Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Chiku Gallawa akiwasilisha taarifa ya
maandalizi ya sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati zitakazo fanyika
sambamba na Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Kitaifa kuanzia Agosti
Mosi Mkoani Dodoma.
Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati zitafanyika sanjari na Maonesho na mashindano maalum ya mifugo ya 5 Kitaifa katika uwanja wa Nzuguni Dodoma kuanzia tarehe 01/08 hadi 08/08/2015.
Sherehe
za Nane Nane mwaka huu 2015 zinakwenda kwa Kaulimbiu inayosema “Matokeo
Makubwa sasa (BRN)– Tuchague viongozi bora kwa maendeleo ya Kilimo na
Ufugaji” Kaulimbiu hii imekuja wakati muafaka ambapo Taifa letu la
Tanzania linaelekea katika Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba na tayari baadhi
ya vyama vya siasa vimeshaanza mchakato wa kuendesha kura za maoni ili
kupata wagombea wa nafasi mbalimbali.
Kaulimbiu
hii inatoa msisitizo kwa wananchi na watanzania wote kuchagua viongozi
bora ambao watasaidia kuleta matokeo makubwa sasa katika nyanja za
Kilimo na Ufugaji kwa maendeleo ya nchi yetu kwa ujumla.
Kama
ilivyo ada, Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati sanjari na Maonesho na
mashindano maalum ya mifugo Kitaifa yanayofanyika kwenye viwanja vya
Nzuguni hapa Dodoma, yameendelea kuwa kitovu na chemchem ya elimu juu
ya:
- Zana bora za Kilimo na Mifugo
- Pembejeo za Kilimo na Mifugo
- huduma za Mawasiliano ya Kibiashara
- Usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo
- taasisi mbalimbali za Fedha na Mabenki
- Mafunzo na Utafiti na
- taasisi za uzalishaji za Serikali.
Hadi kufikia sasa maandalizi muhimu kwa ajili ya kufanikisha Sherehe hizi za Nane Nane yapo katika hatua nzuri.
Maendeleo ya Vipando na Mabanda ya Mifugo kwa ujumla yapo katika hatua nzuri ingawaje hatua iliyofikiwa inatofautiana kati ya taasisi na taasisi.
Miundombinu ya Barabara Inapitika
kirahisi, TASO kwa kushirikiana na Kamati ya Maandalizi ya Nane Nane
Kanda ya Kati inaendelea kufanya usafi wa barabara na kuhakikisha
zinakuwa katika hali nzuri wakati wote wa Maonesho.
Huduma ya Maji inategemea mtandao
wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dodoma (DUWASA) ambao ndiyo
unaotumiwa na wadau wengi na visima virefu (9) ambavyo vimechimbwa na
wadau kwa matumizi yao. TASO Kanda ya Kati inaendelea kushughulikia
changamoto ya kiufundi na kukatika kwa umeme kwa lengo la kuhakikisha
maji hayakosekani kwenye viwanja vya Nane Nane Nzuguni.
Arena ya Mifugo imefanyiwa
usafi na marekebisho madogo ili kuboresha mashindano maalum ya mifugo
ya 5 Kitaifa. Kwa upande wa Mabanda ya Maonesho, Napenda kutoa wito kwa
Wizara, Taasisi za Serikali, Taasisi zisizo za serikali , asasi na wadau
mbalimbali kuendelea kukamilisha ujenzi wa mabanda yao ya maonesho
kwenye viwanja vya Nzuguni ili kuleta ufanisi wa shughuli za Nane Nane.
Washindi wa Maonesho ya uwanjani:
(Wakulima na Wafugaji bora) Kutakuwa na Majaji wasiopungua wanne (4)
kutoka hapahapa Kanda ya Kati na baadae washindi wa Maonesho watapewa
zawadi kulingana na hali ya fedha, naomba nisitaje hapa lakini niweke
wazi kuwa Jukumu la kutoa zawadi ni la Kamati ya Maandalizi kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali.
Natumia
fursa hii kuwakaribisha wakulima na wafugaji kutoka mikoa ya kanda ya
kati na maeneo mengine ya Nchi, Wadau mbalimbali kuja kushiriki maonesho
haya ya Nane Nane na pia nawakaribisha wananchi hususani wakulima,
wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali kuja
kwa wingi kutembelea Maonesho ya Nane Nane na Maonesho na Mashindano
maalumu ya mifugo kwenye viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma kuanzia
tarehe 1-8 Agosti, 2015 ili waweze kujifunza.
