Mwenyekiti
wa Bodi ya Wahandisi nchini Prof. Ninatubu Lema (kulia) na Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje wa Norway, Tone Skogen (kushoto) wakisaini Makubaliano
ya Awali ya Programu ya kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi wanawake
walioko vyuoni yenye lengo la kuongeza idadi ya Wahandisi waliosajiliwa
kwa ngazi ya Ushauri.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wahandisi nchini Prof. Ninatubu Lema (kulia) na Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje wa Norway, Tone Skogen (kushoto) wakibadilishana Hati
za Makubaliano ya Awali ya Programu ya kuwasaidia na kuwaendeleza
Wahandisi wanawake walioko vyuoni yenye lengo la kuongeza idadi ya
Wahandisi waliosajiliwa kwa ngazi ya Ushauri leo jijini Dar es salaam.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani
akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Tone Skogen
(Katikati) kuhusu Mafanikio wanayoyapata Wahandisi Wanawake wa Tanzania
kutokana na msaada wa Mafunzo ya kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi
wanawake walioko vyuoni kutoka Serikali ya Norway.
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani
akijadiliana jambo na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne –Marie
Kaarstad wakati wa kusaini Makubaliano ya Awali ya Programu ya
kuwasaidia na kuwaendeleza Wahandisi wanawake walioko vyuoni yenye
lengo la kuongeza idadi ya Wahandisi waliosajiliwa kwa ngazi ya Ushauri
leo jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wahandisi Nchini (ERB) Prof. Ninatubu Lema akieleza
mafanikio ya uhusiano mwema kati ya Tanzania na Norway katika kusaidia
Wahandisi Wanawake walioko nchini.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Tone Skogen (katikati), akiwa na baadhi
ya Wahandisi Wanawake walionufaika na Programu ya kuwasaidia na
kuwaendeleza Wahandisi wanawake walioko vyuoni na baadhi ya Viongozi
wa ERB.
Msajili
wa Wahandisi (ERB) Eng. Steven Mlote akielezea mafanikio yaliyopatikana
tangu kuanza kwa Ushirikiano katika masuala ya Uhandisi kati ya ERB na
Serikali ya Norway.
Serikali ya Tanzania na Norway zimesaini makubaliano yatakayowawezesha
Wahandisi wanawake wanaohitimu na kufaulu masomo yao katika vyuo
vikuu nchini kujengewa uwezo kupitia mafunzo kwa vitendo katika
makampuni mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo katika fani hiyo.
Pia makubaliano hayo yatawawezesha wahitimu hao kusajiliwa na na Bodi
ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB), kupata ajira kwenye makampuni
na taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na ujenzi pamoja na
kujengewa uwezo wa kuanzisha makampuni yao wenyewe.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa Makubaliano hayo jijini Dar es
salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani ameishukuru Serikali ya Norway kwa kuonyesha njia kwa kuwa
msaada utakaotolewa na Serikali hiyo utasaidia kuboresha maisha ya
wanawake wahandisi wanaohitimu vyuo vikuu kote nchini.
Amesema kupitia makubaliano hayo Norway itatoa fedha za awamu ya pili
ili kuwezesha Programu hiyo kutekelezwa hapa nchini ikiwa ni pamoja
na kutoa kiwango cha gharama halisi itakayotolewa na Serikali hiyo
kufuatia mchanganuo utakaotolewa na watalaam.
"Leo tumesaini makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Norway na
Tanzania kupitia Bodi ya Usajili wa wahandisi kuwasaidia wanafunzi wa
kike wanaomaliza vyuo vikuu hapa nchini katika Fani ya Uhandisi ili
waweze mafunzo kwa vitendo ili kuwawezesha kupata Usajili wa Bodi
hiyo", Ameeleza Eng.Ngonyani.
Amesema programu hiyo imejirudia baada ya ile ya kwanza kukamilika
ambayo Norway ambapo Serikali hiyo ilitoa kiasi cha Dola za Kimarekani
milioni 2 kusaidia mpango huo na kuongeza kuwa fedha zilizotolewa
zimewanufaisha wahandisi wanawake wapatao 297 hivyo kuchangia kukuza
ajira nchini.
Aidha, amesema kupitia mfumo huo ERB huwatafutia nafasi za mafunzo kwa
vitendo wahitimu hao kwa waajiri mbalimbali wenye makampuni
yaliyosajiliwa yenye wahandisi washauri ambao hupewa jukumu la
kuwasimamia hadi wanapohitimu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Tone Skogen
akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo amesema kuwa
Serikali ya Norway imeridhishwa na kufurahishwa na juhudi za kuongeza
Wahandisi wanawake inayofanywa na Serikali kupitia Bodi ya Usajili
wa Wahandisi nchini (ERB).
Amesema hatua hiyo ya Serikali ya Tanzania kutoa udahili kwa wanafunzi
Wahandisi Wanawake wengi ni moja ya juhudi za kuimarisha jamii na
uchumi wenye nguvu kama ilivyofanyika nchini Norway kuanzia mwaka
1970.
Bi. Skogen amebainisha kuwa kupitia mafanikio yaliyooneshwa na
Serikali ya Tanzania Norway itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali
kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania ( ERB) kuhakikisha kuwa
Wahandisi Wanawake Tanzania wanachangia kukuza uchumi wa Tanzania.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Prof.Ninatubu
Lema akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo
ameishukuru Serikali ya Norway kwa ushirikiano inaouonyesha wa
kuwasaidia Wanawake wanaosomea na kuhitimu fani ya Uhandisi.
Amesema kupitia Programu hiyo Wahandisi wanawake Tanzania ambao wako
vyuoni na wale wanaohitimu mafunzo wanapata hamasa ya kuendelea
kufanya vizuri zaidi kutokana na mchango wao kutambuliwa na
kuthaminiwa katika jamii tofauti na miaka iliyopita.
"Ninakumbuka mwaka 1970 wakati Chuo Kikuu cha Dar es salaam
kilipoanzisha kitivo cha Uhandisi kulikua kulikua na akina mama
wachache sana kikiwa na wahandisi wanawake 2 tu mwaka 1978, sasa hivi
hali hii imebadilika, sasa kuna mwamko mkubwa huu ni ushahidi tosha
wa maendeleo ya fani ya uhandisi nchini" Amebainisha Prof. Lema.
Amesema programu hiyo imesaidia kuwahamasisha wanafunzi wanawake walio
vyuoni na shule za sekondari kufanya vizuri kwa kuwa mara baada ya
kuhitimu masomo ya Uhandisi na kufanya vizuri hupewa ufadhili kupitia
programu hiyo ili waweze kutambuliwa na kusajiliwa.
Amesema kwa sasa Tanzania inahitaji Wahandisi wengi kwa kuwa mkakati
uliopo ni kuifanya Tanzania iwe nchi ya uchumi wa Kati ambayo uchumi
wake utategemea uanzishwaji wa viwanda ambavyo ufanisi na uendeshaji
wake utategemea Wahandisi waliopo nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa suala la usawa wa kinjinsia katika udahili wa
Wahandisi wanawake kwenye mafunzo linapewa kipaumbele na Bodi hiyo kwa
kutoakana na matunda mazuri yanayoonyeshwa na Wahandisi wanawake
kupitia kazi wanazopewa kwa kuwa huzifanya kwa ubora na viwango.
No comments:
Post a Comment