Kaimu
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dk. Emmanuel Munishi (kulia) akimkabidhi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kushoto) Mfano wa hundi ya shilingi
milioni 8,000,000/= zilizotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kama
mchango wa chuo hicho kwa jamii kwa ajili ya kununulia madawati yatakayotumiwa
na wanafunzi wa shule za msingi katika mkoa huo.Katikati ni Afisa Uhusiano wa
Jamii wa Chuo hicho Leonidas Tibanga.
Kaimu
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dk. Emmanuel Munishi (katikati) akizungumza
na vyombo vya habari mara baada ya kukabidhi mchango wa wa madawati wa shilingi
milioni 8 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kulia) leo jijini
Dar es salaam. Mchango huo umetolewa na chuo hicho kununulia madawati yatakayotumiwa
na wanafunzi wa shule za msingi za mkoa huo, Kushoto ni Afisa Uhusiano wa Jamii
wa Chuo hicho Leonidas Tibanga.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo (kulia)
akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 17,700,000/= Mkuu wa Mkoa wa Dar
es salaam, Paul Makonda (kushoto) kama mchango wa madawati kwa wanafunzi wa
shule za Msingi jijini Dar es salaam leo.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kushoto) akiangalia mfano wa
hundi ya shilingi milioni 6 zilizotolewa na Taasisi ya Kijamii
inayojihusisha na masuala ya Kijamii ya African Relief Organisation ya
jijini Dar es salaam kwa ajili ya kununulia madawati. Kulia ni
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Shekh Abdallah Ndauga na Mratibu wa Miradi wa
Taasisi hiyo Moadh Shannawi.
Mkuu wa
Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akizungumza na waandishi wa Habari mara
baada ya kupokea msaada wa Fedha kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Taasisi ya Kidini ya Masuala ya Kijamii ya
African Relief Organisation kwa ajili ya kununulia madawati kwa shule za Msingi
za Dar es salaam. Picha/Aron
Na. Aron Msigwa – Dar es
salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar
es salaam, Paul Makonda ametoa wito kwa Taasisi na Mashirika mbalimbali jijini
Dar es salaam kujitokeza kwa wingi kuunga mkono zoezi la uchangiaji wa hiari wa
madawati kwa shule za msingi linaoendelea jijini humo ili kuweka mazingira mazuri
ya kujifunzia yatakayozalisha wanafunzi bora
wa shule za msingi.
Akizungumza mara
baada ya kupokea mchango wa fedha za kununulia madawati kiasi cha shilingi
milioni 31.7 kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) na Taasisi ya kidini ya masuala ya jaamii ya African Relief Organisation
leo jijini Dar es salaam Mhe. Makonda amesema kuwa bado jamii inao wajibu na jukumu la kuhakikisha kuwa mazingira ya
kusomea ya wanafunzi wa shule za msingi yanakuwa bora ili kuzalisha wahitimu
walio na msingi imara.
“Napenda kutumia
fursa hii kuzishukuru taasisi hizi ambazo zimeitikia wito wa kutoa michango yao
ili kuwezesha upatikananji wa madawati, nawashukuru sana viongozi wa taasisi
hizi kwa kuitikia wito wa mkoa wetu na kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. John
Pombe Magufuli za kuhakikisha shule zetu zina madawati na hakuna mwanafunzi
anayekaa chini” Amesisitiza Makonda.
Ametoa wito kwa wananchi
ambao wanaguswa kwa namna moja au nyingine kuendelea kutoa michango yao ili kuwasaidia
wanafunzi wa shule za Msingi katika jiji la Dar es salaam ambao walikuwa
wanapata shida ya kusomea katika mazingira magumu.
Ameongeza kuwa ili
taifa liweze kuwa na wataalam wazuri katika Nyanja zote lazima msingi wa elimu
katika shule za msingi uwe mzuri na kufafanua kuwa ndoto ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na mkoa wa Dar es salaam ni
kukamilisha upatikanaji wa madawati na majengo ya madarasa.
Kwa upande wake Kaimu
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dkt. Emmanuel Munishi akizungumza mara
baada ya kukabidhi mfsno wa hundi ya shilingi milioni 8 kama mchano wa chuo hicho
kwa jamii amesema kuwa wao kama Chuo cha Elimu ya Biashara chenye kampasi mikoa
minne ya Tanzania ukiwemo Mwanza, Dar es salaam, Dodoma na Mbeya kimeguswa
kuchangia kiasi hicho cha fedha kwa kuwa kinawategemea wanafunzi waliofundishwa
vizuri kutoka shule za Msingi.
Amesema wameamua
kuunga mkono Juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ili kuhakikisha kuwa shule Zote za
Dar es salaam zinaondokana na shida ya madawati.
“Sisi tumeguswa na
uchangiaji wa madawati kwa kuwa ni taasisi ya ya elimu ya juu, kama taasisi ya
elimu ya juu hatuwezi kupata wanafunzi wetu kama hakuna shule za msingi,
tumeamua tusiwe watu wa kuvuna tu tukaamua kwenda moja kwa moja kwenye msingi
ili kujenga msingi imara wa shule zetu” Amesisitiza.
Ameziomba taasisi
zote za Elimu ya juu nchini kuiga mfano wa CBE katika kuchangia sekta ya elimu
hapa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi
ya Kidini ya Masuala ya Kijamii ya African Relief Organization ya jijini Dar es
salaam Shekh Abdallah Ndauga iliyochangia shilingi milioni 6 amemshukuru Mkuu
wa Mkoa huo kwa moyo wake wa kuendelea kuwahamasisha wananchi ambao wamekuwa
wakijitokeza kwa wingi kuchangia madawati.
Amsesema Taasisi ya
African Relief Organisation itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na mkoa
wa Dar es salaam katika kuleta maendeleo ya wananchi wake kupitia miradi
mbalimbali wanayotekeleza ikiwemo uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali
nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) Hiiti Sillo akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada uliotolewa na
Mamlaka hiyo wa shilingi milioni 17.7 amesema TFDA inaunga mkono jitihada za
Rais, Dkt. John Pombe Magufuli za kuhakikisha kuwa kila mtoto anakaa katika
dawati ambapo katika bajeti yake ya mwaka 2015/16 inatoa mchango wa madawati
236.
Sillo ameongeza kuwa
TFDA pamoja na majukumu iliyonayo inatambua kuwa elimu ndiyo nguzo muhimu
katika kupambana na maadui wakubwa wa maendeleo, hivyo itaendelea kutoa mchango
wake katika kusaidia sekta ya elimu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment