Shule ya St Mary iliyopo Tengeru mkoani Arusha imefanikiwa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi zaidi ya 200 ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa vijana kujitegemea kiuchumi na kutumia fursa walizonazo kujenga maisha yao.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi huo, Mkuu wa Shule hiyo, Br. Protas Mangu, alisema elimu hiyo imelenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kubuni na kutengeneza bidhaa mbalimbali, ikiwemo sabuni, ili waweze kutumia ujuzi huo kujipatia kipato.
Alisema sababu kubwa ya kuwapatia wanafunzi elimu hiyo ni kuwawezesha kuanza kujijenga kiuchumi kuanzia ngazi ya familia, badala ya kutegemea ajira pekee baada ya kumaliza masomo yao.
Br. Mangu alisema wanafunzi hao wamekuwa wakipata elimu hiyo ya ujasiriamali wakiwa katika mazingira ya shule, huku wakipewa fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazowasaidia kujifunza namna ya kuanzisha na kuendesha miradi midogo ya kiuchumi.
Alisema pamoja na mafunzo hayo, wanafunzi wameanzisha mfuko wao ambao unawasaidia kupata fedha kwa ajili ya mahitaji madogo madogo yanayohusiana na kukuza na kuendeleza mradi huo.
Kwa upande wao, wanafunzi ambao ni wanufaika wa mradi huo walisema elimu hiyo imeanza kuleta mabadiliko katika maisha yao, ikiwemo kuwasaidia kujenga msingi wa kujitegemea kiuchumi kuanzia ngazi ya familia.
Walisema wakati wa likizo hutumia ujuzi walioupata shuleni kutengeneza bidhaa mbalimbali za usafi katika maeneo yao ya nyumbani, hatua ambayo imewapa fursa ya kuendelea kujifunza na kutumia ujuzi huo katika mazingira halisi.
Wanafunzi hao pia walisema mradi huo umewasaidia kutambua kuwa ujasiriamali unaweza kuwa njia muhimu ya kujenga maisha yao ya baadaye, huku wakiwataka wazazi kuendelea kuwaunga mkono katika juhudi hizo.
Aidha, waliomba wazazi na wadau wengine kuendelea kuutunza na kuuendeleza mfuko wa mradi huo ili uweze kukua zaidi na kuwawezesha wanafunzi kupata mitaji ya kuanzisha biashara zao baada ya kumaliza masomo.
Walisema kuwa kupitia elimu hiyo, wanaamini wanaweza kujiajiri na kujenga uchumi wao badala ya kuwa na mtazamo wa kusubiri ajira pekee baada ya kumaliza masomo.


No comments:
Post a Comment