Kwa
muhtasari matukio makuu kwa mujibu wa ratiba, katika siku ya ufunguzi
na Kufunga Msisitizo utakua Kaulimbiu ya Maonesho, Siku ya Pili ya
Maonesho Msisitizo utakua kuona Kiwango cha teknolojia ya Uzalishaji wa
bidhaa za kilimo , mifugo, maliasili na viwanda katika kukuza uchumi.
Siku
ya tatu ya Maonesho Msisitizo utakuwa Serikali za Mitaa kusimamia
maendeleo vijijini; Siku ya nne msisitizo utakua juu ya sera ya mikopo
kwa wakulima na wafugaji wadogo. Siku ya tano itahusisha Ufunguzi wa
Maonesho na mashindano Maalumu ya tano (5) ya mifugo. Siku ya sita ya
Maonesho msisitizo utakuwa kwenye umuhimu wa habari kwa maendeleo ya
kilimo na mifugo. Siku ya saba msisitizo utakuwa kwenye Hifadhi ya
Mazingira kwa kilimo na ufugaji endelevu.
Nawakaribisha
sana wananchi na wadau mbalimbali wa kilimo na mifugo hapa Dodoma na
Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye Maonesho ya Mwaka huu,
niweke mkazo kuwa ulinzi na usalama umewekwa vizuri ili kuhakikisha
Maonesho hayo yanafanyika salama kwa utulivu na amani.
Katika
hatua nyingine, kila Mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine
kuadhimisha ”Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani.” Maadhimisho
haya yaliyoanza mwaka 1992, hufanyika kuanzia tarehe 01 – 07/08 ya kila
mwaka.
Kwa
mwaka huu 2015, Mkoa wa Dodoma Makao Makuu ya Nchi, umepewa heshima ya
kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama kitaifa. Maadhimisho
haya yatakwenda sanjari na Sherehe za Nane Nane Kanda ya Kati na Maonesho na mashindano maalum ya mifugo ya 5 Kitaifa. Maadhimisho hayo
yatafanyika kuanzia Julai 1 - 7, 2015, ufunguzi utafanyika kwenye
wilaya ya Chamwino kwenye Kijiji cha Nkwenda, wakati sherehe za Kilele
cha Maadhimisho hayo Kitaifa zitafanyika hapa Manispaa ya Dodoma kwenye
viwanja vya Maonesho ya Nane Nane Nzuguni.
Kaulimbiu
ya Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama mwaka huu ni
”UNYONYESHAJI NA KAZI: TUHAKIKISHE INAWEZEKANA” (Breastfeeding and Work
Lets Make it Work). Kaulimbiu hii inalenga kuwasaidia wanawake WOTE
wanaofanya kazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi waweze kutunza watoto
wao ipasavyo pamoja na kufanya kazi mathalani kuajiriwa, kujiajiri, kazi
za muda mfupi au mikataba na kazi zisizo za kulipwa kwa mfano kazi za
mazingira ya nyumbani, shamba, mifugo na kutunza familia.
Katika
maadhimisho ya mwaka huu, pamoja na masuala mengine muhimu, kutakuwa na
utoaji wa elimu ya lishe kwa njia za vyombo vya habari, elimu ya lishe
kwenye vituo vya kutolea huduma na eneo la Nane Nane, elimu ya lishe na
unyonyeshaji kwa makundi ya wanafunzi, viongozi na Uhamasishaji kwa njia
ya gari la maonesho na semina.
Hivyo
natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma na Mikoa ya jirani
kuhudhuria ufunguzi na kilele cha maadhimisho haya ya Wiki ya
Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Kitaifa, halikadhalika, kutumia fursa hii
adhimu kupata elimu juu ya masuala ya Unyonyeshaji na lishe ili kusaidia
kumaliza tatizo la Utapiamlo baina ya wanawake walio katika umri wa
kuzaa (15 – 49 yrs) halikadhalika kuondoa tatizo la utapiamlo kwa watoto
wenye umri wa miezi 6 – 59.
Imetolewa na:
OFISI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA
Julai 30, 2015.
No comments:
Post a Comment