Zanzibar : Dkt Shein aweka jiwe la msingi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyopo huko Mazizini, Wilaya ya Mjini, Unguja - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


7 Jan 2017

Zanzibar : Dkt Shein aweka jiwe la msingi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyopo huko Mazizini, Wilaya ya Mjini, Unguja






Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameweka jiwe la msingi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali na keleza kuwa bado kuna tatizo la ukusanyaji, utumiaji na uhifadhi wa takwimu hapa nchini hivyo kuna haja ya kuwekwa mfumo madhubuti katika kuondoa hitilafu hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo, katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kuweka jiwe la msingi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyopo huko Mazizini, Wilaya ya Mjini, Unguja ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 53 ya Mapinduzi ya matukufu ya Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa udhaifu katika utoaji wa takwimu na taarifa, ni ukiukaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa ummma kwa msingi huo aliagiza kwa kila Wizara ihakikishe inakuwa na mtaalamu wake wa takwimu katika Idara ya Mipango na Sera, ili kuimarisha utoaji wa takwimu.
Dk. Shein alisema kuwa taarifa sahihi haziwezi kupatikana bila ya kuwa na mfumo mzuri wa kitaalamu wa ukusanyaji wa takwimu huku akisisitiza kuwa suala la kuwapa wananchi habari na taarifa sahihi za Serikali ni haki yao ya kikatiba na halina budi kutekelezwa ipasavyo.


“Mimi mwenyewe ni mtumiaji mkubwa wa takwimu, lakini unapohitaji takwimu kutoka Wizarani basi kwa wakati mmoja tarajia kupata takwimu tofauti’,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza kuwa kuna haja ya kuondokana na utaratibu uliopo hivi sasa wa kila mmoja kuwa na mamlaka ya kutoa takwimu za Serikali na kueleza kuwa utoaji wa takwimu muhimu za Serikali una taratibu zake.
Hivyo, alieleza haja kwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoa miongozo kwa Wizara na Serikali juu ya njia bora za kukusanya, kutoa na kutumia takwimu na nani katika ngazi ya Wizara anaweza kutoa takwimu.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja kwa hiyo kuhakikisha kuwa inaandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu takwimu na umhimu wake kwa jamii, kwenye ngazi mbali mbali.


Pia, alitumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuongeza kasi ya kuwasomesha wafanyakazi wanaohusika na takwimu, ili kupatikane wataalamu wa kutosha, watakaoweza kukusanya na kutoa tafsiri mbali mbali za takwimu na uhusiano wake wka maendeleo hapa ya hapa nchini.
Kutokana na umuhimu wa takwimu Dk. Shein alieleza azma ya Serikali kutoa semina maalum kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuelewa suala zima la takwimu na hatimae kusaidia kufanya kazi kwa haraka na ufanisi zaidi.
Sambamba na hayoeleza kuwa katika suala zima la kulitafutia soko zao la karafuu, Zanzibar imekuwa ikishindana na nchi nyingi zinazozalisha zao hilo duniani kwenye bei na ubora sambamba na sifa ya karafuu, hivyo Zanzibar ni lazima ijidhatiti katika kuhimili ushindani.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuiopongeza Ofisi hiyo kwa ujenzi huo kwa mashirikiano ya pamoja na SMZ, SMT na Benki ya Dunia nhuku akisisitiza kuwa takwimu ndizo zinazowezesha kujipima na kujitathmini kwani ndio kiii cha nchi.
Nae Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed alieleza kuwa ujenzi huo ni agizo la Rais Dk. Shein la kutaka kila taasisi ya Serikali iwe na jengo linalokwenda na wakati uliopo huku akieleza azma ya kuzipatia Ofisi za takwimu ofisi Pemba katika majengo mapya ya Ofisi yanayotarajiwa kuejengwa kisiwani humo.
Pamoja na hayo, Dk. Khalid alieleza mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika utekelezaji wa suala zima la takwimu huku akieleza jinsi Wizara ilivyofanikiwa kuzigundua taasisi zinazovujisha mapato ya serikali na kumuahidi Rais kuwa ataziwasilisha kwake mara tu baada ya kumaliza sherehe za Mapinduzi.
Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ashatu Kijaji alitumia fursa hiyo kueleza kuwa ujenzi huo unakwenda sambamba na ujenzi wa jengo jengine kama hilo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania huko Dodoma.
Dk. Kijaji alitumia nafasi hiyo kumuomba Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia kuendelea kuzisaidia taasisi hizo za takwimu ili kwa pamoja ziweze kukamilisha miradi yote miwili na kueleza kuwa takwimu ndio masikio na macho ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 kwa Tanzania Bara na 2020 kwa Zanzibar.
Alitoa pongezi kwa kutekeleza kwa kasi kubwa kauli mbiu ya Serikali ya HAPA KAZI TU!! Na kuishukuru Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza DFID, Canada na Umoja wa Ulaya kwa kuunga mkono tasinia ya takwimu hapa nchini.
Nae Mwakilishi wa Benki ya Dunia Elizabeth Ann Talbert alieleza umuhimu wa takwimu katika maendeleo ya nchi huku akiahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha takwimu.
Mapema Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bi Mayasa Mahfoudh Mwinyi alileza kuwa kiini cha ujenzi wa jengo hilo la takwimu ni kuongezeka kwa mahitaji ya takwimu katika sekta za kiuchumi na kijamii.
Alisema kuwa mahitaji hayo yamepelekea kuongezeka kwa idadi ya wataalamu wa fani ya takwimu sambamba na kuongezeka kwa mahitaji ya vifaa na nafasi za kufanyia kazi ikiwemo mazingira bora ya kazi.
Bi Mayasa alieleza historia ya kuazishwa kwa Ofisi hiyo pamoja na viongozi walioongoza ambapo alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo umeanza rasmi mwezi Oktoba 2015 na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu ambapo ujenzi huo unakadiriwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 7.9 hadi kukamilika kwake.
Ujenzi huo umejengwa na Mkandarasi “Messrs World Class Engineering and Contractors Limited” pamoja na Msimamizi wake Y & P Architects (T) Limited zote ni Kampuni za Kizalendo zilizopo Tanzania ambapo jengo hilo litakuwa na ghorofa nne.
Viongozi mbali mbali walihudhuria hafla hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wengine wa Serikali, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Zanzibar, viongozi wa dini na wananchi mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad