Mkurugenzi kwa mujibu wa sheria hivyo watafikisha taarifa kwa tume ya uchaguzi ili uchaguzi uweze kufanyika kuziba pengo hilo.
No comments:
Post a Comment