Mkurugenzi
Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Cosmas Mwaisobwa (kulia)
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majuku ya Bodi kwa Naibu Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela leo (Jumatano,
Aprili 22, 2015) jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alifanya ziara ya
kikazi katika Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa Bodi.
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela (wa pili
kulia) akimsikiliza Meneja Upangaji Mikopo wa Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bi. Emma Sabaya (kushoto) leo
(Jumatano, Aprili 22, 2015) jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alifanya
ziara ya kikazi katika Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa Bodi.
Mkurugenzi
wa Mipango, Utafiti na TEHAMA wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu
ya Juu (HESLB) Bw. Asangye Bangu (mwenye tai ya njano) akimweleza Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela (kulia)
jinsi kumbukumbu za waombaji wa mikopo zinavyohifadhiwa katika Bodi
hiyo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Aprili 22, 2015). Naibu Waziri
alifanya ziara ya kikazi katika Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa
Bodi.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) Bw. Hamisi Chagonja akimkabidhi zawadi Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela jijini Dar es Salaam leo
(Jumatano, Aprili 22, 2015). Naibu Waziri alifanya ziara ya kikazi
katika Bodi hiyo na kukutana na uongozi wa Bodi.Picha na HESLB.
Na Mwandishi Wetu
Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Anne Kilango Malecela
ameilekeza Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuongeza
kasi ya utoaji elimu kwa wadaiwa wake na umma kwa ujumla ili kuongeza
makusanyo ya marejesho na hatimaye kuwa na mfuko endelevu wa mikopo ya
wanafunzi.
Akizungumza
na uongozi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Aprili 22,
2015), Naibu Waziri Malecela amesema wadaiwa wa Bodi hiyo wakielewa
umuhimu wa kulipa mikopo yao, kasi ya ulipaji itaongezeka.
“Ongezeni
juhudi zaidi na hasa tengenezeni matangazo ya televisheni yanayotoa
elimu ili kuwakumbusha wadaiwa na wananchi kwa ujumla juu umuhimu wa
kulipa,” amesema Naibu Waziri wakati wa ziara yake ya kikazi katika
ofisi za Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Maelekezo
ya Naibu Waziri yalifuatia taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi
iliyowasilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa
HESLB Bw. Cosmas Mwaisobwa ambaye alitaja changamoto mbalimbali
zinazoikabli HESLB ikiwemo wakopaji wengi na waajiri kutokutoa
ushirikiano kwa Bodi katika urejeshwaji mikopo.
“Wakopaji
wengi ambao mikopo yao inapaswa kuanza kurejeshwa hawatoi ushirikiano
wa kutosha kwa Bodi katika kurejesha mikopo yao, na hili linachangiwa
pia na kutokuwepo kwa Vitambulisho vya Kitaifa ambavyo vingerahisisha
ugunduzi wa wapi walipo wadaiwa hao,” amesema Mwaisobwa katika kikao na
Naibu Waziri.
Mwaisobwa
alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na mtazamo potofu kuwa fedha
zinazotolewa na Bodi hiyo ni ruzuku badala ya mikopo na kuongezeka kwa
idadi ya waombaji mikopo wakiwemo hata wale ambao wazazi wao wana uwezo
wa kuwagharamia.
Kwa
mujibu wa Mwaisobwa, changamoto nyingine ni pamoja na baadhi ya wazazi,
walezi na waajiri na wafadhili wenye uwezo kujitoa katika kugharamia
wanafunzi wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu kwa kutegemea mikopo
inayotolewa na Bodi.
Pamoja
na changamoto hizo, Mwaisobwa, kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi
alimweleza Naibu Waziri Malecela kuwa katika mwaka wa masomo 2014/2015,
kati ya waombaji wa mikopo 39,411 wa mwaka wa kwanza waliofanyiwa
tathmini ya uwezo wa kiuchumi, wanafunzi 33,595 walipangiwa mikopo.
Kati
ya hao, amesema Mwaisobwa, wanafunzi 31,238 ni wa shahada ya kwanza
katika vyuo vya ndani, 2,117 ni wa wanafunzi wa Diploma ya Ualimu katika
fani ya sayansi na hisabati na wengine 160 ni wa mwaka wa kwanza
wanaosoma nje ya nchi. Wanafunzi 80 ni wa shahada ya Umahiri na Uzamivu
katika vyuo vya ndani ya nchi.
Mikopo
hiyo hutolewa ili kugharamia maeneo sita ambayo ni chakula na malazi;
mafunzo kwa vitendo; vitabu na viandikwa; fedha za utafiti; ada ya
mafunzo; na mahitaji maalumu ya kitivo
HESLB
ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi
mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa
wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu. Aidha,
jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa
wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali
ilipoanza kukopesha wanafunzi.
Kwa
mujibu wa Mwaisobwa, jumla ya wanafunzi 291,582 wamenufaika na mikopo ya
elimu ya juu inayotolewa na Serikali kati ya mwaka 1994 na Juni mwaka
jana (2014). Jumla ya kiasi cha fedha kilichokopeshwa hadi kufikia mwaka
jana (Juni, 2014) ni Tshs 1.8 trilioni ambapo Tshs 51.1 bilioni
zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu Juu, Sayansi na Teknolojia na
Tshs 1.75 trilioni zimetolewa na HESLB tangu ilipoanza kazi rasmi Julai
2005
No comments:
Post a Comment