Matukio /Dini : Wanadiaspora Waadhimisha Idd Al -Adh'ha - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Friday, 25 September 2015

Matukio /Dini : Wanadiaspora Waadhimisha Idd Al -Adh'ha


Na Muwandishi wetu Swahilivilla Washington DC Waislamu kote ulimwenguni jana waliadhimisha Siku Kuu ya Idd Al-Adh'ha kwa Ibada na sherehe mbalimbali.Wanadiaspora wa Tanzania noa walijumuika na Waislamu wenzao ulimwenguni kuadhimisha siku hiyo muhimu katika Dini ya Kiislamu.
Baadhi ya waumini wa Tanzanian Muslim Community Washington DC wakipata picha ya pamoja baada ya kumaliza sala ya Eid Al-Adhw-haa iliosaliwa Siku ya Alhamis Sept 24, 2015 katika msikiti wa Islamic Center New Hampshire Maryland US.( Picha zote na swahilivilla.blogspot.com)
Katika kuadhimisha siku hiyo, Jumuiya ya Waislamu wa Tanzania waishio katika jiji la Washington na vitongoji vyake (TAMCO), iliandaa sherehe iliyoendelea hadi usiku katika viwanja vya wazi.
Akizungumza na Swahilivilla, mmoja wa wanachama wa jumuiya hiyo Bwana Abubakar Qullatein, aliiambia Swahilivilla kuwa amefurahi kuadhimisha siku hii adhimu katika dini ya Kiislamu. Hata hivyo furaha yake hiyo imeingiwa na dosari kutokana na maafa ya ajali zilizotokea huko Makka, Saudi Arabia zilizosababishwa na moto na mkanyagano wa watu.
Bwana Abubakar Qullatein, akipata picha ya 
pamoja na Abou Shatry baada ya swala ya Eid.
"Iddi hii imekumbwa na misukosuko kidogo kutokana na ajali za hapa na pale zilizotokea, sehemu mbalimbali duniani, na hata huko Makka", alielezea masikitiko Bwana Qullatein, na kendelea kusema kuwa, Iddi hii inakuja baada ya kukamilika kwa Ibada ya Hijja, kwa hivyo kwenye Hijja yenyewe kukitokea ajali kama hizi, inaleta huzuni.
Aliwatolea wito Waislamu kuondoa shari na fitna miongoni mwao na kuitetea Dini yao kwa kuonesha tabia na mtendo mema, jambo ambalo litasaidia kuondosha chuki kutoka kwa wasiokuwa Waislamu.
"Waislamu tushikamane, tupendane, tuondoe fitna na shari, tuwe kitu kimoja, tuoneshe tabia nzuri na mahusiano mema na watu wa dini nyengine, hii itasaidia kuondoa chuki zao" alihubiri Sheikh Qullatein, na kuelezea matumaini yake kuwa kuadhimisha Siku Kuu ya Idd Al-adh'ha siku moja kote ulimwenguni, kutakuwa ni mwanzo wa kuelekea kufunga na kufungua Ramadhani kwa pamoja.
Kwa upande wake, Mratibu wa sherehe za Siku Kuu wa TAMCO Bibi Asha Harris, aliiambia Swahillivilla kuwa, siku hii kama ilivyo adhimu kwa Waislamu kote ulimwenguni, pia ina umuhimu mkubwa kwa Jumuiya yake.
Bi Asha Hariz, kulia, akipata picha na  waumuni wa Tanzanian Muslim Community Washington DC, kwa chai ya asubuhi. "Siku hii ina umuhimu mkubwa kwa jumuiya yetu, kwa vile tunapata fursa ya kujumuika pamoja, na kuhuisha upendo na ushirikiano miongoni mwetu", alielezea Bi Hariss, na kuendelea kuwa ''Maadhimisho haya tunayagawa katika sehemu mbili; asubuhi na jioni"
Katika sehemu ya subuhi, Bi Harris ameelezea kuwa, mara tu baada ya Swala ya Iddi Wanajumuiya hukutana katika ukumbi maalum na kujipatia chai na vitafunio vyepesi. "Lakini kabla ya chai, kwanza huanza kwa Dua maalum ili kuwaombea wazee wetu na wenzetu wengine waliotangulia mbele ya Haki", alifafanua Bi Hariss.
Baada ya sehemu hiyo kumalizika, Wanajumuiya huondoka na baadaye kukutana tena jioni ili kuanza sehemu ya pili ya sherehe za Iddi Al-Adh'ha.
"Baadaye tunakutana tena jioni kwenye viwanja vya wazi kwa ajili ya nyama-choma na shamra-shamra nyengine" aliendelea kufafanua Bi Harris, na kusema kuwa sehemu hii ya pili ina umuhimu mkubwa zaidi, kwa vile huwajumuisha Watanzania wote hata wasiokuwa Waislamu.
Miongoni mwa vibwagizo vya sherehe hizo ni pamoja na michezo na mashindano ya watoto. Watoto hupata nafasi ya kupokea zawadi za aina mbalimbali, na kwa wale wanaoshinda kwenye mashindano yaliyoandaliwa hupata zawadi za nyongeza.
Mashindano ya watoto hujikita zaidi kwenye umuhimu wa Siku Kuu ya Idd Al-Adh'ha. "Tunafanya chemsha bongo kwa jili ya watoto, na maswali yote hujikita kwenye kuwahamasisha watoto juu ya umuhimu wa siku hii", alisema Bi Hariss.
Aliidokeza kuwa hapo awali, TAMCO ilikuwa inafanya sherehe za Idd wakati wa jioni tu, lakini katika miaka ya karibuni ikaonekana umuhimu wa kuwepo kwa sehemu ya asubuhi ambayo mbali na chai hujikita zaidi kwenye dua na maombi kama ilivyo ada nyumbani Tanzania.
Katika Jimbo la Washington, Watanzania nao hawakuwa nyuma katika kuadhimisha Siku Kuu ya Idd A-Adh'ha.
Bwana Adullah Kidume, alisema kuwa, Waislamu wa Tanzania waishio katika jiji la Seattle na vitongoji vyake walikodi ukumbi maalum kwa jili ya Swala ya Iddi.
Akizungumza na Swahilivilla kutoka Tacoma, Bwana Kidume alisema kuwa ni ada ya Waislamu katika maeneo hayo kukodi ukumbi kwa jili ya Ibada, na baadaye kuendelea na sherehe za kawaida.
Licha ya kutokuwa na Jumuiya rasmi, Waislamu wa Tanzania katika eneo hilo wameweza kudumisha ada ya kujumuika pamoja katika Siku Kuu mbalimbali za kidini. "Ni sisi wenyewe tu Waislamu tunaojuana...., siyo Kamati rasmi" alisema Bwana Kidume.
Hapo awali Waislamu hao walikuwa hukutana kwa ajili ya Swala tu, lakini, juhudi za akina mama ndizo zilizozaa wazo la kuendeleza sherehe hizo ambazo hudumu mpaka usiku wa manane.
Miongoni mwa vikorobwezo vya sherehe hizo ni pamoja na vyakula vya aina mbalimbali vinavyoonyesha ustadi wa mapishi ya Kitanzania, mavazi, michezo na mengineyo.
Licha ya Ibada ya Hija mwaka huu kukumbwa na maafa ya moto na watu kufariki dunia kutokana na mkanyagano huko Makka, hata hivyo, Hija hiyo imekuwa na umuhimu wa aina yake kwa baadhi ya Wazanzibari kwa vile ni mara ya mwanzo bendera ya Zanzibar imepepea katika Maeneo hayo Matakatifu.
Akiongea na mwandishi wetu kutoka Dar es Salaam, Bwana Omar Abdullah ameelezea furaha yake kuona bendera ya Zanzibar ikipepea katika Hija ya mwaka huu.
"Tulipopata taarifa za maafa kule Makka, Moyo wangu uliingiwa na huzuni.., japokuwa hakuna ndugu yangu, lakini Waislamu wote ni ndugu", alisema Bwana Abdullah, na kuongeza kuwa "lakini kitu kilicholeta furaha katika Siku Kuu hii kwangu, ni kuiona bendera ya Zanzibar ikipepea kule, japo kuwa kwa juu kulikuwa na kibendera kidogo cha Tanzania".
Alielezea matumaini yake kuwa katika Hija ya mwakani, Mahujaji kutoka Zanzibar watabeba bendera yao kamili bila kuwa na kibendera chengine ndani yake. Angalia Taswira mbali mbali za Eid Al- Adhw-haa Washington DC hapa

No comments:

Post a Comment