
Msaada huo umetolewa na Shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza (Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF) kwa lengo la kurahisisha kazi kwa watoa huduma ya afya kwa ngazi ya jamii ambao hufanya kazi na shirika hilo kuelimisha jamii kuhusu VVU na UKIMWI.Zoezi la kugawa baiskeli hizo limefanyika Februri 02,2016 na Februari 03,2016.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga
Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali AGPAHI (Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI limetoa msaada wa baiskeli 104 kwa watoa huduma ya elimu ya VVU na UKIMWI ngazi ya jamii katika halmashauri nne za wilaya mkoani Shinyanga. Zoezi la kugawa baiskeli hizo limefanyika jana na leo ambapo Halmashauri zilizopata msaada huo ni Halmashauri ya Mji Kahama iliyopata baiskeli 25, Halmashauri ya Msalala baiskeli 32, Halmashauri ya Ushetu 27 na Manispaa ya Shinyanga iliyopata baiskeli 20. Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli hizo ,Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii kutoka Shirika la AGPAHI, Cecilia Yona alisema msaada huo umetolewa na Shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Mfuko wa kusaidia watoto wenye VVU wa watu wa Uingereza (Children’s Investment Fund Foundation UK - CIFF) ambao ni moja ya wafadhili wa shirika la AGPAHI “Mfuko huu wa CIFF unafadhili mradi wa kusaidia kuongeza usajili wa watoto waishio na VVU kupata huduma za tiba na matunzo, hivyo, lengo la ufadhili wa baiskeli hizi ni kurahisisha kazi kwa watoa huduma ya afya kwa ngazi ya jamii ambao hufanya kazi na shirika hili”, alisema Yona. “Matumaini yetu ni kwamba baiskeli hizi zitatumika kwa ajili ya kufuatilia wateja waliopotea katika huduma ya kupata dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARV’s),kufuatilia watoto chini miaka miwili, wajawazito, wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka 15 wanaoishi na VVU pamoja na kuisaidia jamii kupata elimu ya VVU na UKIMWI", aliongeza Yona. Yona aliwataka watoa huduma wa afya waliopata baiskeli hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa huku akiwasisiza juu ya umuhimu wa kufuatilia wateja waliopotea kwani taifa linapoteza nguvu kazi kutokana na baadhi ya watu waliopata maambukizi ya VVU kutozingatia masharti waliyopewa na wataalam wa afya ikiwemo kuacha kabisa kutumia dawa za ARV’s. "Bado kuna changamoto ya wateja wetu kuacha kutumia dawa hasa wanapoona miili yao ina nguvu lakini pindi tu miili ikianza kudhoofika hukimbilia hospitali,naomba jamii ibadilike,na kupitia baiskeli hizi mtawafikia wale wote waliopotea katika huduma",alieleza Yona. Naye Meneja mradi kutoka AGPAHI mkoa wa Shinyanga Dkt Gastor Njau alitumia fursa hiyo kuwataka watoa huduma ya afya majumbani kuwafikia watoto wenye maambukizi ya VVU kwani bado watoto wengi hawajafikiwa na kuamini kuwa baiskeli hizo watazitumia kuwafikia watoto walio wengi zaidi. Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Kahama Dkt Samwel Mwalutambi mbali na kulishukuru shirika hilo kwa kuwajali watoa huduma ya afya majumbani aliwataka waliopata baiskeli hizo kuzitunza kama zao huku akiahidi uongozi wa wilaya kusimamia baiskeli hizo katika vituo vyao vya afya kwa maslahi ya jamii nzima. Naye Muuguzi mkuu katika Kituo cha afya Lunguya halmashauri ya Msalala Pili Paulo alisema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni wateja wengi kukatisha huduma hali inayowawia ugumu kuwapata ili warudi katika huduma ya tiba kutokana na eneo lao kuzungukwa na migodi hivyo watu wanakuja na kuondoka katika eneo hilo. Msimamizi wa kituo cha Huduma na Matunzo kwa watu wanaoishi na VVU kilichopo katika hospitali ya mji wa Kahama, Dkt John Malulu alisema hivi sasa hali ya unyanyapaa kwa wagonjwa wa UKIMWI imepungua ukilinganisha na miaka iliyopita na kilichobaki sasa ni unyanyapaa wa watu binafsi kuogopa kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya VVU au la. Kwa upande wao baadhi ya watoa huduma ya afya waliopata msaada huo, Stella Paul na Nobert Zephania walisema kabla ya kupata baiskeli walikuwa wanalazimika kutumia gharama zao kuwafikia wateja wao hivyo baiskeli hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuifikia jamii. AGPAHI ni shirika la kitanzania lisilo la kiserikali linalojishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI,kutoa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,kutoa huduma ya uchunguzi na huduma za awali ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango.
No comments:
Post a Comment