Matukio : Makatibu Wakuu Watembelea Mpaka wa Tunduma /Nakombe - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Monday, 30 January 2017

Matukio : Makatibu Wakuu Watembelea Mpaka wa Tunduma /Nakombe

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (kushoto), akiwa pamoja na Mkuu wa wilaya ya Momba mkoani Songwe, Bw. Juma Irando (katikati), na maafisa kadhaa wa Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara naUwekezaji, wakitoka katika Ofisi za Mkurugenzi wa Mji wa Tunduma kuelekea mpakani mwa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma na Nakonde

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (aliyeshika mkoba), Mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Bw. Juma Irando (aliyeshika mikono yake), Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (Aliyesimama nyuma ya Mkuu wa wilaya), wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-Tunduma, Bw. Magori Cosmas (wa pili kulia), kuhusu maandalizi ya kuanzisha rasmi Kituo cha Pamoja cha Mpakani Tunduma/Nakonde katika nchi za Tanzania na Zambia

Afisa Mifumo ya Kompyuta wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Bw. Yasin Kilima (aliyeshika simu katikati), akitoa ufafanuzi wa namna TRA ilivyojiandaa kuweka mifumo itakayo saidia kurahisisha kazi ya utoaji huduma wa pamoja na wenzao wa Zambia, mbele ya Ujumbe ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (wa pili kulia laiyevaa miwani), wakati walipotembelea mpaka wa Tanzania na Zambia kujionea maandalizi ya kuanzishwa rasmi kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani unaotarajiwa kuanza Februari mosi, 2017.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (kushoto), akisisitiza jambo wakati timu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na wizara yake walipotembelea na kukagua miundombinu ya Ofisi ya Uhamiaji Kituo cha Mpakani cha Tunduma.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Bw. Juma Irando, akiongea jambo wakati timu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ilipofanya ziara katika Kituo cha mpakani cha Tunduma/Nakonde kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja na Mpakani baada ya kusainiwa kwa mikataba kati ya Tanzania na Zambia, na kutakiwa kuanza rasmi mwanzoni mwa Februari, 2017

Kaimu Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha mpakani Tunduma/Nakonde, Bw. Tabaran Mzee (kulia), akiueleza ujumbe kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji namna idara yake ilivyojiandaa kuanza kutoa huduma ya pamoja mpakani kati ya maofisa kutoka Zambia na Tanzania ambao watakuwa wakitumia ofisi moja kuwahudumia watu wanaotumia mpaka huo kuvuka kwenda kila upande wa nchi (Tanzania na Zambia)
Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakiwa pamoja na maofisa wa mamlaka ya Mapato kutoka Zambia wakiangalia hali ya biashara na uwekezaji katika Mpaka wa Tunduma na Nakonde ikiwa ni maandalizi ya kuanza rasmi kwa utoaji wa huduma wa pamoja kati ya nchi hizo mbili ili kuboresha mazingira ya biashara baada ya kusainiwa kwa mikataba ya kuanzishwa kwa huduma hiyo katika mpaka huo

Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakiwa pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Mapato kutoka Zambia (ZRA) walipotembelea upande wa pili wa mpaka huo-Nakonde ili kujionea maandalizi ya kuanza rasmi kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani kati ya Tanzania na Zambia baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya kuanzishwa kwa huduma hiyo Februari mosi, 2017

Kituo cha Forodha cha Nakonde Upande wa Zambia

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Zambia-Nakonde, Bw. Nase Lungu, (aliyenyoosha mkono), akitoa maelezo namna ofisi yake ilivyojipanga kuhudumia wateja wao kupitia utaratibu mpya wa kushirikiana kwenye jengo moja kati ya maafisa wa Forodha wa Tanzania na Zambia, wakati Ujumbe kutoka nchi hizo mbili walipotembelea mpaka huo kujionea maandalizi yalipofikia kabla ya kuanza rasmi kwa utaratibu huo Februari Mosi, 2017

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (katikati), akisalimiana na mmoja wa madereva wanaoendesha malori kwenda Zambia, kabla ya kusikiliza kero zao mbalimbali, ambapo malalamiko makubwa yalikuwa ni kutumia muda mrefu mpakani mwa Tunduma/Nakonde kunakowatia hasara na kuchelewesha biashara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (wa pili kulia), akitoa maelekezo namna ambavyo maofisa wa TRA Tanzania na Zambia wanavyopaswa kushughulikia kero za madereva na wananchi wanaotumia mpaka wa Tanzania na Zambia (Tunduma na Nakonde) ili kuboresha biashara mpakani hapo

