Mwenyekiti wa Soko la Gezaulole lililopo Kiwalani Bomu bomu, Muhidin Waziri 'Ndolanga' akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu changamoto iliyokuwepo katika soko hilo juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo hivi sasa vimedhibitiwa baada ya kupata mafunzo kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG). Kulia ni Mwezeshaji wa Kisheria wa soko hilo.
Mwezeshaji wa Kisheria katika soko hilo, Amina Mussa
akizungumza na wanahabari.
Mfanyabiashara katika soko hilo, Zena Mohamed akielezea wanawake kupiga hatua ya maendeleo baada ya kupata mafunzo hayo yaliyotolewa na EfG.
Wanawake wakipata mahitaji mbalimbali katika soko hilo.
Mteja akinunua bamia.
Mfanyabiashara, Mzee Mohamed Bawe akisubiri wateja.
Mfanyabiashara Mwantum Mohamed akizungumza na waandishi (hawapo pichani ), kuhusu kupungua kwa vitendo vya ukatili katika soko hilo la Gezaulole.
Mfanyabiashara wa kisamvu katika soko hilo, Asna Andrew (katikati), akitwanga kisamvu tayari kwa kukiuza. Alisema ushirikiano baina ya wafanyabiashara na viongozi umeleta tija ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mfanyabiashara wa Soko la Tabata Muslim, Sauda Kalengela akizungumza kupungua kwa ukatili wa kijinsia.
Muuza samaki wa kukaanga katika Soko la Tabata Muslim, Anthony Venance akionesha miundombinu mibovu katika soko hilo. Katika masoko kukikosekana miundombinu mizuri wakati Manispaa zinazosimamia masoko hayo zikitoza ushuru bila kukarabati miundombinu hiyo pia ni ukatili wa kijinsia kwa wanatumiaji wa masoko hayo.
Mwezeshaji wa kisheria katika soko la Tabata Muslim, Aisha Juma akizungumzia ukatili wa kijinsia aliofanyiwa mwanaume mmoja katika maeneo ya Tabata ya kuporwa vyombo vyake na mke wake.
Mwezeshaji wa kisheria katika soko la Tabata Muslim, Irene Daniel akizungumzia wanawake katika soko hilo kujitambua na kushika nafasi mbalimbali za uongozi baada ya kuwezeshwa na EfG.
Na Dotto Mwaibale
WANAWAKE Wafanyabiashara katika masoko jijini Dar es Salaam hasa yale yaliyowezeshwa mafunzo na Shirika la Equality for Growth (EfG) wamejitambua na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika maeneo yao ya biashara.
Hayo yamebainishwa na Mwezeshaji wa Kisheria katika Soko la Tabata Muslim, Irene Daniel wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu faida waliyoipata baada ya kupata mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia katika masoko kupitia Shirika la Equality for Growth (EfG)
"Kwa kweli wanawake hivi sasa tupo imara, tunajitambua na tunauthubutu baada ya kupata dozi kutoka EfG kwani hapo awali tulikuwa waoga na hatukuzijua haki zetu ndio maana tulikuwa nyuma kimaendeleo" alisema Daniel.
Alisema baada ya kupata mafunzo hayo na kuwezeshwa kuzijua sheria na mambo yaliyokuwa yakimdhalilisha mwanamke hali imekuwa shwari katika masoko kwani hivi sasa wanafanya biashara zao katika mazingira salama.
Alisema kutokana na hali hiyo wanawake wameweza kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuwa wajumbe katika kamati za masoko jambo ambalo ni la kujivunia.
"Tuna kila sababu ya kulishukuru shirika hilo kwani sasa tumeweza kufungua akaunti zaidi ya moja baadhi yetu wamefanikiwa kununua hata magari na tunaendelea na biashara zetu bila ya kuwepo vitendo vya udhalilishaji kama ilivyokuwa siku za nyuma" aliongeza Daniel.
Mfanyabiashara mwingine katika soko hilo ambaye pia ni Mwezeshaji wa Kisheria Aisha Juma alisema mafunzo hayo waliyopata ya uwezeshaji wa kisheria yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia masokoni na hata majumbani.
Alisema elimu hiyo waliyoipata kupitia EfG imesaidia sana kuweka mambo sawa na ushirikiano baina yao katika masoko kwani leo hii hakuna mtu wa kumnyanyasa mwenzake kutokana na jinsia yake na anayebainika amekuwa akichukuliwa hatua.
Akitolea mfano alisema ukatili wa kijinsia hafanyiwi mwanamke peke yake kwani yeye ameweza kusimamia moja ya kesi ya ukatili wa kijinsia aliofanyiwa mwanaume mmoja maeneo ya Tabata baada ya kuporwa vitu vyake vya ndani na mke wake ambaye alisaidiana na mama yake licha ya vitu hivyo kununua mwanaume huyo.
Mfanyabiashara katika Soko la Gezaulole lililopo Kiwalani Bomubomu, Mwantum Mohamed alisema wanawake katika soko hilo wana nguvu ya pamoja jambo lililosaidia kuondoa kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia,
Mwenyekiti wa Soko hilo, Muhidin Waziri 'Ndolanga' alisema faini ya sh.10,000 anayotozwa mtu atakayebainika kutoa lugha ya matusi au kumdhalilisha mtu yeyote kwenye soko hilo imesaidia kuwatsha watu wenye nia ya kutenda kosa hivyo kulifanya soko hilo kuwa eneo salama la kutafuta riziki na si matusi.
Shirika hilo liliendesha mafunzo na kufanya kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia katika masoko ya Ferry, Temeke Sterio, Tabata Muslim, Gezaulole, Kisutu na Ilala Mchikichini yote yakiwa jijini Dar es Salaam ambapo kampeni hiyo pia inafanyika katika Mikoa ya Mwanza na Tanga.
No comments:
Post a Comment