Uchumi : Pato la Taifa limekua kwa thamani ya Shilingi Trilioni 11.7 - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


30 Sept 2016

Uchumi : Pato la Taifa limekua kwa thamani ya Shilingi Trilioni 11.7

Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu hali ya pato la Taifa kwa robo ya pili  kuanzia Aprili hadi Juni 2016 jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa, Daniel Masolwa na kulia ni Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Joyce Sawe.
Baadhi ya Viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Picha na Avila Kakingo, Globu ya Jamii. 
PATO LA TAIFA LIMEKUA KWA THAMANI YA SHILINGI TRILIONI 11.7

Na Veronica Kazimoto. Pato la Taifa limekua kwa jumla ya thamani ya Shilingi trilioni 11.7 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 10.9 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema ukuaji wa pato la Taifa umetokana na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ambapo shughuli  hizo zimekuwa  kwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Kwa upande wa shughuli za uchumi za viwanda na ujenzi, Dkt. Chuwa alisema kumekua  na ongezeko la asilimia 20.5 katika kipindi hicho ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 11.2 mwaka 2015 katika shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto.
Aidha shughuli za uzalishaji bidhaa na viwanda zimeongeza kwa asilimia 9.1 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ukilinganisha na kasi ya asilimia 5.2 ya mwaka 2015.
Shughuli za uchukuzi na uhifadhi, Dkt. Chuwa amesema kuwa shughuli hizo zimekua kwa kiwango cha asilimia 30.6 zikisababishwa  na usafirishaji wa abiria kwa njia ya reli na barabara ikiwa ni pamoja na usafiri wa UDART.
Vilevile, shughuli za fedha na bima zimeongezeka kwa kasi ya asilimia 12.5 ikilinganishwa na asilimia 10.0 iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Dkt. Chuwa amefafanua kuwa  huduma za elimu zimekua kwa kasi ya asilimia 8.0 katika robo hiyo ya mwaka ikilinganishwa na aslimia 7.4 ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 ambapo ukuaji wa shughuli hii imetokana na ongezeko la wanafunzi waliodahiliwa mwaka 2016.
Kwa upande wa Nchi za Afrika Mashariki ambazo zimeshachambua na kutoa Pato la Taifa katika kipindi kinachoishia Juni 2016 ni Rwanda ambapo Pato halisi la Nchi ya Rwanda katika kipindi cha Aprili – Juni 2016 limeendelea kukua kwa asilimia 5.4 ikilinganisha na asilimia 7.2 ya miezi kama hiyo mwaka 2015.
Takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka hupimwa kwa kutumia thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini katika vipindi vya miezi mitatu mitatu ambavyo ni Januari – Machi, Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba – Desemba ambapo hujumuisha shughuli zote za kiuchumi, na hutumika katika kutathmini, kupanga mipango na kutayarisha sera za kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad