Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga akifungua rasmi semina
kuhusu matumizi ya gesi asilia iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli
ya Serena jijini Dar es Salaam.
Balozi
wa Japan Tanzania, Masaki Okada akizungumza na wadau na wataalamu wa
gesi asilia (hawapo pichani) waliohudhuria semina ya matumizi ya gesi
asilia iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Serena ya jijini Dar
es Salaam.
Wataalamu
na wadau wa gesi asilia kutoka Japan na Tanzania wakimsikiliza Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga (hayupo pichani) wakati wa
ufunguzi wa semina ya matumizi ya gesi asilia iliyofanyika hivi
karibuni katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Kamishna
Msaidizi Nishati (Gesi), Mhandisi Norbert Kahyoza (wa kwanza kulia)
akifuatilia uwasilishaji wa mada kwenye semina iliyohusu matumizi ya
gesi asilia iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Serena, Dar es
Salaam.
Na Mohamed Saif
Wizara
ya Nishati na Madini imeishukuru Serikali ya Japan kupitia Shirika la
Kimataifa la Maendeleo ya Japan (JICA) kwa ushirikiano wake katika
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo nchini na kuahidi
kuuendeleza ushirikiano huo.
Shukrani
hizo zilitolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Charles Kitwanga kwa Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada wakati
akifungua semina kuhusu matumizi ya gesi asilia iliyoandaliwa na JICA
kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini na kuhudhuriwa na wadau
na wataalamu wa masuala ya gesi kutoka nchini Japan na Tanzania.
Naibu
Waziri Kitwanga alieleza kuwa Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na wa
muda mrefu na Watu wa Japan na Serikali yao. Aidha, alibainisha kuwa
uhusiano huo ulianza tangu mwaka mwaka 1966 na akisisitiza kuuenzi na
kuuendeleza uhusiano uliopo.
Akizungumzia
umuhimu wa semina hiyo, Kitwanga alisema ni wakati muafaka kwa
wataalamu wa Tanzania kuwa na uelewa mpana zaidi kwenye masuala
mbalimbali yanayohusu gesi asilia na mafuta kwa manufaa ya taifa.
“Semina
hii ni fursa nzuri kwa wadau na wataalamu wetu wa masuala ya gesi kwa
kuwa imelenga kuainisha matumizi mbalimbali ya gesi asilia. Ni imani
yangu kupitia wadau na wataalamu mliohudhuria semina hii, Watanzania
wataelewa namna gani watafaidika na gesi asilia. Tuitumie semina hii
vizuri kwa ajili ya kuliletea maendeleo taifa letu,” alisema Kitwanga.
Alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanafaidika na rasilimali
ya gesi asilia kutokana na fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa
gesi asilia nchini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali katika
kampuni zinazojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi.
Aidha,
Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada alimuhakikishia Naibu Waziri
Kitwanga kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Serikali ya
Tanzania katika miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Balozi
Okada alisisitiza umuhimu wa Tanzania kujipanga vizuri katika
kuhakikisha gesi asilia inaleta maendeleo makubwa ya kiuchumi ikiwa ni
pamoja na kuwatumia wataalamu kutoka Japan.
“Semina
hii itahusisha mada mbalimbali ambazo zitatolewa na wataalamu
waliobobea katika masuala ya gesi asilia, ni matumaini yangu wadau na
wataalamu mbalimbali mtanufaika na mada ambazo wataalamu hawa kutoka
Japan wameandaa,” alisema Balozi Okada.
No comments:
Post a Comment