Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ( PAC) imetoa miezi sita kwa Taasisi na Mashirika yote kulipa madeni ya ankara wanayodaiwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na endapo watashindwa kufanya hivyo watakatiwa huduma hiyo.
Agizo hilo limetolewa mkoani Mbeya na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC , Livingtone Lusinde wakati wa ziara ya Wajumbe wa
Kamati hiyo wakati wa kukagua matumizi halisi ya fedha za Serikali katika kutekeleza Miradi ya Umeme Vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati wa Vijijini( REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme nchini Tanesco.
Lusinde alisema Tanesco imekuwa ikishindwa kutimiza majukumu yake kutokana na kukosa fedha za kutosha kujiendesha na hivyo kuwakosesha wananchi hudumu muhimu ya umeme katika maeneo mbalimbali .
" Tanesco imetapakaa nchi nzima, lakini haiwezi kutoa huduma bora za uhakika kwa wateja wake katika maeneo yote hayo kutokana na miundominu mibovu na kutomfikia mteja kwa wakati kwa vile tu hawana fedha", alisema Lusinde.
Alifafanua kuwa kwa sasa kila Shirika au Taasisi inatakiwa kulipa ankara ya madeni yake moja kwa moja kutoka hazina, hivyo PAC inaimani kuwa kwa kipindi cha miezi sita hawatarajii tena kusikia malalamiko ya madeni ya ankara kutoka tanesco dhidi ya Taasisi na Mashirika.
Aliweka wazi kuwa ili kitimiza azma ya Serikali ya kuviunganisha vijiji vyote nchini na huduma ya umeme, ni vyema Taasisi na mashirika yote yanayodaiwa kulipa madeni yao ili kuipa nguvu Tanesco kutimiza majukumu yake ipasavyo na kwa wakati.
Aidha alionya kuwa kwa kipindi cha miezi sita PAC haitaraji kusikia malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa huduma ya umeme nchini juu ya Tanesco, kwa kuwa itakuwa imelipwa madeni yote na hivyo hutoa huduma bora na za uhakika kwa wateja wake.
Hata hivyo LUSINDE, aliwaagiza Tanesco, REA , Viongozi wa Serikali za Vijiji,Madiwani, Wilaya pamoja na Mikoa, kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya kifaa maalum ,kinachojulikana kama umeme tayari( UMETA) kwa ajili ya kuunganishwa na huduma ya umeme majumbani pasipo kusuka waya ndani ya nyumba yaani Wire Ring kinachopatikana kwa bei nafuu.
Aliweka wazi kuwa kwa mujibu wa Tanesco, kifaa hicho UMETA kinaweza kutumika kwa nyumba za vijijini zenye vyumba kuanzia kimoja hadi vitatu .
Kamati ya PAC imeridhishwa na matumizi ya fedha za Serikali katika kutekeleza Miradi ya Umeme Vijijini na hivyo imewataka wananchi kuwa tayari kwa Mradi wa REA Awamu ya Tatu ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka minne kuanza sasa.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani(kulia), Mwenyeketi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali( PAC) Livingstone Lusinde (katikati) wakisaini vitabu vya wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya umeme vijijni wilayani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa( katikati) akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), pamoja na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, walipomtembelea ofisini kwake, wakati wa ziara ya kukagua matumizi halisi ya fedha za Serikali katika utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini.
No comments:
Post a Comment