Ujumbe wa Tanzania na maafisa wa Zambia walipotembelea na kukagua miundombinu ya utoaji huduma pamoja baada ya kutiwa saini kwa mikataba ya kuanza kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani, (Tunduma/Nakonde), huduma inayotarajiwa kuanza rasmi Februari Mosi, 2017

Ujenzi wa Kituo cha Pamoja Mpakani upande wa Tanzania-Tunduma, ukiendelea kwa kasi na una tarajiwa kukamilika baada ya miezi 16 ijayo


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)


………….


Na Benny Mwaipaja, WFM, Songwe


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amewaonya mawakala wa forodha katika mpaka wa Tanzania na Zambia wa Tunduma/Nakonde kuacha Mara moja tabia ya kuwachelewesha madereva wa malori yaendayo masafa marefu kwa makusudi ili wapewe rushwa.


Prof. Mkenda ametoa onyo hilo katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya madereva wa malori waliodai wamekuwa wakicheleweshwa kuvuka mpaka huo kwa zaidi ya siku tatu hadi tano.


Wadereva hao wameeleza kuwa mawakala wa forodha wamekuwa wakiwaambia kuwa nyaraka zao zinazohusika na mizigo wanayosafirisha zimekuwa zilicheleshwa na kituo cha Forodha upande wa Zambia.


Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA), Kituo cha Nakonde, Bw. Nase Lungu, amekana kuhusika na ucheleweshaji huo na baada ya ukaguzi wa moja ya nyaraka hizo ilibainika kuwa upande wa Zambia unatoa nyaraka hizo kwa wakati lakini zimekuwa zikifichwa na Mawakala wa Forodha upande wa Tanzania.


Wakitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, madereva hao wamesema kuwa mawakala wa forodha kwa muda mrefu wamekuwa wakiwaeleza kuwa mtandao wa intaneti wa Upande wa Zambia unaotumika kuchakata nyaraka zao uko chini, hivyo walitakiwa kutoa shilingi 10,000 kwa kila nyaraka ili “kurahisisha” kazi hiyo kwa kuwapa kitu kidogo maafisa wa forodha wa Zambia.


“Mawakala wengine wa forodha wana nyumba zao za kulala wageni hapa Tunduma kumbe wanatulazimisha kukaa hapa ili tulale kwenye nyumba hizo hali inayotutia hasara na wanatumia kutokujua kwetu kutudanganya kwamba mtandao uko chini wakijua hatuna uwezo wa kufuatilia huko Zambia” alieleza kwa masikitiko dereva mmoja


Baada ya kubaini uwepo wa vitendo hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, ameagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA upande wa Tunduma kuandika kibao chenye namba za simu za Mkuu wa TRA mpakani hapo zitakazotumiwa na madereva wanaocheleweshwa kwa makusudi kutoa malalamiko yao.


“Tunataka madereva mtumie siku moja tu kukamilisha nyaraka zenu ili muendelee na safari yenu vinginevyo tutadumaza biashara kati ya Zambia na Tanzania na pia tutaifanya Bandari yetu ya Dar es salaam kushindwa kuleta tija” aliongeza Prof. Mkenda


Alisema kuwa wakala wa forodha atakayebainika kufanya mchezo huo mchafu wa kuwarubuni madereva na kuwachelewesha kupeleka mizigo nchini Zambia, watanyang’anywa leseni zao za biashara.


Meneja Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, mikoa ya Songwe na Mbeya, Bw. Jomimassa Nsindo, amesema kuwa ofisi yake itashirikiana na madereva kukomesha vitendo hivyo ambavyo amesema vinaharibu uchumi na biashara mpakani hapo.


Naye Mkuu wa wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Bw. Juma Irando, alisema kuwa ataitisha kikao cha Madereva, Mawakala wa Forodha na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Mpaka huo wa Tunduma/Nakonde mapema, ili kuweka msimamo wa serikali na kuwaeleza wahusika wanaokiuka taratibu hatua watakazochukuliwa.


Prof. Mkenda na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, walikwenda katika mpaka huo wa Tunduma na Nakonde, kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani kati ya Tanzania na Zambia, unaotarajiwa kuanza Februari mosi, 2017, baada ya kusainiwa kwa mikataba kati ya nchi hizo mbili, juzi.

No comments:

Post a Comment