Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein amewataka Waumini
wa Madhehebu ya Kikristo wasichoke kuiombea nchi amani kwani bila ya amani
hakuna maendeleo.
Mama Mwanamwema Shein aliyasema hayo leo
huko katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali Vitongoji, Chake Chake Pemba
katika mkutano maalum kati yake na Waumini wa Madhehebu ya dini ya Kikristo.
Katika maelezo yake Mama Shein, alisema
kuwa bila ya amani hakuna mafanikio na wala mwanaadamu hawezi hata kupata muda
wa kumuwabudu Muumba wake, hivyo suala la amani halina mbadala.
Alisema kuwa ni ukweli uliowazi kwamba
amani inapotoweka, waathirika wakubwa kwa bahati mbaya ni akina mama na watoto
hivyo aliwataka wananchi kutolipa nafasi jambo hilo kutokea kwani athari zake
ni kubwa.
Mama Shein alitumia fursa hiyo
kuwapongeza waumini hao kwa kuwa wapenda amani na usalama wa nchi yao kwa
kuiombea amani kabla ya uchaguzi na hadi sasa baada ya uchaguzi, bila ya
kuchoka kama wanavyofanya waumini na wananchi wa dini nyengine ambao wanaitakia
mema nchi hii.
“Kwa mapenzi makubwa ya Mwenyezi Mungu
amezisikia sala na dua tunazoziomba na anaendelea kutupa neema hii, ambayo
katika sehemu nyengine duniani wanaitamani lakini wanaikosa”,alisema Mama
Shein.
Aidha, Mama Shein alitoa wito kwa waumini
hao kutochoka kuiombea nchi amani na kuijenga kwa nguvu zao zote.
Mama Shein alitoa nasaha zake kwa akina
mama wenzake na kuwataka kuepuka kushiriki kwenye jambo lolote linaloweza
kuondoa amani na kutoa wito kwa jamii kuendelea kutekeleza wajibu wao wa
kuzungumza na watoto wao ili waepuke kutumika kwa malengo mabaya yanayoweza
kuwaharibia maisha yao.
“Vitabu vya dini vimetueleza juu ya
kuwapenda, kuwaenzi na kuwatunza watoto wetu kwani watoto ni neema ambayo
Mwenyezi Mungu ametujaalia, na hatuna budi kuonesha shukurani zetu kwake kwa
kuwalea vyema ili waje watufae katika siku zijazo”,alisema Mama Shein.
Aidha, Mama Shein aliwataka wazazi
wenzake kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa kutoa ripoti katika vyombo
vya sheria na taasisi zinazohusika pale inapobainika matukio ya udhalilishaji.
Mama Shein aliwahakikishia wananchi kuwa
Serikali yao iko imara na inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti
vitendo vya udhalilishaji kupitia Taasisi, Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee,
Vijana, Wanawake na Watoto pamoja na vyombo mbali mbali vya sheria.
Sambamba na hayo, Mama Shein aliwataka
wananchi kuendelea kushirikiana bila ya kubaguana kwa kuzingatia mila, silka na
utamaduni wa tangu enzi wa kuvumiliana na kuheshimiana kwani hiyo ni nguzo muhimu ya kuendeleza amani na utulivu uliopo
hapa nchini.
Wakati wa mchakato wa Kampeni za Uchaguzi
uliopita Mama Shein alikutana na Waumini hao ambapo aliwanasihi kuliombea taifa
ili lizidi kuwa na amani na kuingia katika mchakato huo kwa salama na hatimae
ndicho kilichotokea ambapo Mwenyezi Mungu ameivusha nchi salama na viongozi
waliochaguliwa na wananchi wanaendelea kuyatekeleza majukumu yao kwa mafanikio
makubwa.
Nae Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Mama Asha Balozi aliwaeleza waumini hao kuwa mkutano huo una lengo la
kuwashukuru na kuwasalimia waumini hao kutokana ushiriki wao uliopelekea
kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwa salama na amani na hatimae Chama Cha Mapinduzi
na viongozi wake kupata ushindi.
Alisema kuwa mshikamano uliopo ndio
uliowafikisha hapo huku akiwapa pole kwa changamoto mbali mbali walizopambana
nazo katika kipindi cha uchaguzi na kuwapongeza kwa mshikamano wao huku
akieleza kuwa dini zote zinahubiri amani na utulivu wala hakuna dini
inayohubiri ugomvi na fujo.
Mapema Mama Fatma Karume nae alitumia
fursa hiyo kueleza uhusiano wa kihistoria uliokuwepo kati ya waumini wa dini ya
kikristo na dini nyengine hapa nchini kwani waumini wote ni ndugu na walikuwa
kitu kimoja katika kugombania uhuru wa Zanzibar na hatimae kufanyika Mapinduzi matukufu
ya Januari 12, 1964 yaliyowaweka huru wanyonge wa nchi hii.
Katika hafla hiyo, Mama Shein alizindua Albamu ya Kwaya yenye jina la
‘Mungu Baba’ ambayo ina nyimbo 11 zikiwa katika mfumo wa sauti kutoka Kanisa la
Redeemed Gospel lililopo Chake Chake Pemba, ambapo wanakwaya hao nao walipata fursa
ya kutumbuiza baadhi ya nyimbo zao hizo.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Wachungaji Pemba, kutoka Kanisa la
Anglican Wete, Mchungaji Emanuel John Masoud alieleza kuwa mchakato wote wa
uchaguzi umeenda salama na kila aliekuwa na haki ya kupiga kura alipata nafasi
nzuri ya kupiga kura.
Pia, Mchungaji Masoud alivipongeza vikosi
vyote vya Ulinzi na Usalama kwa kufanya kazi yao vizuri, iliyosaidia kuondoa
hofu kwa wapenda amani wote na kuweka mashaka na woga kwa wale waliokusudia
kuchafua amani ya nchi.
Wachungaji hao walieleza kuwa dua, sala
na maombezi ya kuiombea nchi, wananchi pamoja na viongozi wote hapa nchini kwao
ni kitu kilichopewa kipaumbele katika ibada zao zote wanazofanya kila siku.
Viongozi mbali mbali wa madhehebu ya dini ya kikristo walihudhuria katika hafla hiyo wakiwemo Wachungaji wa Makanisa yote ya Pemba na kutoa shukurani zao kwa Mama Shein kwa kwenda kuwashukuru kwa kushiriki uchaguzi uliokwenda kwa amani na utulivu na kuahidi kuendelea kuhubiri utii wa sheria bila shuruti sambamba na amani na utulivu kwani ni agizo la Mungu.
No comments:
Post a Comment