Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama |
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt Jakaya Kikwete leo anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya
siku mbili mkoani Kilimanjaro ambapo miongoni mwa shughuli
anazotazamiwa kufanya ni pamoja na
kufungua jengo la kitega uchumi la
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF).
Mbali na ufunguzi huo Rais Kikwete pia
anatarajia kufungua jengo la Upasuaji na kuweka jiwe la msingi
katika jengo la wodi ya wazazi na watoto katika hosptali ya rufaa ya
mkoa wa Kilimanjaro ,Mawenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake ,mkuu wa mkoa huo Leonidas Gama alisema Rais Kikwete
atawasili mkoani humo leo jioni
majira ya saa 11:00 jioni ambapo
atapokelewa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na
kuelekea Ikulu ndogo kwa ajili ya kupokea taarifa ya Mkoa.
Alisema Kesho (February 10) Rais
Kikiwete atafanya shughuli katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ikiwemo
ufunguzi wa jengo la Upasuaji (Theater) ambalo limekuwa tatizo la
muda mrefu katika hosptali hiyo.
“Kwanza kama mnavyo fahamu tumekuwa na
tatizo la muda mrefu ya wodi ya upasuaji katika hospitali yetu ya
Mawenzi,lakini kwa juhudi zilizofanywa na serikali na ushirikiano wa wadau
mbalimbali lile jengo
la Upasuaji limekamilika na liko
katika kiwango kizuri kwa hiyo shughuli ya kwanza atakuja kulifungua
rasmi jengo la upasuaji.”alisema Gama.
RAS-Seviline Kahitwa (shoto) RC Gama (Kulia) |
Gama alisema pia Serikali tayari
imefanya juhudi za kujenga jengo jipya la Wodi kwa ajili ya Wazazi na
Watoto katika hosptali hiyo na kwamba Rais Kikwete ataweka rasmi jiwe
la msingi kwa ajili ya muendelezo wa ujenzi wa jengo
hilo.
Alisema kwa mujibu wa ratiba shughuli
ya mwisho anayotazamia kufanya Rais Kikwete ni ufunguzi rasmi wa
jengo la kitega Uchumi la NSSF,jengo
ambalo litatumika kufanya shughuli
mbalimbali za kiuchumi .
“Ufunguzi rasmi wa jengo hili
utabadilisha taswira ya mji wetu,ni jengo la kisasa lenye Hotel,Maofisi
mbalimbali,Kumbi za mikutano na maduka mbalimbali makubwa kwa madogo
ambayo yatahudumia wananchi wote”alisema Gama.
Gama alitoa wito kwa viongozi na
wananchi wote wa mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi
wa jengo hilo la NSSF majira ya saa 2:00 asubuhi ambapo rais Kikwete
pia atapata nafasi ya kuzungumza na wananchi.
“Lengo la Rais Kikwete kuja ni
kutuunga mkono sisi wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika miradi yetu ya
maendeleo hivyo basi tufike mapema katika maeneo hayo ili tumsubiri na
tumuone rais na kumshangilia”alisema Gama.
Hili ndio jengo jipya la kisasa la kitega Uchumi la Mfuko wa Hifadhi ya Jami NSSF mkoani Kilimanjaro. Na Dixon Busagaga |
No comments:
Post a Comment