|
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
|
Oktoba 23, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tamko
la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuhusu umuhimu wa
kuzingatia sheria kwa ajili ya Uchaguzi Huru, wa Haki na Amani
TUME
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imekuwa ikifuatilia kwa
karibu matamshi mbalimbali ya wanasiasa, viongozi wa vyama vya siasa,
viongozi wa Serikali, Tume ya Uchaguzi, na Jeshi la Polisi kuhusu nini
kifanyike baada ya kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 25, 2015.
Matamshi haya yamesababisha mkanganyiko na malumbano miongoni mwa
viongozi na wananchi pia.
THBUB
inapenda kusema kwamba, licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza
katika baadhi ya maeneo, wakati wa kampeni za uchaguzi, kwa ujumla
kampeni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani zimefanyika nchi nzima
kwa amani na utulivu. Ni wajibu wetu sote kudumisha amani katika nchi
yetu muda wote, wakati wa uchaguzi na baada ya kutangaza matokeo ya
uchaguzi mkuu.
Tume
(THBUB) inawashukuru na kuwapongeza wananchi kwa jinsi walivyoonyesha
utulivu wakati wa mikutano mikubwa ya kampeni, ambayo imekuwa ikivuta
maelfu ya wananchi.
Tume
(THBUB) inatoa pongezi kwa Jeshi la Polisi kwa ulinzi ambao umekuwepo
katika mikutano hiyo. Aidha, inavipongeza vyombo vya habari kwa kazi
nzuri ya kuwapasha wananchi habari mbalimbali za uchaguzi.
Tume
(THBUB) inatambua na kupongeza jitihada zinazofanywa na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi, na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa maandalizi ya uchaguzi.
Tume
(THBUB) inapenda kutahadharisha kwamba malumbano haya ambayo
yanaendelea hayaonyeshi dalili nzuri, pamoja na jitihada za wadau
mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kuhubiri umuhimu wa uchaguzi wa
amani. Malumbano haya yasipotafutiwa ufumbuzi wa haraka, kwa kutumia
busara na kuzingatia sheria, haki za binadamu, na misingi ya utawala
bora, kuna dalili kubwa ya kuwepo vurugu, uvunjifu wa sheria na amani,
kwani pande zote hizi zimeendeleza malumbano na kushikilia misimamo yao.
Tume
(THBUB) inaonya kwamba vurugu zinaweza kutokea, ama kwa makusudi, au
kwa bahati mbaya, iwapo wananchi na wafuasi wa vyama vya siasa
watashikilia misimamo yao, ama watagoma na kukaidi amri ya Polisi.
Lolote katika hayo likitokea, kuna uwezekano mkubwa wa kuvurugika kwa
uchaguzi, na haki za binadamu zitaathirika.
Vile
vile, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesikitishwa na
matamshi yanayoashiria kutoiamini Tume ya Uchaguzi, na hata tuhuma za
uwezekano wa wizi wa kura. Pia kumekuwa na matamshi ya kuwataka wananchi
walinde kura, jambo ambalo halina msingi wowote wa sheria.
Ni
vyema ifahamike kuwa, wajibu wa ulinzi wa kura upo kisheria, na ni
wajibu ambao wamepewa mawakala wa vyama vya siasa na wagombea, ama
wagombea wenyewe, wanaoruhusiwa kuwa ndani ya vituo, wakisaidiana na
wasimamizi wa Tume ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba
taratibu zote zinazosimamia upigaji kura zimefuatwa.
Kwa
mujibu wa Vifungu vya 48(2) na 49 vya Kanuni za Uchaguzi (Urais na
Ubunge) za mwaka 2010, Tanzania Bara, vyama vya siasa vinavyoshiriki
katika uchaguzi vinatakiwa kuteua mawakala wao wa uchaguzi kwa kila
kituo, jambo ambalo Tume (THBUB) inaamini limefanyika. Mawakala
wanatakiwa kula kiapo cha uaminifu.
Vifungu
vya 59 na 60 vya Kanuni za Uchaguzi vinaeleza jinsi wakala wa chama au
mgombea, atakavyoshiriki katika taratibu za kuhesabu kura, na jinsi
malalamiko yatakavyo shughulikiwa na Msimamizi wa Uchaguzi.
Vifungu
vya 61 hadi 66 vya kanuni hizo vinaeleza utaratibu wa kujumlisha kura
za wagombea, na kutangazwa matokeo. Kanuni zinazungumzia pia uhusika wa
mawakala katika hatua zote. Mawakala watapewa nakala za fomu mbalimbali
husika, zikiwemo zenye malalamiko yaliyowasilishwa, na matokeo.
