Ndege moja ya abiria ya Air France Boeing 777 AF463, inayohudumu kati ya Mauritius na Paris imelazimika kutua kwa ghafla katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Mombasa - Kenya baada ya kifaa kinachodhaniwa kuwa bomu kupatikana ndani ya choo cha ndege hiyo.
Mhudumu mmoja wa ndege hiyo alimfahamisha rubani kuhusiana na kifaa hicho ndipo shughuli za kutua kwa dharura zikaanza.
Katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter, kamanda mkuu wa polisi nchini Kenya Jenerali Joseph Boinnet, amesema kuwa ndege hiyo iliyokuwa njiani kuelekea Paris Ufaransa ikiwa na abiria 473 na wahudumu 14 ilitua salama na abiria wote kuokolewa.
Bomu' yasababisha ndege ya Ufaransa kutua Kenya
Ndege hiyo inasemekana kutua saa sita usiku wa kuamkia leo Jumapili, huku wataalamu wa kutegua mabomu kutoka jeshila wanamaji la Kenya wakiingia ndani ya ndege hiyo kukagua kifurushi kilicholeta taharuki.
Habari za hivi punde zinasema kuwa maafisa wa upelelezi wanasemekana kuwa wamewatambua washukiwa wawili abiria wa ndege hiyo.
Shirika linalosimamia viwanja vya ndege nchini Kenya linasema kuwa kifaa hicho kimeondolewa ndani ya ndege hiyo.
Shughuli za kawaida za usafiri zimerejea katika uwanja huo wa ndege baada ya kusitishwa ilikukabiliana na tishio hilo.
BBC
No comments:
Post a Comment