Ujumbe
wa wataalamu wa Fedha, Sera na Uchumi kutoka Tanzania wakifuatilia kwa
makini Mazungumzo ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika,
Louis Rene Peter Larose (hawapo Pichani), Makao Makuu ya Benki hiyo
Jijini Washington DC, Marekani, ambapo unafanyika Mkutano wa Mwaka wa
Benki hiyo ambayo Tanzania ni Mwanachama, wa kwanza kushoto ni Kamishna
wa Sera Augustine Ollal, Kamishna wa Bajeti John Cheyo na Kaimu Kamishna
wa Fedha za Nje Mamelta Mutagwaba.
Ujumbe
wa wataalamu wa Fedha, Sera na Uchumi kutoka Tanzania wakifuatilia kwa
makini Mazungumzo ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika,
Louis Rene Peter Larose (hawapo Pichani)
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kulia) akisalimiana na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika,
Louis Rene Peter Larose walipokutana ofisini kwake Jijini Washington DC,
Marekani, ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo
ya Tanzania na namna Benki hiyo ilivyojipanga kuhakikisha kuwa
inaiwezesha Tanzania kufikia ndoto yake ya kuwa nchi yenye uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025
Ujumbe
wa Tanzania ukiongozwa na waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango, wakishikana mikono kuonesha umoja na mshikamano mara baada ya
kumalizika kwa mazungumzo kati ya ujumbe huo na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter
Larose, Jijini Washington DC nchini Marekani, ambako ujumbe huo
unahudhuria Mkutano wa Mwaka wa Benki hiyo.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Katikati, Akiagana na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika
mara baada ya viongozi hao kumaliza mazungumzo yaliyogusia Nyanja
mbalimbali za kijamii na kiuchumi, Jijini Washington DC, nchini
Marekani, ambapo Tanzania inashiriki Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia
na Shirika la Fedha Duniani-IMF.
Baadhi
ya wajumbe wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia
na Shirika la Fedha Duniani-IMF, baada ya kumalizika kwa kikao kati ya
ujumbe huo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia
Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, wakiwa nje ya Majengo ya Benki
hiyo Jijini Washington DC nchini Marekani. Wa kwanza kushoto ni Kaimu
Kamishna wa Fedha za nje, Wizara ya Fedha na Mipango, Mamelta Mutagwaba,
Kamishna wa Bajeti, John Cheyo, Kamisha wa Madini James Andilile na
Kamishna wa Sera Augustine Ollal.
Wajumbe
kutoka takribani nchi 180 duniani kote, wanachama wa Benki ya Dunia na
Shirika la Fedha Duniani-IMF, wakiwa katika Siku ya kwanza ya Mkutano wa
Mwaka wa Taasisi hizo Jijini Washington DC nchini Marekani, Tanzania
inawakilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt, Philip Mpango ambaye
ameongoza ujumbe wa wataalamu wa Fedha na Uchumi katika mkutano huo.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (wa kwanza kushoto),
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (wa pili), Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania BOT, Prof Benno Ndulu (wa tatu kutoka Kushoto),
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BoT Dkt. Dkt. Natu El-Maamry
Mwamba, Kamisha Msaidizi wa Nishati, Wizara ya Nishati na Madini, James
Andilile, wakiangalia ripoti iliyotolewa na timu ya wataalamu wa Benki
ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF, kuhusu miradi mbalimbali
inayotekelezwa nchini Tanzania kwa ufadhili na mkopo kutoka Taasisi
hizo.
Ujumbe wa Tanzania na badhi ya viongozi
wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani-IMF wakikatisha Mitaa ya
Jiji la Washington DC nchini Marekani kwa miguu kuwahi vikao mbalimbali
vinavyoendeshwa na Taasisi hizo kabla ya kufikiwa kwa kilele cha
Mkutano wa Mwaka wa Taasisi hizo Oktoba 9 mwaka huu. Picha zote na Wizara ya Fedha na Mipango.
Na Benny Mwaipaja,
MoFP
Washington DC,
Marekani
8.10.2016
WAZIRI wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha sekta
ya kilimo na Utalii ili ziweze kutoa mchango mkubwa kuinua uchumi wa Taifa
pamoja na kuwaondoa wananchi wake kutoka katika lindi la umasikini
Waziri Mpango
ameyasema hayo Jijini Washington DC, nchini Marekani, wakati akizungumza na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis
Rene Peter Larose, ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yanayohusu
utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taasisi hiyo.
Amesema kuwa
kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya watanzania hivyo mapinduzi yanayokusudiwa
katika sekta hiyo ni kuendesha kilimo biashara kwa kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya wakulima.
Kuhusu sekta ya
Utalii, Dkt. Philip Mpango anayeongoza ujumbe wa wataalamu wa Uchumi na Fedha
katika Mkutano wa Mwaka ulioandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha
Duniani, IMF, amesema kuwa serikali inakusudia kupitia upya kodi zinazoleta
kero mbalimbali katika sekta hiyo pamoja kilimo.
Eneo jingine
alilotaka Benki ya Dunia kuingilia kati, ni kuipatia Tanzania Mkopo na ruzuku
utakaosaidia kukabiliana na madeni yake makubwa inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii pamoja madeni ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, ili
shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida na kuchangia ukuaji wa uchumi wa
Taifa kwa haraka.
Kwa Upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis
Rene Peter Larose, ameihakikishia Tanzania kuwa pamoja na miradi mingine,
itafadhili mradi mkubwa wa kilimo wa ukanda wa kusini “Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT)” ili kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wananchi na
taifa kwa ujumla.
“Mimi
nimefika Tanzania na ninaifananisha nchi hiyo kuwa itafikia ama kuzidi hadhi ya
Dubai kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo ambazo zikisimamiwa vizuri
zitaibadili kabisa nchi hiyo kimaendeleo” alisema Larose.
Ameitaka
Tanzania kutosita kuitumia ipasavyo benki hiyo kufanikisha malengo yake ya
maendeleo na kwamba yeye mwenyewe binafsi pamoja na kwamba anaongoza kundi la
nchi 22 za kiafrika katika Benki hiyo, atahakikisha Tanzania kama zilivyo nchi
nyingine, inanufaika na uwepo wa Taasisi hiyo.
Mkurugenzi
huyo Mtendaji amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, namna anavyosimamia mambo kwa nguvu zake zote na ametoa pole kwa nchi
hiyo kutokana na madhara iliyoyapata kufuatia tetemeko kubwa la ardhi
lililoukumba mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani.
Ameahidi kuwa Benki hiyo itatuma wataalamu watakaosaidia kufanya utafiti na kuishauri nchi kitaalamu na kimiundombinu namna ya kukabiliana na majanga ya matetemeko pamoja na vifaa vitakavyosaidia kutoa tahadhari kabla ya kutokea kwa majanga kama hayo.
No comments:
Post a Comment