Utaratibu huu wa sheria ndiyo unaotoa ulinzi mahususi wa kura.
Tume
(THBUB) inawataka mawakala wafanye kazi zao kwa uadilifu na weledi.
Mawakala wasiende kwenye vituo wakiwa na nia potofu (bad
faith/malafide) ya kuharibu zoezi la kupiga kura. Tume (THBUB) inalisema
hili kwa kuwa imebaini kuwepo matamshi yanayoonyesha hisia za
kutoiamini Tume ya Uchaguzi. Tume (THBUB) inasisitiza umuhimu wa
kuiamini na kuipa ushirikiano Tume ya Uchaguzi ili itekeleze majukumu
yake bila ya kuingiliwa ama kubezwa.
Kwa
hiyo Tume (THBUB) inapenda kutamka kwamba mlinzi mkuu wa kura ni wakala
wa chama cha siasa, mgombea, na siyo mpiga kura au mwananchi wa kawaida
ambaye hajapewa majukumu hayo kwa mujibu wa sheria.
Tume
(THBUB) inatahadharisha kuwa ni vyema kila mdau wa uchaguzi atimize
majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi. Jeshi la
Polisi liendelee kutumia weledi katika kutoa ulinzi siku ya uchaguzi,
kama lilivyofanya wakati wa kampeni za uchaguzi ambapo tulishuhudia
mikutano mikubwa ikimalizika kwa usalama.
Kwa
maana hiyo wananchi wanawajibu mkubwa wa kuwa watulivu wakati wa zoezi
zima la uchaguzi kuanzia kupiga kura na kusubiri matokeo kwa amani.
Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaamini kuwa utawala wa sheria
lazima uheshimiwe na kila mtu, vikiwemo vyombo vya dola na mamlaka za
Serikali.
Hivyo basi Tume (THBUB) inatamka:
1. Viongozi wa vyama vya siasa na wagombea waepuke lugha zinazoweza kusababisha hofu, vurugu na uvunjifu wa amani.
2. Inazishauri Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar, na Jeshi la Polisi
kuzingatia sheria na kudumisha misingi ya utawala bora, mambo ambayo
ndiyo msingi wa kulinda haki za binadamu.
3. Aidha, THBUB inawataka wananchi kupiga kura kwa amani na kuheshimu sheria zinazoongoza zoezi zima la uchaguzi.
4. Vyama
vya siasa vihakikishe kuwa Mawakala wao wanafanya kazi zao kwa uadilifu
na wahakikishe kuwa wanatambua wajibu wao na wanazingatia taratibu za
uchaguzi.
5. Jeshi
la Polisi litoe ulinzi mahsusi, bila vitisho, ili kuhakikisha kwamba
zoezi la kupiga kura linafanyika kwa amani na kwa kuzingatia haki za
binadamu na misingi ya utawala bora.
6. Viongozi
wa vyama vya siasa na wafuasi wao wawe wavumilivu na wajiepushe na
matamshi au matendo yanayo weza kusababisha uvunjifu wa sheria, haki za
binadamu, misingi ya utawala bora na kusababisha vurugu na kutoweka kwa
amani.
7. Tume
ya Uchaguzi na Wasimamizi wa uchaguzi, na mawakala wa vyama wahakikishe
kuwa zoezi zima la kupiga kura, kuhesabu kura, kubandika na kutangaza
matokeo linafanyika kama sheria inavyotamka.
Tume
ya Haki za Binadamu itaendelea kufanya ufuatiliaji wa mchakato wa
uchaguzi nchini kote ili kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na
misingi ya utawala bora.
Tume
inawataka wananchi watakaobaini uvunjifu wowote wa haki za binadamu, au
uvunjifu wa sheria ya uchaguzi, kuzijulisha mamlaka husika
zinazosimamia zoezi la uchaguzi.
Aidha,
wanaweza kutoa taarifa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kupitia
ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani (SMS) kwenda Na. 0754 460 259.
Ujumbe
lazima uanze na neno 'TAARIFA' au ' RIPOTI' kisha andika taarifa
yenyewe. Namba hii inapokea ujumbe mfupi tu. Kwa taarifa zaidi piga Na.
+255 22 2135747-8.
Kauli
mbiu ya THBUB katika kuelekea Uchaguzi Mkuu ni “Watanzania wote tufanye
Uchaguzi Mkuu kwa utulivu ili uwe Huru, wa Haki, na Amani.”
Imetolewa na:
(SIGNED)
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Oktoba 23, 2015
No comments:
Post a Comment