Ndugu Mweshimiwa mgeni rasmi, mh Mwantumu Mahiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga,
Ndugu wajumbe wenzangu wa Mkutano Mkuu
Ndugu wageni waalikwa.
Salam aleikum,
Nianze
kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa ajili ya
aliyotujalia na kutufanikisha kuwepo hapa leo. Ni kwa Rehema zake
Mwenyezi Mungu tumeweza kujumuika hapa leo.
Ninaomba nichukue fursa hii kuwaomba wote tusimame ili kuwarehemu waliotangulia mbele ya haki.
Ndugu
zangu, kama mnavyofahamu tarehe 25/10/2015 nchi yetu ilifanya Uchaguzi
Mkuu. Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wetu Mpendwa Dr John Pombe
Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wetu pamoja na Makamu wa Rais Mama
Samia Suluhu. Pongezi za pekee ni kwa Mh. Nape Nnauye kwa kuteuliwa kuwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo na Mh Anastacia Wambura
kuwa Naibu Wake.
Pongezi za kipekee kwa wanafamilia ya mpira wa miguu Tanzania ambao wamepata nyadhifa kama ifuatazo:
1. Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa, ameshinda nafasi ya ubunge wa jimbo la Ruangwa na pia kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
2.
Mstahiki Paschal Kihanga, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Mkoa wa
Morogoro, alishinda udiwani na pia amepata wadhifa wa Meya wa Manispaa
ya Morogoro.
3. Mh John Kadutu mjumbe wa mkutano mkuu toka Mwanza, ameshinda ubunge jimbo la Ulyankulu.
4. Mh. Maftah Nachuma Katibu wa Chama cha Mpira wa miguu Lindi vijijini ameshinda nafasi ya ubunge jimbo la Mtwara Mjini.
5. Mh.
Leonard Kiganga Bugimala, Mwenyekiti klabu ya Geita Gold Sport
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti Halmashauri ya mji wa Geita na Makamu wake
Mh. Costantian Mdindi pia amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo.
6. Mh. Khalid Mohammed Abdallah Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TFF ameshinda nafasi ya udiwani.
7. Mh Yusuf Kitumbo Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa Tabora, ameshinda udiwani.
8. Mh. Golden Sanga, Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa Ruvuma, ameshinda udiwani.
9. Mh. Bartholmeo Kimario, Mwenyekiti chama cha mpira mkoa wa Singida, ameshinda udiwani.
10. Mh. Omari Kinyento, mjumbe wa Mkutano Mkuu toka Singida ameshinda udiwani.
11. Mh. Omar Gindi, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira Mkoa Kigoma ameshinda Udiwani.
12. Mstahiki James Bwire, Mshirika wa TFF, Mkurugenzi Alliance School kwa kuchaguliwa udiwani na umeya jijini Mwanza.
Tunampongeza pia Makamu wa Rais wa TFF, Ndg Wallace Karia kwa kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba.
Ushindi
huu ni heshima kubwa kwa familia ya mpira wa miguu Tanzania na
unaonyesha jinsi gani watanzania wanathamini na kuenzi mpira wa miguu.
Viongozi wetu hawa tunawaombea mafanikio katika kutimiza majukumu yao.
Ndugu
wajumbe wenzangu wa Mkutano Mkuu, ninawapeni pole sana kwa usumbufu
uliotokana na kuahirishwa Mkutano wetu wa tarehe 19-20 Desemba mwaka
jana, hii ilitokana na sababu ambazo tulizieleza wakati huo. Ufumbuzi wa
matatizo yetu na mamlaka za kodi unaendelea kutafutwa. Ninawashukuru
sana kwa kuitikia wito wa Kamati yetu ya utendaji wa kuhudhuria mkutano
mkuu huu muhimu ulioitishwa kwa mujibu wa Katiba yetu.
Ninaomba
nichukue fursa hii kutoa taarifa ya mambo muhimu ambayo uongozi wetu
umeyatekeleza kati ya kipindi tulichokutana mwezi Machi mwaka jana mjini
Morogoro hadi sasa. Kama nilivyotoa rai kwenye mkutano wetu wa
Morogoro, ninaomba tuyapitie, tuyajadili na kuangalia wapi utekelezaji
haukuwa mzuri ili changamoto hizo ziweze kufanyiwa kazi. Azma yetu ni
kuhakikisha mpira wa Tanzania unakua na sisi tunafikia lengo la kutoa
upinzani wa kutosha katika hatua za Kimataifa kuanzia ukanda wetu wa
CECAFA, Afrika na hatimae kung’ara duniani.
