Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Maria Bilia akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wadadisi 200 wa Sensa ya Viwanda itayofanyika nchi nzima mwezi huu. Mafunzo hayo yanafanyika chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kilichopo eneo la Changanyikeni jijini Dar es salaam.
Mkuu wa chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kilichopo eneo la Changanyikeni jijini Dar es salaam Prof.Ngalinda Innocent akizungumza na wadadisi watakaokusanya takwimu za Sensa ya Viwanda mwezi huu wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku 14.
Mkuu wa chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Prof. Ngalinda Innocent akizungumza jambo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bi. Maria Bilia (katikati) na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makzi Bi. Hajjat Amina Mrsiho Said leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza na wadadisi 200 watakaokusanya takwimu za viwanda wakati wa Sensa ya Viwanda itakayofanyika nchini nzima mwezi huu leo eneo la Chuo cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wadadisi wa Sensa ya Viwanda wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kukusanya takwimu sahihi wakati wa Sensa ya Viwanda leo jijini Dar es salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirikisho la wenye Viwanda nchini Bw.Hussein Kamote akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi 200 watakaokusanya takwimu wakati wa Sensa ya viwanda itakayofanyika nchini mwezi huu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Maria Bilia akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya NBS na wadadisi wa Sensa ya Viwanda Picha na Aron Msigwa - MAELEZO
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
SERIKALI imewataka wamiliki wa viwanda kuwapa ushirikiano wadadisi wa Sensa ya Viwanda watakaopita katika maeneo yao kwa lengo la kukusanya takwimu sahihi za viwanda vilivyopo nchini na mchango vinaotoa katika maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Maria Bilia wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku 14 ya wadadisi wa Sensa ya Viwanda yanayoendelea katika chuo cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika kilichopo eneo la Changanyikeni jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa mafanikio ya Sensa hiyo yatatokana na wamiliki wa viwanda kuthamini na kutambua umuhimu za Sensa hiyo kwa kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaopita katika maeneo yao kupata taarifa zinazohusu masuala mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa bidhaa na masuala ya ajira;
Amesema upatikanaji wa takwimu sahihi kuhusu Sekta ya Viwanda nchini Tanzania utaiwezesha Serikali kuweka Sera na mipango endelevu ya maendeleo itakayoisaidia sekta hiyo kupiga hatua kimaendeleo.
“Sensa hii ya viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, na mafanikio yake yatatokana na wenye viwanda kutupa ushirikiano maana bila wao kutoa takwimu sahihi mipango ya maendeleo kuhusu viwanda haitatekelezeka kwa sababu ya kukosa takwimu sahihi” Amesema Bilia.
Kuhusu sampuli ya viwanda vitakayoguswa na Sensa hiyo amesema ni pamoja na maeneo ya viwanda yaliyoajiri watu wengi na yanayohusisha uzalishaji mkubwa wa bidhaa za viwandani ,maeneo ya uzalishaji wa bidhaa za kokoto, bidhaa za vyakula na maeneo yaliyoajiri mtu zaidi ya mmoja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa Sensa hiyo ya viwanda itakayohusisha viwanda vyote nchini inafanywa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Amesema kukamilika kwa Sensa hiyo kutaliwezesha taifa kuwa na takwimu sahihi za viwanda na kutambua mchango wa Sekta ya viwanda katika uchumi wa taifa na mchango wa ajira kwa wananchi.
Kuhusu mafunzo hayo ya siku 14 kwa wadadisi 200 watakaoendesha zoezi hilo amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupitia Chuo cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika inaendesha mafunzo hayo kwa vitendo na nadharia ili kuwawezesha na kuwajengea uwezo wadadisi hao kukusanya takwimu bora.
“Lengo la kuendesha Sensa hii ni kuhakikisha kuwa nchi yetu inapiga hatua na kuwa nchi yenye maendeleo ya kati kwa kuwa na matumizi sahihi ya takwimu zetu”
Kaimu Mkurugenzi wa Shirikisho la wenye Viwanda nchini Bw.Hussein Kamote akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya wamiliki wa Viwanda nchini amesema kuwa Sensa ya viwanda itakayofanyika nchini mwezi huu italiwezesha taifa kuwa na takwimu sahihi zinazohusu sekta ya viwanda.
“Sensa hii ya viwanda ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa nawaomba wenye viwanda watoe ushirikiano wa kutosha maana bila wao zoezi hili litakuwa gumu”
Ameongeza kuwa Sensa ya viwanda ni muhimu kutokana na mchango wake katika nchi nyingi za Asia ambazo zimefanikiwa na kupiga hatua kimaendeleo kwa sababu ya kuwa Sensa endelevu na takwimu sahihi za sekta ya viwanda na mchango wake katika pato la taifa.
No comments:
Post a Comment