Mkurugenzi
wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es
Salaam wakati akitoa taarifa ya kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei nchini kwa
mwezi Februari, 2015. Kulia kwake ni Kaimu Meneja wa Takwimu za Ajira
na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja.
Baadhi
ya Waandishi wa Habari wakiwa kazini wakati Mkurugenzi wa Sensa na
Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu
akizungumza nao leo jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya kuongezeka
kwa Mfumuko wa Bei nchini kwa mwezi Februari, 2015. (PICHA ZOTE NA
VERONICA KAZIMOTO).
Na Veronica Kazimoto,
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Februari, 2015 umeongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka asilimia 4.0 mwezi Januari mwaka 2015.
Hayo
yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim
Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo amesema kuwa
kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi
Februari, 2015 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa
mwaka ulioishia mwezi Januari, 2015.
“Kuongezeka
kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 kumechangiwa na kuongezeka
kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa
kipindi kilichoishia mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za
mwezi Februari, 2014, amesema Kwesigabo”.
Bidhaa
za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi Februari, 2015
zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014 ni pamoja na bei za
mchele (asilimia 18.5), unga wa mihogo (asilimia 9.3), nyama (asilimia
8.9), samaki (asilimia 12.4) na maharagwe kwa asilimia 7.1.
Kwa
upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi
Februari, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014 ni pamoja
na bei za mavazi ya wanaume (asilimia 4.7), mavazi ya wanawake (asilimia
3.3), mkaa (asilimia 5.1), mashuka (asilimia 3.1) na gharama za kumuona
daktari kwa asilimia 11.2.
Akizungumzia
kuhusu Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwezi Mkurugenzi Kwesigabo amesema
kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 unaopimwa kwa kipimo cha
mwezi umeongezeka kwa asilimia 1.6 ukilinganisha na ongezeko la asilimia
1.0 mwezi Januari, 2015.
Aidha,
Kwesigabo amesisitiza kuwa Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi kufikia
154.83 mwezi Februari, 2015 kutoka 152.43 mwezi Januari, 2015 ambapo
kuongezeka kwa fahirisi kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za
vyakula na bidhaa zisizo za vyakula.
Kwa
upande wa thamani ya shilingi, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii
Epraim Kwesigabo amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika
kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 64 na senti 59 mwezi
Februari, 2015 kutoka mwezi Septemba, 2010 ikilinganishwa na Shilingi 65
na senti 60 ilivyokuwa mwezi Januari, 2015.
Hata
hivyo, Mfumuko wa Bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi
ya nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi
Februari, 2015 nchini Uganda umeongezeka hadi asilimia 1.4 kutoka
asilimia 1.3 mwezi Januari, 2015; na nchini Kenya, Mfumuko wa Bei wa
Mwezi Februari, 2015 umeongezeka hadi asilimia 5.61 kutoka asilimia 5.53
mwezi Januari, 2015.
No comments:
Post a Comment