Matukio : Tanzania na Malawi kufanya Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


26 Jan 2017

Matukio : Tanzania na Malawi kufanya Mkutano wa Nne wa Tume ya PamojaMkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tarehe 26 Januari, 2016. Katika kikao hicho Bi. Mindi alizungumza kuhusu tuzo za ubunifu zilizotolewa na Umoja wa Afrika (AU) kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambazo zilikuwa miongoni mwa taasisi zilizoshindanishwa na kuibuka washindi.Pia alitumia fursa hiyo kuwaarifu waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika unaoendelea nchini Ethiopia-Addis Ababa na Mkutano wa Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Februari, 2017.

Kutoka kushoto ni Bw. Felix Tinkasimile Meneja wa Mradi wa Mfumo wa Forodha wa TANCIS, kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA, Bi. Sarah Kibonde kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Bw. David Nghambi kutoka Mamlaka hiyo

Bi. Sarah akizungumza kuhusiana na tuzo iliyotolewa kwa SSRA ambapo alieleza wameshinda Tuzo hiyo katika kipengele cha utunzaji data ambapo wamekuwa wakishirikiana na taasisi za Serikari zinashughulika na umma katika masuala mbalimbali kama Mamlaka ya Vitambulika, Mamlaka ya Mapato na RITA.

Bw. Richard Kayombo akizungumzia tuzo hizo ambapo aliishukuru Wizara ya Mambo ya Nje kwa uratibu na kutambua umuhimu wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato kwa umma katika kuboresha utendaji na kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Bi Mindi akimkabidhi Bi. Sarah kombe la ushindi kwa niaba ya Wizara. Bi. Kibonde aliipokea zawadi hiyo kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Meneja wa Mradi wa Mfumo wa Forodha wa TANCIS kutoka TRA akipokea zawadi ya cheti cha ushindi kutoka kwa Bi. Mindi Kasiga.


Picha ya pamoja ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, TRA na SSRA.Taarifa kuhusu Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi, Tuzo za AU kwa SSRA na TRA na Mkutano wa AU-Addis Ababa


Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi umepangwa kufanyika mjini Lilongwe, Malawi tarehe 03 hadi 05 Febuari 2017. Mkutano huo utawakutanisha viongozi na wataalamu wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania na Malawi.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine P. Mahiga (Mb), anategemewa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo. Aidha, Uongozi wa Mkoa wa Mbeya ambao umekuwa ukishiriki katika vikao vya maandalizi, unategemewa kushiriki katika mkutano huo.


Lengo la mkutano huu ni kujadili na kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Tatu wa JPCC uliofanyika Tanzania, tarehe 24 hadi 30 Juni, 2003.


Miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa kwenye utekelezaji wa makubaliano ya mikutano iliyopita kwa upande wa Tanzania ni pamoja na; Kuanzishwa kwa mradi wa Kituo cha Huduma za Pamoja Mipakani (One Stop Border Post – OSBP) katika mpaka wa Kasumulu/Songwe ambao umefikia katika hatua nzuri; Idara za Uhamiaji, Polisi na Forodha za nchi zetu mbili zinaendelea kushirikiana katika kutoa huduma na kudhibiti abiria na mizigo katika maeneo ya mpakani.


Pia, Mamlaka ya Bandari Tanzania imeruhusu Mamlaka za Malawi kuwa na maeneo yao katika bandari zetu, kwa ajili ya kuhifadhia mizigo na bidhaa nyingine zinazopitia nchini kabla ya kwenda Malawi.


Aidha, mkutano huo utatoa fursa kwa nchi zetu mbili kujadiliana na kukubaliana kuhusu maeneo mapya ya ushirikiano. Miongoni mwa maeneo hayo (kwa upande wa Tanzania) ni pamoja na: Kuanzisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa majini, ambapo mbali na faida za kiuchumi, safari hizo zitaimarisha mwingiliano wa watu na kupunguza tofauti zilizopo. Kwa hivi sasa Serikali inajenga meli tatu, mbili kwa ajili ya kusafirisha mizigo na moja kwa ajili ya abiria.


Maeneo mengine ni kuanzisha Mkataba wa ushirikiano katika Sekta ya Usafiri wa Anga (BASA); Kuanzisha mfumo wa kurahisisha ufanyaji biashara kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo hasa katika maeneo ya mpakani; Kuanzisha ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira na masuala ya afya ikiwemo magonjwa ya mlipuko hususan maeneo ya mipakani; na Kuanzisha ushirikiano katika sekta ya elimu ya vyuo vikuu na vyuo vingine vya amali.


Tangu kuanzishwa kwa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi nchi hizi mbili zimeshafanya vikao vinne vya Tume hiyo. Kikao cha mwisho kilifanyika hapa Dar es Salaam, Tanzania tarehe 24 hadi 30 Juni, 2003 na kuhudhuriwa na viongozi na wataalam wa sekta mbalimbali kutoka nchi zetu mbili.


Wakati huohuo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga kwa niaba ya Wizara amekabidhi tuzo kwa wawakilishi wa taasisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Bi. Sarah Kibonde na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard Kayombo baada ya kuibuka washindi wa Tuzo zilizotolewa na Umoja wa Afrika (AU).


Akipokea kombe baada ya kuibuka mshindi kwenye kipengele B kuhusu “Innovative Partnership in Service Delivery for its National Social Security Collaborative Database Bridging Project" Bi. Kibonde alisema kuwa ushindi huo ni chachu ya taasisi yao kufanya vizuri zaidi katika kutoa huduma bora kwa wananchi wote kwa ujumla.


Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Bw. Kayombo ambaye taasisi yake imefanikiwa kushika nafasi ya pili kipengele C kuhusu "Tanzania customs Integrated System" ameushukuru Umoja wa Afrika kwa kuandaa mashindano hayo ambayo ni muhimu katika kujenga uwazi kwenye eneo la ulipaji kodi.


Pia ameushukuru Ubalozi wa Tanzania kwa kupokea Tuzo hizo kwa niaba yao na kuishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki kwa kukabidhi ushindi huo kwao.


Katika hatua nyingine, Bi. Kasiga alizungumzia juu ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika (AU Summit) unaotarajiwa kufanyika Jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 30 na 31 Januari, 2017. Mkutano huo umetanguliwa na kikao cha Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu na Maafisa Waandamizi kilichofanyika tarehe 22 hadi 24 Januari, 2017 na kufuatiwa na kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoanza tarehe 25 hadi 27 Januari, 2017.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Januari, 2017

Post Top Ad