Meneja wa kinu cha kuchenjua dhahabu wa Mgodi wa Buzwagi Festo Shayo
(wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa Naibu waziri ofisi ya makamu wa
rais anaeshughulikia mazingira na Muungano, Luhaga Mpina namna mgodi
wake unavyohifadhi maji yaliyotumika kusafishia dhahabu.
Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga
Mpina, ameupongeza Uongozi na wafanyakazi wa Mgodi wa Buzwagi kwa
kuzingatia sheria za mazingira Mgodini hapo.
Pongezi
hizo alizitoa wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika Mgodi huo
kwa lengo la kujionea namna mwekezaji huyo anavyozingatia maelekezo ya
wataalamu wa wizara yake juu ya utunzaji wa mazingira.
Akiwa
katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo alitembelea bwawa maalumu kwa ajili
ya kuhifadhia maji yalitumika kuchenjulia dhahabu na kujionea namna
ambavyo mgodi huo unavyochukua tahadhari ya hali ya juu katika
kuhakikisha maji yanayohifadhiwa ndani ya bwawa hilo hayawezi kuwa na
madhara kwa Jamii, pia naibu Waziri huyo alitembelea kituo cha udhibiti
taka, Uwanda wa kuvuna maji ya mvua mgodini hapo pamoja na karakana ya
mgodi huo.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano Luaga Mpina (wa
kwanza kushoto), akisikiliza maelezo ya Afisa Mazingira wa Mgodi wa
Buzwagi bwana Frank Ngoroma (wa kwanza mkono wa kulia), aliyesimama
katikati ni meneja mkuu wa mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo.
“Bwawa
hili kama unavyoliona usanifu wake, umezingatia tahadhari zote
kuhakikisha hakuna maji yoyote yanatoka nje na hasa ukizingatia maji
yanayopatikana hapa ni yenye mchanganyiko wa madawa yanayotumika
kuchenjua dhahabu” Alisema Meneja wa Kituo cha Uchenjuaji dhahabu bwana
Festo Shayo, wakati alipokuwa akitoa maelezo juu bwawa hilo.
Kwa
upande wake naibu Waziri Mpina amesema licha ya kufanya ziara katika
Migodi mingi bwawa la kuhifadhia maji yanayotoka katika kinu cha
kuchenjulia dhahabu la Buzwagi ni la kiwango cha juu na ameitaka Migodi
mingine pia kutembelea kwa lengo la kujifunza usanifu wake.
“Ni
seme tumepita maeneo mengi ila hapa mmejitahidi kuhakikisha wananchi
wanaowazunguka wako salama, nafikiri kuna haja ya migodi mingine kuja
kujifunza hapa, karakana yenu pia ni nzuri na inazingatia utunzaji wa
mazingira. Alisema mh Mpina.
Naibu
Waziri pamoja na wataalamu wake wakikagua moja ya maeneo ambayo NEMC
yalitoa ushauri kuwa yafanyiwe kazi katika ziara zao, ambapo wakati wa
ziara hii utekelezwaji wake ulikutwa umeisha kamilika kama walivyokuwa
wameelekezwa.
Aidha
akiwa katika kituo maalumu cha udhibiti taka Mgodini hapo Naibu Waziri
huyo ameutaka uongozi kujenga paa kwenye eneo la udhibiti wa taka za
vyuma ili kuzuia maji ya mvua kugusa taka hizo.
“Mmejitahidi
kuhakikisha taka zinawekwa katika utaratibu mzuri, ila kukosekana kwa
paa hapa ni tatizo, hivyo nawaagiza ndani ya siku therathini eneo hili
liwe na paa” alisema Naibu Waziri Mpina.
Awali
akiukaribisha ugeni wa naibu Waziri huyo Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi
Mhandisi Asa Mwaipopo alimueleza naibu Waziri huyo kuwa sekta ya madini
kwa sasa duniani imekumbwa na changamoto ya kuporomoka kwa bei ya
dhahabu, hali ambayo imepelekea wawekezaji wengi kujikuta wakijiendesha
kwa hasara.
“Mheshimiwa
naibu Waziri, Mgodi wa Buzwagi toka uanze shughuli zake umekuwa
ukishirikiana na Jamii katika kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo
na tunaendelea kufanya hivyo, Hata hivyo changamoto ni kubwa kwani kila
siku bei ya dhahabu inashuka na hii inatufanya tushindwe kujiendesha kwa
faida”alisema Mwaipopo.
“Tumeanza
mchakato wa maandalizi ya kusitisha shughuli za uchimbali maana gharama
zinazidi kuwa kubwa hata hivyo kama bei ya soko itabadilika tutafikiria
vinginevyo” aliongeza Mwaipopo.
Akizungumzia
hatua ya mgodi huo kutaka kusitisha shughuli za uchimbaji naibu Waziri
Waziri ofisi ya makamu wa rais anaeshughulikia mazingira na muungano
Luaga Mpina, amewaomba wawekezaji hao kuangalia namna ingine
itakayowawezesha kuchimba kwa gharama ndogo inayoendana na bei ya
dhahabu.
“kwa
kweli serikali inawahitaji sana wawekezaji na tunaposikia mnaondoka
kwetu sisi ni hasara kwa sababu kodi mbalimbali ambazo mmekuwa mkilipa
kwa halmashauri ya mji wa Kahama hazitakuwepo tena na hii itafanya
miradi mingi ya Maendeleo isitekelezeke baada ya ninyi kuondoka,
tunawaombea bei ya dhahabu ipande ili muendelee kuwepo” Alisema Mpina.
Ziara
hiyo ya kushitukiza ili lenga kujionea namna ambavyo mgodi wa Buzwagi
unazingatia maelekezo mbalimbali ya wataalamu wa wizara yake.
Mh Luhaga Mpina akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo katika eneo la kituo cha Uthibiti wa taka mbalimbali mgodini hapo.
Mmoja wa maafisa wa mazingira aliyekuwa ameandamana na naibu Waziri akiuliza jambo wakati wa ziara hiyo.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo akifafanua jambo wakati wa ugeni wa naibu Waziri wa mazingira.
Baadhi
ya maofisa wa Mgodi wa Buzwagi wakitoa maelezo mbele ya Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira na Muungano Luaga Mpina
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Shinyanga.
Na Dixon Busagaga wa Kanda ya Kaskazini.
No comments:
Post a Comment