1. Timu ya Taifa (Taifa Stars)
Baada
ya timu yetu ya Taifa , Taifa Stars kutofanya vizuri katika michuano ya
COSAFA huko Afrika Kusini mwezi Mei mwaka jana na baadae kufanya vibaya
katika mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano ya CHAN,Kamati ya
Utendaji ya TFF ilichukua maamuzi ya kusimamisha ajira ya kocha wa
kigeni Martin Nooj na badala yake kuingia mkataba na makocha wazawa
Boniface Charles Mkwasa akisaidiana na Hemed Morocco. Tangu walimu hawa
wemechukua timu ya Taifa imeboreka na hadi sasa tumefungwa mechi mbili
tu za mashindano dhidi ya Algeria na Malawi ugenini, tumetoka sare mbili
nyumbani dhidi ya Nigeria na Algeria na kuifunga Malawi nyumbani.
Aidha
timu ya Kilimanjaro Stars chini ya kocha Abdalla Kibadeni na msaidizi
wake Juma Mgunda katika mashindano ya CECAFA Challenge katika mechi nne
ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja katika “Open Play”
ingawa ilitolewa kwa penati tano tano katika hatua ya nusu fainali.
Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha wazawa kiwango cha Tanzania
FIFA kimekuwa kikipanda mara zote. Tunawapongeza sana makocha wetu hawa
na benchi la ufundi.
Kwa
sasa tunajiandaa na mechi za kufuzu kucheza fainali za Afrika AFCON
2017 nchini Gabon. Mechi hizi ni dhidi ya Tchad tarehe 23/03/2015
ugenini Ndjadema na mechi ya marudiano Dar es Salaam tarehe 28/03/2015.
Imani yetu ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi. Katika
kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Nigeria Taifa stars iliweka kambi
nchini Uturuki na pia timu iliweka kambi Afrika kusini kujiandaa na
mechi dhidi ya Algeria. Kambi hizi zimesaidia sana kuimarisha timu yetu
kabla ya mechi hizi kubwa mbili.
2. Timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars.
Timu
yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars chini ya kocha Rogasian Kaijage
ilifanikiwa kuitoa Zambia na hivyo kufuzu kucheza fainali za michezo ya
Afrika nchini Kongo Brazaville. Katika fainali hizi Tanzania ilifungwa
na Ivory Coast na Nigeria na kutoka sare na Congo, hivyo kutolewa katika
hatua za makundi. Uzoefu uliopatikana katika mashindano hayo umempa
fursa kocha mpya wa Timu ya Twiga stars Bi Nasra kuweza kuunda kikosi
kipya kichanga ambacho majuzi kilitoa changamoto kwa timu ya Zimbabwe,
imani yetu ni kwamba hii timu itafanya vizuri mechi ya marudiano mjini
Harare. Aidha timu ya Twiga stars ilipata mechi moja ya majaribio dhidi
ya Malawi.
3. Udhamini na Michuano Mipya.
Ninayo furaha kuwajulisha wajumbe wenzangu wa mkutano mkuu kuwa katika kipindi hiki tumefanikiwa katika maeneo yafuatayo:
3.1 Kufufuliwa Kombe la Shirikisho.
Kwa
kushirikiana na mdhamini Azam Sport Kombe la Shirikisho limefufuliwa na
kuboreshwa. Kwa mwaka huu tumeanza na timu 64 ambazo ni za ligi Kuu
(16), Ligi daraja la kwanza FDL (24) na Ligi daraja pili SDL (24). Ili
kupanua uwigo wa ushiriki wa Mikoa kwa misimu ya usoni timu mabingwa wa
mikoa (RCL) nazo zitashirikishwa katika mashindano haya ili kila mkoa
wa Tanzania ushiriki katika mashindano haya. Kwa sasa mashindano haya
yako hatua ya robo fainali na yana ushindani mkubwa. Inatia moyo kuwa
mpaka hatua hii bado kuna timu moja ya ligi daraja la kwanza ya Geita
Gold ambayo bado inapambana. Bingwa wa Kombe hili atawakilisha Tanzania
katika Kombe la Shirikisho la Afrika.
