ESTOM SANGA-TASAF
Wadau wa maendeleo wanaochangia fedha za utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF nchini wameonyesha kuridhishwa na kasi ya kupambana na umaskini kupitia mpango huo ulioanza kutekelezwa takribani miaka minne iliyopita.
Wadau hao wa maendeleo kutoka nchi na mashirika kadhaa ya misaada ya kimataifa wameonyesha kuridhishwa na namna walengwa wa Mpango huo wa kunusuru kaya maskini wanavyotumia fedha za ruzuku katika kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi inayowaongezea kipato na kuwawezesha kuboresha maisha hususani katika sekta za elimu,afya na kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba za kudumu.
Wadau hao wa maendeleo ambao wako kisiwani Zanzibar kuona namna walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini wanavyonufaika na shughuli za Mpango huo,wametembelea shahia ya Potoa kaskazini Unguja ambako wamekutana na walengwa wa Mpango huo na kujionea shughuli walizozianzisha kwa kutumia fedha ya ruzuku inayotolewa na serikali kupitia TASAF ikiwemo uundaji wa vikundi vya ususi wa vikapu,mikeka na mapambo mbalimbali ya nyumbani .
Aidha wadau hao wa maendeleo wameshuhudia namna walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika shehia ya Potoa walivyoanzisha kitalu cha miche ya matunda na miti chenye jumla ya miche 40,000 chini ya utaratibu wa TASAF wa kuwapa fursa walengwa wake kuibua miradi na kuitekeleza wakati wa kipindi cha hari na kisha kuwalipa ujira ili kuwaongezea kipato.
Walengwa hao wamewaeleza wadau hao wa maendeleo kuwa licha ya kuiuza miche hiyo ,lakini pia huipanda kwenye maeneo yao kama njia mojawapo ya kutunza mazingira na kujiongezea kipato na pia kuongeza ujuzi wa namna ya kuotesha miche na kuitunza kitaalam kinyume na hali ilivyokuwa kabla ya kuanza kwa Mpango huo katika shehia yao.
Mwakilishi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia, Bwana Muderis Mohamed amesema kasi ya walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini nchini Tanzania ni ya kuvutia na kutia matumaini makubwa ya kupunguza umaskini miongoni mwa walengwa kutokana na mwitiko mzuri wanaouonyesha katika matumizi ya fedha na uanzishaji wa miradi midogo midogo ya kiuchumi kama ufugaji wa bata, kuku na hata mbuzi kwa kutumia fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali kupitia TASAF.
Picha ya kwanza nay a pili chini wadau wa maendeleo wakiangalia baadhi ya vifaa vilivyotengenezwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini wa eneo la Potoa kisiwani Zanzibar.
Mmoja wa wadau wa maendeleo hakusita kununua kikapo kutoka kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini baada ya kuvutia na kazi hiyo ya mikono. Kikapo kimoja huuzwa kwa takribani shilingi 15,000 hadi 20,000.
Mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini katika shehia ya Potoa kisiwani Zanzibar bi. Munono Mohamed (wa pii kushoto) akizungumza na baadhi ya wadau wa maendeleo juu ya hatua yake ya kujenga nyumba kwa kutumia ruzuku ya fedha kutoka TASAF. Picha ya chini ni nyumba anayoendelea kuijenga Bi. Munono mama wa watoto SABA.Aliyeshika daftari ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga.
Wadau wa Maendeleo wa TASAF, wakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika eneo la Potoa Bi. Panga Makame juu ya mradi wa kufuga bata aliouanzisha baada ya kupata ya kupata ruzuku. Bata mmoja huuzwa kwa takribani shilingi elfu 30.
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini katika shehia ya Potoa wameanzisha kitalu cha miche ya matunda na miti kupitia utaratibu wa ajira ya muda ambao ni sehemu ya Mpango huo wenye lengo la kuongezea kipato hususani wakati wa kipindi cha hari.
Wadau wa Maendeleo wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini katika shehia ya Potoa kisiwani Zanzibar.
No comments:
Post a Comment