Matukio : Tume ya Mipango yafanya ziara mradi wa ufugaji Ng'ombe na Uzalishaji Maziwa - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


17 Dec 2016

Matukio : Tume ya Mipango yafanya ziara mradi wa ufugaji Ng'ombe na Uzalishaji MaziwaKaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri anayeongoza timu ya ukaguzi wa miradi kutoka Tume ya Mipango akielekea kukagua mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa katika eneo la Narunyu wilayani Lindi. Kulia ni Bi, Yasinta Mrose (Mtawa) ambaye anasimamia upande wa mifugo.

Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akitoa ushauri kwa uongozi wa mradi ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa (ambao ni watawa) katika moja ya mabanda ya ng’ombe wa maziwa. Wengine ni maofisa wa Serikali walioambatana na Kaimu Katibu Mtendaji huyo.

Baadhi ya ng’ombe wa maziwa wa mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wakiwa katika banda.

Bi Yasinta Mrose (Mtawa) akimwonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri hatua za awali za kutengeneza gesi kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe.

Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Florence Mwanri akiwa ndani ya chumba ambapo gesi inazalishwa (gesi ipo ndani ya turubai lililojaa ndani ya chumba hicho linaloonekana chini).

Mwonekano wa Kiwanda cha kuzalisha nishati inayotokana na kinyesi cha ng’ombe.

Ndama wanaofugwa katika mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wakiwa katika banda.
 

PICHA ZOTE NA ADILI MHINA, TUME YA MIPANGO
Na Adili Mhina, Lindi
Tume ya Mipango imefanya ziara katika mradi wa ufugaji ngo’ombe na uzalishaji wa maziwa unaoendeshwa na watawa eneo la Narunyu wilayani Lindi na kushauri uongozi wa mradi huo kutumia fursa za mikopo ya kilimo ili kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ya mifugo pamoja na kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia kinyesi cha wanyama.


Mradi huo umekuwa ukizalisha maziwa na nyama kwa ajili ya biashara huku nishati ya umeme kwa ajili kuendesha shughuli za kiwanda hicho ikiwa inazalishwa kutokana na kinyesi cha wanayama hao.


Kwa sasa uzalishaji umepungua baada ya kiwanda kushindwa kuzalisha nishati ya umeme ya kutosha na kuanza kutegemea umeme wa tanesco ambao kwa mujibu wa mmoja wa wasimamizi wa mradi huo, Bi Yasinta Mrose umesababisha gharama za uzalishaji kuongezeka.


Changamoto nyingine ni kuharibika kwa baadhi mashine zinazotumika kuandaa malisho ya ngo’ombe, ukosefu wa soko la karibu kwa mazao ya nyama na maziwa, pamoja na uhaba wa maeneo kwa ajili ya malisho ambapo kwa sasa mradi una zaidi ya ng’ombe 400.


Kutokana na changamoto hizo, Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri aliueleza uongozi huo kuwa ni vyema wafanye taratibu za kuomba mkopo hususani katika benki ya kilimo ili waweze kuongeza mtaji, uzalishaji na kupanua soko.


“Huu ni mradi mzuri na msirudi nyuma katika uzalishaji wenu, nawashauri mkae mjadiliane muone namna ya kupata mkopo ili muweze kununua mashine za kisasa na muongeze uzalishaji. Bila kuchukua hatua hizo mnaweza mkashangaa mradi unakufa wakati unafaida kwenu na hata kwa wananchi wanaowazunguka,” alieleza.


Kuhusu changamoto ya soko la karibu, Mwanri alieleza kuwa uongozi unapaswa kufikiria kuzalisha maziwa na kutengeneza bidhaa zinazotokana na maziwa na kusafirisha nje ya wilaya ya Lindi kwani soko bado ni kubwa.


Aliongeza kuwa hatua iliyofikiwa ya kuzalisha umeme wa kutosha kuhudumia shughuli zote za uzalishaji kiwandani hapo ni nzuri na Serikali inaiunga mkono jitihada za sekta binafsi katika kukuza maendeleo ya uchumi ikiwa ni njia ya kutekeleza malengo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21).


“Nimefarijika sana kusikia mlikuwa mnazalisha umeme wa kuwatosheleza, mmejitahidi kutekeleza mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa vitendo. Tume ya Mipango inatambua na kuunga mkono jitihada zenu hivyo nawasihi shirikianeni na Halmashauri kufanya kila linalowezekana ili shughuli zenu ziendelee zaidi ya mlivyokuwa mnazalisha huko nyuma,” aliongeza.

Post Top Ad