Mwandishi wa Habari wa Star Tv na Redio
Free Africa Mbeya, Fredy Bakalemwa amefariki dunia.
Mtandao huu umepokea kwa masikitiko
makubwa taarifa za kifo cha mwanatasnia
huyo wa Sahara Media Group na upo pamoja na wanahabari wote, familia yake na
marafiki zake katika kuomboleza kifo chake.
Bakalemwa ameondoka huku tasni ya habari
ikipita katika kipindi kigumu kinachohusisha juhudi, mbinu na njama za wazi za
kukwaza Uhuru wa kupata habari.
Kwa mfano, Sheria ya Takwimu ya mwaka
2014 yenye nia ya kurasimisha kila matokeo ya utafiti wa taasisi mbalimbali au
watu binafsi wakiwemo wasomi; itaathiri wepesi na haraka ya kukusanya taarifa
hivyo kuua maana ya habari kitaaluma.
Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka
2015 inanyima fursa adhimu ya uandishi wa habari za uchunguzi; hivyo kubaki na
fursa pekee ya kuchapisha taarifa na habari kwenye mitandao ya Intaneti.
Kwa mfano kashfa ya Vodacom ambayo ni
kubwa kuliko kashafa ya EPA na ESCROW imebakia kusomwa Jamii Forums pekee kwa
kuwa vyombo vingine vyote vya habari, ama vimekosa ujasiri au vimeathiriwa na
uhusiano wa kibiashara kati yake na kampuni hiyo.
Muswada wa Sheria ya Huduma kwa Vyombo
vya Habari unapokonya kazi za Baraza la Habari Tanzania (MCT): hivyo uhuru wa
waandishi wa habari kujiongoza na kujitawala unakuwa shakani; na sasa suala la
maadili linafanywa kuwa la kisheria badala ya usuluhishi.
Mwisho Muswada wa Haki ya Kupata Habari,
unaompa kila mwananchi haki ya kudai habari kutoka kwa mtoa habari wakiwemo
watawala umekwazwa na ukiritimba wa elimu na malipo; jambo ambalo litampa
wakati mgumu mwandishi mwenye sifa ya elimu chini ya digrii na mwananchi wa
kawaida kupata habari anayoitaka.
Bakalemwa umeondoka, lakini umeacha kundi
kubwa nyuma yako; tunaahidi kukuwakilisha vyema katika kudai haki na uhuru wa
kupata habari.
R.I.P BAKALEMWA.
No comments:
Post a Comment