Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga (wa kwanza kulia),
akizungumza na viongozi wa ujumbe wa Serikali ya Sudan Kusini
waliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es salaam jana.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga, akizungumza
katika kikao cha mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya
ujenzi wa miundombinu ya barabara na viongozi wa Sudan Kusini. (wa pili
kushoto) ni Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi Eng. Venny
Ndaymukama, anayemfuatia ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Barabara za
Mkoa Eng. Laurent Kyombo.
Naibu
Waziri wa Usafirishaji, Barabara na Madaraja wa Sudan Kusini Mh. Simon
Mijok, akitoa salamu za Serikali yake kwa viongozi wa Wizara ya ujenzi,
kutokana na ziara ya mafunzo ya siku tatu inayoendelea hapa nchini.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) Dr. James Wanyancha, akimkabidhi
zawadi Naibu Waziri wa Usafirishaji, Barabara na Madaraja wa Sudan
Kusini Mhe. Simon Mijok alipotembelea ofisi za Mfuko wa Barabara kwa
ajili ya mafunzo ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya ujenzi wa
miundombinu ya barabara jijini Dar es salaam.
Ujumbe
wa Sudan Kusini katika picha ya pamoja na viongozi wa Bodi ya Mfuko wa
Barabara (RFB) walipoitembelea Bodi hiyo jana kujifunza inavyofanyakazi.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga amezungumzia
umuhimu wa Tanzania kuimarisha uhusiano wake na Sudani Kusini na kueleza
kuwa hatua hiyo itawezesha nchi hiyo kuwa na amani na kupiga hatua za
haraka za maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza
mara baada ya kupokea ujumbe wa Serikali ya Sudan Kusini ulioitembelea
Wizara ya Ujenzi kujifunza namna bora ya kuendesha Wizara
inayoshughulikia usafirishaji,ujenzi wa barabara na madaraja Eng.
Nyamhanga amesema kuwepo na mipango endelevu,wataalam wa ndani na
uhusiano mwema baina ya nchi na nchi ni kigezo muhimu cha kuleta
maendeleo katika sekta ya miundombinu.
“Tumieni
uzoefu wa Tanzania kuanzisha taasisi zinazosimamia sekta ya ujenzi na
usafirishaji na kuongeza idadi ya wahandisi na makandarasi ili kujenga
miundombinu mipya na kuiendeleza iliyokwishajengwa”, amesisitiza Eng.
Nyamhanga.
Amezungumzia
umuhimu wa Serikali ya Sudan Kusini kuwa na mfuko wa ukarabati na
ujenzi wa barabara,kuwa na taasisi zinazosimamia makandarasi,wahandisi
na wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi ili kuimarisha sekta ya
ujenzi nchini humo.
Akitoa
mada kuhusu hatua za haraka za kuchukua ili kufikia malengo ya
maendeleo Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Barabara za Mikoa Eng. Laurent
Kyombo, amesema Sudan Kusini itapata maendeleo ya haraka kama
itaimarisha taasisi zinazohusika na sekta ya ujenzi na kujifunza kwa
nchi jirani ambazo zimepiga hatua kubwa katika ujenzi wa barabara katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza
kwa niaba ya ujumbe huo Naibu Waziri wa Usafirishaji,Barabara na
Madaraja wa Sudan Kusini Mhe. Simon Mijok, ameishukuru Tanzania kwa
jitihada zake kwa nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo diplomasia
na ujenzi huku akisisitiza kwamba watatumia ziara yao ya mafunzo
kuanzisha taasisi za ujenzi zenye sura ya Tanzania ili kuharakisha
maendeleo ya nchi hiyo.
“Tangu
enzi za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania imekuwa kimbilio
la raia wa Sudan Kusini na baadhi yao wamepata elimu hapa nchini ,
hivyo naiomba Tanzania iendelee kuilea nchi yetu changa iliyopata uhuru
wake hivi karibuni baada ya mapambano ya muda mrefu ya kudai uhuru”,
amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Nchini (RFB), Dkt. James
Wanyancha ameueleza ujumbe huo umuhimu wa kuwa na mfuko maalum wa
barabara utakaowezesha kuendeleza na kukarabati barabara zilizojengwa
ili zitumike wakati wote.
“Hakikisheni
fedha zitakazotengwa kwaajili ya miradi ya ujenzi wa barabara na
madaraja zinatumika kwa kazi hizo; hii itasaidia barabara zilizojengwa
kufanyiwa ukarabati na kuziendeleza ziwiane na mahitaji ya eneo husika”,
amesisitiza Dkt. Wanyancha.
Ziara
hiyo ya mafunzo ya siku tatu ambayo imedhaminiwa na Shirika la Maendeleo
la Japan (JICA)upande wa Sudan Kusini na Tanzania, inajumuisha ujumbe
wa viongozi 15 waandamizi wakiwemo wa Wizara ya Usafirishaji,Barabara na
Madaraja, Wizara ya Mazingira na Wajumbe wa Bodi wa Mamlaka ya Barabara
ya Sudan Kusini (SSRA).
Ukiwa
hapa nchini, ujumbe huo utapata fursa ya kutembelea taasisi mbalimbali
zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na kuona zinavyofanya kazi ya
utekelezaji wa miradi ya ujenzi hapa nchini.
Pia
utatembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo-Msata,Ruvu chini na
kituo cha mizani cha Vigwaza wilayani Bagamoyo mkoani pwani.
No comments:
Post a Comment