3.2 Udhamini Ligi Daraja la Kwanza.
Tumefanikiwa
kupata udhamini wawili kwa ligi daraja la kwanza FDL. Tumempata
STARSTIMES ambaye ndiye mdhamini mkuu wa ligi na pia kampuni za
Television ya Sahara Media kupitia STAR TV imepewa haki za kuonyesha
mechi hizi moja kwa moja. Haya ni mafanikio makubwa kwa ligi ya Daraja
la kwanza kwani pia soko la wachezaji hawa litapanuka kwa kuwa
wanaonekana moja kwa moja na pia itakuza jina la ligi lenyewe.
Changamoto ya vilabu kucheleweshewa malipo ya udhamini tumeliona na
tunalifuatilia kwa karibu kupata ufumbuzi ili lisitokee tena.
3.3 Mkataba wa Vodacom na Ligi Kuu.
Kampuni
ya Vodacom baada ya mzungumzo marefu tuliafikiana na kusaini mkataba
mwingine wa miaka mitatu wa udhamini wa Ligi Kuu wenye ongezeko la
thamani ya udhamini kwa asilimia 40%. Jitihada zimefanyika kuvutia
wadhamini wengine nao waje waongeze udhamini kwa ligi kuu.
Tunashukuru
mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF umeitikia wito. Vilabu vya Ligi
Kuu na ligi Daraja la Kwanza navyo vimeongeza jitihada za kupata
wadhamini, tunayashukuru makampuni ya madini ya ACACIA (Stand United))
na Geita Gold Mining (Geita Veterans) kwa kujitolea kusapoti mpira.
Tunazidi kutoa wito kwa makampuni mengine yajitokeze kutoa udhamini
ikiwa ni sehemu ya kutangaza biashara zao.
3.4 Udhamini Tarajiwa.
Tunatarajiwa
kupata wadhamini kwa ajili ya Ligi Kuu ya vilabu vya wanawake (Women
Premier League) pamoja na ligi ya vilabu vya Ligi Luu ya vijana chini ya
umri miaka 20 (U20).
Jambo
hili likifanikiwa matumaini yetu ni kuwa tutaanzisha ligi mpya mbili, ya
vilabu vya wanawake Women Premier League na ya vilabu vya Ligi Kuu kwa
vijana umri chini ya miaka 20. Hii itasaidia sana kuinua kiwango cha
mpira wetu kwa wanawake na wanaume.
4. Soka la Vijana.
4.1 Fainali za Afrika za vijana U17 mwaka 2017.
Kikosi
chetu cha Taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 17 (U17)
kinachojiandaa na hatua za mtoano mwezi juni, 2016 ilikuwa kifanye ziara
ya kimichezo kwenda Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya. Lengo lilikuwa ni
kukipatia kikosi hiki uzoefu wa kimataifa. Wakati tayari kikosi
kimejiandaa na kukabidhiwa bendera, akaunti za TFF zilifungiwa na TRA na
hivyo safari kuvunjika kwa ukosefu wa fedha. Pamoja na changamoto hiyo
mpango mkakati umefanyika na sasa kikosi hiki kitacheza moja ya kirafiki
ya kimataifa hapa Tanzania mwezi April na baadae kwa hisani ya Chama
cha Mpira cha India timu itakwenda India kuweka kambi ya wiki tatu
tayari kwa kuikabili Seychelles mwezi Juni. Tunakishukuru Chama cha
Mpira cha India pamoja na serikali ya India kwa kutupatia sapoti hii.
4.2 Fainali za Afrika U17 mwaka 2019.
Maandalizi
ya fainali hizi ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji yanaendelea vizuri na
vikao na Wizara tayari vimeanza kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu
ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Pia maandalizi ya timu
itakayoshiriki fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya miaka 13
(U13) kujumuisha pamoja katika shule ya Alliance mjini Mwanza. Mwalimu
Kim Poulsen tumemleta mahsusi ili pamoja na majukumu mengine, atuandalie
kikosi cha ushindi cha vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
Imani yetu ni kuwa Tanzania tutafanikiwa kuandaa mashindano mazuri mwaka
2019 na pia kunyakua kombe hili.
