Elimu : Kamati za Umoja wa Walimu na Wazazi wa Shule za Msingi Zarudisha Nidhamu Shuleni. - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


10 Jan 2017

Elimu : Kamati za Umoja wa Walimu na Wazazi wa Shule za Msingi Zarudisha Nidhamu Shuleni.


 
Lilian Lundo - MAELEZO


Kamati za Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika Shule za Msingi za Serikali nchini zimefanikiwa kudhibiti utoro, nidhamu na kutofanya vizuri kwa baadhi ya Wanafunzi katika shule hizo kwenye mitihani yao ya kumaliza Elimu ya Msingi. Lilian Lundo wa Idara ya Habari (MAELEZO) anaelezea.


Mwaka 2015 Serikali kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (Education Quality Improvement Programme –Tanzania (EQUIP-T), ilianzisha Kamati za Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika shule za msingi nchini kwa lengo la kujenga uhusiano mzuri kati ya Walimu na Wazazi ikiwa ni njia mojawapo ya kuinua ubora wa elimu.


Aidha, Kamati hizo zilipewa jukumu la kufuatilia maendeleo ya Kitaaluma kwa Wanafunzi, kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya shule na kubuni klabu mbalimbali ambazo zitawashirikisha Wananfuzi katika kujadili masuala ya kijamii na hivyo kuwavutia Wanafunzi kupenda masomo.


Mpango huo ambao awamu ya kwanza ulianza katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Lindi, Mara, Simiyu, Shinyanga na Tabora, umeleta mafanikio makubwa kimaendeleo ya kitaaluma darasani, kuongezeka kwa nidhamu na kudhibiti utoro jambo ambalo pia limeongeza ufaulu katika mitihani yao ya Elimu ya Msingi.


Kwa mujibu wa wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Uhelela iliyoko Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Bw. Dankan Kamwela, mpango huo umepata mafanikio makubwa katika shule yake ambapo imefanikiwa kupunguza utoro kutoka Wanafunzi 127 sawa na asilimia 30 kwa siku mwaka 2015 hadi Wanafunzi 12 sawa na silimia 8 kwa siku mwaka 2016.


Ameelezea kwamba, kwa kuitumia Kamati ya Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) wamekuwa wakifanya vikao mara kwa mara kwa kuwashirikisha Wazazi na Wanafunzi kujadili maendeleo ya Shule ikiwa ni pamoja na wajibu wa Walimu, Wazazi, na Wanafunzi kwa ujumla.


Amesema, kufuatia vikao hivyo ilibainika kuwa iko haja ya kuweka mikakati itakayosaidia kurekebisha kasoro zote zilizoonekana kuchangia kushuka kwa maendeleo ya kitaaluma, utoro na nidhamu ambavyo kwa pamoja vinasabisha kutofanya vizuri kwa Wananfunzi katika mitihani yao kwenye shule zilizo katika Kata hiyo.


Kwa upande wake, Afisa Elimu Mkoa wa Mara Bw. Hamis Lissu amesema ufaulu wa darasa la saba mkoani humo umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2014. Ameeleza kuwa mwaka huo mkoa wa Mara ulikuwa katika nafasi ya 25 kati ya mikoa 25. Mwaka 2015 mkoa wa Mara ulishika nafasi ya 17 kati ya 25 na mwaka 2016 umeshika nafasi ya 13 kati ya mikoa 26.


Mratibu Elimu Kata wa Chamwino, Chitema Simango amesema kuwa Kamati hiyo imewezesha kwa kiasi kubwa ushiriki wa Wazazi katika maendeleo ya shule ambapo kabla ya kuanzishwa Umoja huo Walimu walikuwa wakiachiwa ufuatiliaji wa maendeleo ya Wanafunzi pamoja na shule lakini kwa sasa Wazazi na Walimu wanashirikiana kwa katika kufuatilia maendeleo ya Wanafunzi na shule kwa ujumla.


Vile vile amesema kuwa UWW umeleta uwazi katika mapato na matumizi ya Shule ambayo yanabandikwa katika mbao za matangazo za shule husika na Wazazi wanapewa nafasi ya kuhoji juu ya mapato na matumizi hayo.


Aidha ametoa ushauri kwa Maafisa Elimu, Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu katika mikoa ambayo bado haijaanzisha Kamati za UWW kuanzisha Kamati hizo katika shule zao ili kuleta mabadiliko ya uendeshaji wa shule za msingi za Serikali kwa kuishirikisha jamii. Kwani kupitia UWW Walimu na Wazazi wanajadiliana kwa pamoja na kukubaliana namna ya kuboresha taaluma ya Wanafunzi katika shule husika na hata katika kusimamia miradi ya shule.


Pia amesema kuwa Wazazi wanaposhirikiana na walimu inapelekea Wanafunzi kuwa na nidhamu ya hali ya juu kutokana na mwanafunzi asiye na nidhamu au mtoro anakosa pakukimbilia kwani mwalimu na mzazi wamekuwa kitu kimoja.


Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (Education Quality Improvement Programme -Tanzania) EQUIP-T ni mpango unaosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudhaminiwa na Serikali ya Uingereza. Mpango huu ni wa miaka minne ambao ulianza mwaka 2014 katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Kigoma, Mara na Lindi.


Mpango huo umejikita katika kuinu ubora wa Elimu Shule za Msingi katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wa madarasa ya awali mpaka la tatu katika kuwajengea uwezo katika ufundishaji, utoaji wa vifaa vya kufundishia, uanzishwaji wa kamati za walimu na wazazi pamoja na mafunzo ya uongozi kwa walimu wakuu, kamati za shule pamoja na umoja wa walimu na wazazi.

Post Top Ad