Wilhelm Gidabuday |
Tayari wanafamilia wa michezo wanne, wametangaza
nia ya kuhakikisha wanachukua majimbo kwenye uchaguzi huo kupitia Chama
cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wanamichezo hao ni: Wilhelm Gidabuday (anagombea kupitia Chadema)
Huyu ana kumbukumbu nzuri katika tasnia ya michezo
hasa riadha kwani alikuwa mstari wa mbele kukosoa maandalizi waliyopewa
wanariadha wa Tanzania walioshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka
jana nchini Scotland.
Gidabuday amejitosa kuwania ubunge wa Jimbo la
Hanang kwa tiketi ya Chadema, jimbo linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Mary Nagu wa CCM.
“Kwa kuamini kwamba kugombea nafasi yoyote ni haki
ya msingi kikatiba, mimi kabla ya kujitathmini mwenyewe nimefanyiwa
tathmini na watu wa rika tofauti ndani ya jamii, makundi hayo
yakiwakilisha watu wenye busara katika jamii na kuniweka katika orodha
ya watu wenye sifa stahiki,” anasema Gidabuday.
Ataitetea michezo bungeni
“Wananchi wa Hanang pia wameridhishwa na harakati
zangu za kutetea wanamichezo, hususan riadha kitaifa, Watanzania wengi
wananifahamu kwa jina la (mwanaharakati wa michezo Tanzania). Harakati
zangu michezoni zimenifanya kuaminiwa na wadau wa michezo kote
Tanzania,” anasema Gidabuday.
“Sheria namba 12 ya Baraza la Michezo Tanzania
(BMT) ya mwaka 1967 licha ya kukosa meno, lakini pia imedharauliwa na
viongozi wa wizara, BMT wenyewe na taasisi zilizokusudiwa kusimamiwa na
sheria hiyo, na matokeo ya udhaifu huo umesababisha ufisadi ndani ya
vyama vya michezo, ndiyo maana Tanzania tumekuwa watalii katika viwanja
vya michezo kimataifa.
Ili kuondoa hali hiyo nitatoa hoja binafsi sheria
hii ibadilike sambamba na kuikumbusha Serikali umuhimu wa kuwa na
kijiji cha michezo,” anasema Gidabuday.
Mada Maugo (anagombea kupitia Chadema)
“Sijaingia kugombea ubunge kwa bahati mbaya, nimedhamiria
kuwatumikia wananchi wa Rorya ambao kwa kiasi kikubwa wameonyesha imani
na mimi,” anasema Maugo bondia namba tatu kwa ubora nchini kwenye uzani
wa super middle.
Ataendelea na ngumi?
“Ngumi siwezi kuacha hata kama nitapewa ridhaa ya
kuwa Mbunge wa Rorya, nitakachofanya ni kutenga muda wa kufanya mazoezi
na kupunguza idadi ya mapambano kwa mwaka na kutenga muda mwingi wa
kuwatumikia wananchi wa Rorya,” anasema Maugo.
Anasema kikubwa atakachokifanya bungeni ni
kuwapigania Wanarorya hasa katika huduma muhimu za kijamii kama afya,
barabara, maji na kunufaika na rasilimali walizonazo.
“Katika sekta ya michezo, hasa ngumi nitahakikisha
unakuwa na usimamizi mzuri ili kuwafanya mabondia wa Tanzania kupiga
hatua kimataifa kwani kuna madudu mengi yanafanywa na viongozi
wanaosimamia ngumi ambayo yanadidimiza mchezo huu na kuufanya
usisonge,”anasema Maugo.
Frederick Mwakalebela (Anagombea kupitia CCM)
Kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, Mwakalebela ambaye
hivi sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe amejitosa
tena kuwania ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwani mwaka 2010 alitoswa
kwenye kura za maoni ndani ya CCM hivyo kushindwa kugombea kiti hicho.
Jimbo hilo sasa lionaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.
Mwakalebela ambaye kabla ya kujiingiza katika
siasa, alipata kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
anasema atatumia muda mwingi kuwatumikia Wanairinga katika masuala
mbalimbali ya maendeleo ya jimbo lao endapo atapata ridhaa hiyo.
“Pamoja na kuwatumikia wananchi wa jimbo langu,
sitaipa kisogo michezo, nitahakikisha Iringa haibaki nyuma katika soka
la Tanzania na hata michezo mingine, sioni cha kutushinda katika hilo
kama nimeweza kuhamasisha vijana kushiriki mashindano mbalimbali ya
ndani, hakuna shaka kuwa tutapiga hatua pia kwenye michezo.
Innocent Melleck (Anagombea kupitia CCM)
Melleck anasema ameshawishika kuwania ubunge wa
Jimbo la Vunjo ambalo sasa Mbunge wake ni Agustino Mrema wa Chama cha
TLP, baada ya kushinikizwa kufanya hivyo na wazee wa jimbo hilo na
atagombea kupitia CCM. Anasema kama atapata ridhaa ya Wanavunjo kwenye uchaguzi mkuu
mwaka huu atatimiza ndoto yake ya siku nyingi ya kuwa mtetezi kwa
wananchi wa Vunjo, sambamba na kuipigania sekta ya michezo nchini ambayo
tayari ameanzisha mbio za Uhuru marathoni zinazolenga kutangaza amani
ya Tanzania na kuwasaidia wanariadha nchini.
Wanamichezo walioonyesha njia
Wakati wanamichezo hao wakitia juhudi kuingia
bungeni kwenye uchaguzi wa mwaka huu, tayari wapo wanamichezo bungeni
kama Juma Nkamia ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, pia ni Mbunge wa Kondoa Kusini ambaye amewahi kuwa Katibu
Mwenezi wa Simba.
Pia yupo Mohamed Dewji ambaye ni Mbunge wa Singida
Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye ni Waziri kivuli wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo na Mbunge wa Mbeya Mjini, yupo Ismail Aden Rage
aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu ya Simba ambaye sasa ni Mbunge wa
Tabora Mjini.CHANZO: Mwananchi
No comments:
Post a Comment