4.3 Mashindano ya Olimpiki Tokyo 2020
Tumedhamiria
kushiriki fainali za Olimpiki Tokyo mwaka 2020. Ili kufanikisha lengo
hili zoezi la kuwapata vijana wenye umri stahiki (waliozaliwa mwaka 1997
na kuendelea) limeanza. Chini ya uangalizi wa Kocha Poulsen tunaamini
tutaweza kujenga kikosi imara cha kufaulu kushiriki fainali hizi.
Kwa
kuweza kujenga vikosi imara vya U17 mwaka huu na mwaka 2019 na pia kuwa
na timu nzuri ya Olimpiki Tokyo 2020 imani yetu ni kuwa hiki kizazi
tunachokijenga na kukikuza ifikapo mwaka 2026 kitaweza kutuvusha
tucheza fainali za kombe la dunia inshallah.
4.4 Vituo vya mikoa vya kukuza na kuendeleza vipaji.
Kama
nilivyoainisha kwenye mkutano wa mwezi Machi mjini Morogoro, azma ya
TFF ni kuhakikisha kuwa kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa kinakuwa
na kituo mama cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira. Mkataba wa
mfano (template) umekwisha pelekwa mikoani ili vyama vya mikoa kama
havina vituo vyake basi viingie mkataba wa ushirikiano na kituo kimoja
kwa lengo la kukifanya kiwe kituo mama cha Mkoa. Kupita vituo hivi TFF
itaweza kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira wa vijana katika mikoa
yetu na kuongeza nguvu kwa kuvipatia vifaa na walimu.
Mipira
5000, koni 3000, na beeps 2000 tayari vimeagizwa toka nje ya nchi kwa
kutumia vyanzo vya fedha vya TFF yenyewe bila kuomba msaada kwa ajili ya
kuendeleza program hii. Tayari kila mkoa una mwalimu angalau mmoja
aliyefanya kozi ya FIFA ya ukocha isipokuwa mikoa miwili tu Manyara na
Njombe. Hivyo mtaji wa kutosha tunao wa kuanzisha vituo hivi. Shime
viongozi wenzangu wa mikoa tujidhatiti tuweke nguvu katika uwanzilishaji
na uendelezaji wa vituo hivi ambavyo vitakuwa chachu kuu ya kutoa
wachezaji wa Taifa wa kike na wa kiume.
Imani
yetu ni kuwa vituo hivi vikiimarika vitakuwa ni chachu ya kuendeleza
vituo vingine ambavyo vitamilikiwa na vyama vya mpira vya wilaya,
vilabu, taasisi binafsi, mashule nk. Kwa utaratibu baadae tutaweza kuwa
tunaratibu mashindano kati ya vituo hivyo ngazi ya wilaya, mikoa, kanda
na hatimae Taifa ili tuweze kutafuta wachezaji bora wa kuimarisha timu
zetu na hatimae kuwa na timu za kuleta mafanikio Kimataifa kwa siku
zijazo.
Tunashukuru
tumeweza kupata ardhi yetu wenyewe katika mikoa ya Tanga na Manyara.
Ninarudia kutoa wito kwa viongozi wote wa mikoa tuzidi kukamata ardhi
mikoani kwetu ili hatimae tuweze kujenga vituo vya kukuza na kuendeleza
vipaji, centres of excellency.
5. Kozi mbali mbali.
Kwa
kushirikiana na CAF na FIFA Shirikisho letu limeandaa kuratibu na kutoa
kozi mbali mbali za waamuzi na makocha katika ngazi mbali mbali.
Jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha mikoa iliyokuwa na hazina ndogo
ya makocha na waamuzi inapewa fursa ya kuratibu kozi hizi. Tunashukuru
viongozi wote wa mikoa na wilaya ambao tumeshirikiana nao kutimiza azma
hii. Juhudi zinaendelea ili tuweze kupata kupata makocha, waamuzi,
madaktari wa michezo na watawala bora na wengi zaidi. Ninatoa rai kwa
wakinamama wazidi kujiunga katika kozi hizi maana wana umuhimu wa
kipekee katika maendeleo ya mpira hasa wa wanawake.
