Sehemu ya kituo cha kupoza umeme cha KIA 132/33kV kilichopo mkoani Kilimanjaro kama kinavyoonekana pichani.
Meneja
Miradi ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO), Mhandisi Emmanuel Manirabona (wa pili kutoka kulia)
akielezea mafanikio ya kituo cha kupoza umeme cha KIA 132/33kV
kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Meneja
wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mkoa wa Arusha Mhandisi Gaspa
Msigwa ( wa pili kutoka kulia) akielezea hali ya upatikanaji wa umeme
mkoani Arusha kutokana na kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA
132/33kV kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Meneja
Miradi ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO), Mhandisi Emmanuel Manirabona ( katikati) akielezea
namna ya uwekaji wa nyaya za umeme chini ya sakafu kwa lengo la
kuimarisha usalama katika kituo cha KIA 132/33kV kilichopo mkoani
Kilimanjaro.
Meneja
Miradi ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO), Mhandisi Emmanuel Manirabona akielezea jinsi kifaa cha
kuongozea mitambo ya umeme kinavyofanya kazi mbele ya waandishi wa
habari (hawapo pichani).
Sehemu
ya mitambo ya kampuni inayojishughulisha na uzalishaji wa kokoto ya
Ravji Aggregate Limited iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha ambayo
ni moja ya wanufaika wa umeme kutoka katika kituo cha KIA 132/33kV.
John
Augustino mkazi wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha akielezea mchango
wa kituo cha KIA 132/33kV katika ukuaji wa uchumi wa wakazi wa mkoa
huo.
Mwarobaini wa kukatika kwa umeme Arusha wapatikana.
Ni baada ya kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA
Wateja zaidi ya 89,000 waunganishwa; TANESCO kukusanya bilioni 9 kwa mwezi
Juni 06, 2016.
Na Greyson Mwase, Arusha
Imeelezwa
kuwa kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA kilichopo karibu
na Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kilimanjaro International
Airport) kumepelekea tatizo la kukatika kwa umeme kuisha katika mkoa wa
Arusha na baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro na
kuongeza kipato kwa wakazi wa mkoa huo.
Kauli
hiyo ilitolewa na Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mkoa wa
Arusha Mhandisi Gaspa Msigwa, kwenye ziara ya waandishi wa habari
kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini katika miradi ya TEDAP na
mradi wa usafirishaji umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga katika msongo
wa kilovolti 400 (BITP) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Lengo
la ziara hiyo lilikuwa ni kuona hatua za utekelezaji, mafanikio na
changamoto za miradi hiyo pamoja na kupata maoni ya wanufaika wa miradi
hiyo.
Akielezea
mradi huo Mhandisi Msigwa alisema ujenzi wa kituo hicho uliogharimu
Dola za Marekani Milioni 7, ulianza mwaka 2011 na kukamilika mapema
Desemba mwaka 2013.
Alisema
kabla ya ujenzi wa kituo hicho, umeme ulikuwa unasafirishwa kutoka
katika kituo cha Kiyungi kilichopo mkoani Kilimanjaro hadi jijini Arusha
umeme ambao ulikuwa hautoshelezi katika matumizi ya majumbani na
katika viwanda vidogo.
Aliongeza kuwa pia kulikuwepo na tatizo la kupotea kwa umeme mwingi kutokana na kusafirishwa katika umbali mrefu.
Alisema
kuwa tangu kukamilika kwa kituo hicho wateja zaidi ya 89,000
waliunganishiwa umeme ambapo mpaka sasa wanapata umeme ambao ni wa
uhakika.
Alisema
kutokana na ongezeko la wateja pamoja na kupatikana kwa umeme wa
uhakika katika mkoa huo, TANESCO imeweza kukusanya shilingi bilioni
tisa kwa mwezi tofauti na kipindi cha awali ambapo makusanyo yalikuwa
yanafikia wastani wa shilingi bilioni nane kwa mwezi.
Aliendelea
kusema kuwa kukamilika kwa kituo hicho kumehamasisha kuongezeka kwa
ujenzi wa nyumba pamoja na kuanzishwa kwa viwanda vidogo katika mkoa
wa Arusha.
Wakati
huo huo Julius Urassa ambaye ni msimamizi wa kampuni inayojihusisha na
uzalishaji wa kokoto ya Ravji Aggregate Limited iliyopo wilayani Arumeru
mkoani Arusha alisema kuwa kabla ya kukamilika kwa kituo hicho hali
ya umeme katika mkoa wa Arusha haikuwa nzuri.
“
Kabla ya kuwepo kwa kituo cha KIA, umeme ulikuwa unakatika mara kwa
mara na kuathiri uzalishaji katika kiwanda chetu; lakini sasa tunapata
umeme wa uhakika,” alisema
Aliogeza
kuwa kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika, kampuni yake ina
uwezo wa kuzalisha tani 100 za kokoto kwa siku tofauti na zamani ambapo
walikuwa na uwezo wa kuzalisha kati ya tani 40 hadi 60 za kokoto kwa
siku.
Naye
Meneja wa Kampuni inayojihusisha na utengenezaji wa matofali kwa njia
ya umeme ya Melck Hardware iliyopo Maji ya Chai nje kidogo ya jiji
la Arusha, Hansi Said alisema kuwa hali ya umeme katika mkoa wa Arusha
imetengemaa hali iliyopelekea uzalishaji kuongezeka katika kampuni
yake.
Alisema
kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika, kampuni yake ambayo
hutengeneza matofali kulingana na oda kutoka kwa wateja, imeongeza
uzalishaji kutoka wastani wa tofali 700 hadi 2,000 kwa siku.
Naye
John Augustino mkazi wa Arumeru mkoani Arusha aliongeza kuwa tangu
kuanza kupatikana kwa umeme wa uhakika, hali ya maisha katika familia
yake imeboreka kutokana na kuuza bidhaa zaidi ya maziwa tofauti na
mwanzo katika duka lake.
“Bidhaa
za vinywaji hususan maziwa yalikuwa yanaharibika kutokana na
kukatika kwa umeme, lakini kwa sasa tunapata umeme wa uhakika, hali
inayochangia kuuza bidhaa bora zaidi,”alisisitiza.
No comments:
Post a Comment