Muziki : Rais Dkt Samia amkumbuka nguli Zahir Zorro - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Tuesday, 10 March 2026

Muziki : Rais Dkt Samia amkumbuka nguli Zahir Zorro



Na Mashaka Mhando


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtumia salamu za faraja na mkono wa heri nguli wa muziki wa dansi nchini, Mzee Zahir Ally Zorro, ambaye kwa sasa anakabiliwa na changamoto za kiafya.

Salamu hizo za Rais zimefikishwa nyumbani kwa mwanamuziki huyo Kisota, Kigamboni Jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA). Katika ziara hiyo, Mhe. Mwinjuma alipokelewa na Mzee Zahir Zorro pamoja na mwanawe, mwanamuziki nyota wa R&B, Banana Zorro.

Akizungumza kwa niaba ya Rais, Mhe. Mwinjuma alisema kuwa Mkuu wa Nchi ameguswa na hali ya Mzee Zorro na ametambua mchango wake usiofutika katika utamaduni na sanaa ya Tanzania.

"Nimetumwa na Mheshimiwa Rais kuja kukujulia hali na kukushika mkono. Rais anajua mchango wako na ameelekeza nikukabidhi kiasi hiki cha Shilingi Milioni 10 kusaidia taratibu zako za matibabu na mahitaji mengine," alisema Mhe. Mwinjuma.

Kwa upande wake, mwanamuziki Banana Zorro, aliishukuru serikali kwa niaba ya familia kwa kumkumbuka baba yao katika kipindi hiki ambacho pia familia bado inakabiliwa na majonzi ya kuondokewa na binti yao, Maunda Zorro miaka kadhaa iliyopita.

Mzee Zahir Zorro, ambaye ni mmoja wa magwiji wa mwisho wa kizazi cha dhahabu cha muziki wa Dansi nchini, alitoa shukrani za dhati kwa Rais Samia, akibainisha kuwa upendo huo unampa nguvu na matumaini ya kurejea katika hali yake ya kawaida.

Ziara hiyo imetafsiriwa na wadau wa sanaa kama ishara ya utu na utambuzi wa dhati wa mchango wa wasanii wakongwe walioasisi sanaa ya kisasa nchini.






No comments:

Post a Comment