6. Vilabu.
Pamoja
na jitihada za kutafuta wadhamini wa mashindano mbalimbali
yanayohusisha vilabu, jitihada pia zinaendelea kufanyika kuhakikisha
vilabu vyetu vinaimarisha utawala bora. Kufuatia CAF na FIFA kuanzisha
utaratibu wa kutoa leseni kwa vilabu (Club Licencing) jitihada sasa
zinafanyika kuhakikisha vilabu vinaelimishwa kwa kina juu ya mahitaji ya
leseni hizi. Katika utaratibu wa leseni za vilabu, vilabu vyetu sasa
vitalazimika kuwa na ofisi, kuwaajiri watendaji wakiwemo makatibu na
watunza kumbukumbu za mahesabu, kuwa na maeneo ya kufanya mazoezi, kuwa
na program ya maendeleo ya mpira wa vijana, kuajiri walimu wenye sifa
nk. Tunaamini utaratibu wa leseni za vilabu ukitekelezwa ipasavyo
uendeshaji wa vilabu vyetu utaboreshwa na hivyo kuongeza tija kwa vilabu
vyetu.
7. Kitega uchumi Karume.
Jitihada
za kuendeleza kiwanja chetu uwanja wa Karume, kama tulivyoahidi,
zinaendelea. Tayari tumekwisha malizia kujenga chumba ambacho kitakuwa
ni duka la TFF la kuuzia vifaa vya michezo na pia ujenzi wa chumba
kingine utakapowekwa mgahawa unaendelea. Kwa sasa tunashugulikia kupata
mashine ya TRA ya tozo ya kodi (EFD machine) ili tuweze kufungua duka
letu la vifaa vya michezo.
8. Tiketi za Elektroniki.
Kutokana
na matatizo yaliyojitokeza matumzi ya tiketi ya elektronik
yalisimamishwa na mmiliki wa uwanja wa Taifa ambaye ni Serikali. Baada
ya mazungumzo na mwenye mkataba ambaye ni Benki ya CRDB ilikubaliwa
apatikane mshauri mtaalam wa kupitia mfumo mzima na kupendekeza
marekebisho. Baada ya tenda kutangazwa mtaalam amepatikana na sasa
anasubiriwa aanze kazi hiyo. Lengo ni kuhakikisha utaratibu wa tiketi za
elektronik unaanza kutumika msimu ujao wa ligi.
9. Mfuko wa maendeleo ya mpira (Football Development Fund).
Baada
ya mfuko huu kuanzishwa kikatiba katika mkutano mkuu uliopita, kamati ya
utendaji ya TFF iliteua wajumbe wa kamisheni ya uendeshaji wa mfuko
huu chini ya mwenyekiti Ndugu Tido Mhando. Lengo la mfuko huu kama
ilivyoanishwa ni kuwa chanzo kikuu cha kupata rasilimali kwa ajili ya
maendeleo ya mpira wa miguu nchini mwetu. Ninaomba tuwaunge mkono na
kuwapa ushirikiano watendaji wa mfuko huu huku tukitambua kuwa maendeleo
ya mpira wa miguu yanahitaji rasilimali nyingi.
PONGEZI MAALUM
Ninaomba
nichukue fursa hii kumpongeza tena Bwana Gianni Infantino kwa
kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa FIFA. TFF tulishiriki kikamilifu katika
mchakato mzima wa uchaguzi huu. Tunaamini chini ya uongozi wake
mabadiliko makubwa chanya yatatelezwa katika mpira wetu.
Aidha
nirudie tena kumpongeza kijana wetu Mbwana Samatta kwa kuteuliwa kuwa
mwanamichezo bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya bara letu
na pia kwa kufanikiwa kupata fursa ya kucheza katika ligi kuu ya
Ubelgiji. Tunazidi kumuombea na kumtakia mafanikio.
Ndugu
wajumbe wa Mkutano Mkuu baada ya kuyasema haya ninaomba nirudie
kuwashukuru wote kwa kuhudhuria kwenu mkutano huu, ninaomba Mola
aubariki Mkutano wetu ili tutakayojadili na kukubaliana yawe ni ya kheri
na yajenge mpira wetu.
Ahsanteni sana.
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
Tanga
12 MARCH 2016
No comments:
Post a Comment