Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva
akizunguza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya tume ya
uchaguzi jijini Dar es salaam wakati alipozungumzia maandalizi ya
uboreshaji wa daftari la wapiga kura, kura ya maoni ya Katiba mpya na
uchaguzi mkuu mwezi oktoba mwaka huu, kulia ni Mkurugenzi wa Tume ya
Uchaguzi Bw. Julius Mh.Julius Mallaba.
Baadhi ya waadishi wa habari wakiwa katika kutano huo.
.................................................................................................................
Ndugu Waandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Watendaji wa Tume, Mabibi na Mabwana.
Kwa
niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, napenda kuchukua fursa hii
kuwakaribisheni kwa mara nyingine katika Mkutano huu. Nawashukuru
kwamba, pamoja na majukumu mengi mliyo nayo, mmeweza kuupa umuhimu wa
pekee mkutano wetu huu na kuhudhuria kwa wingi. Kwa niaba ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, nasema Ahsanteni na Karibuni sana.
Katika
mkutano huu, Tume inalenga kutoa taarifa kuhusu tathmini ya utekelezaji
wa zoezi la majaribio ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
(Pilot Registration) kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR)
zoezi ambalo lilikamilika wiki iliyopita.
Ndugu
Wanahabari, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imepewa jukumu la kisheria
Kuandikisha Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na
kuliboresha Daftari hilo kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani. Kwa mujibu wa Sheria ya Kura
ya Maoni, Daftari hili la Kudumu pia litatumika katika Kura ya Maoni
kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Ndugu
Wanahabari; mtakumbuka kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa katika
mchakato wa Maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
kwa kutumia Teknolojia Mpya ya ”Biometric Voter Registration” (BVR) na
mara kwa mara imekuwa ikiomba kukutana nanyi ili kuwapa taarifa kuhusu
hatua mbalimbali ambazo Tume imekuwa ikizipitia.
Kwa
kuwa Uboreshaji huu ulihusisha matumizi ya vifaa vya teknolojia ya
kisasa, vifaa ambavyo vilikuwa havijawahi kutumika katika Uboreshaji
nchini, tuliona si vyema kuagiza vifaa vingi kabla ya kuvifanyia
majaribio. Zoezi la majaribio lilifanyika ili kuwa na uhakika kuwa vifaa
hivi vya Biometric Registration vina uwezo wa kuandikisha Wapiga Kura
katika mazingira ya nchi yetu.
Zoezi
hili liliangalia uwezo wa watendaji kutumia BVR katika uandikishaji na
pia uwezo wa vyombo vyenyewe katika Software na Hardware kwenye
uandikishaji. Katika zoezi hili tuliangalia changamoto zilizojitokeza
ili kuzipatia ufumbuzi kabla ya kuanza Zoezi halisi la Uandikishaji wa
nchi nzima.
Ndugu
Wanahabari, Kama nilivyosema, Tume inakutana nanyi ili kuwapa taarifa
kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa zoezi la Majaribio la Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kwa siku saba (7) katika
Kata za Bunju na Mbweni katika Jimbo la Kawe, Manispaa ya Kinondoni
jijini Dar es salaam; Kata za Ifakara, Kakingiuka, Ipangala, Mlabani na
Viwanja Sitini katika Jimbo la Kilombero Halmashauri ya Wilaya ya
Kilombero, mkoani Morogoro; na Kata za Ikuba, Usevya na Kibaoni katika
Jimbo la Katavi, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Tume
kwa namna ya pekee, inawashukuru sana Waandishi wa Habari kwa kujitokeza
na kufuatilia zoezi hili la majaribio ya uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura. Waandishi wa Habari wamesaidia sana katika
kuhamasisha Wananchi wa Majimbo husika kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Vilevile,
Waandishi wa Habari wamesidia katika kutoa taarifa za maendeleo ya zoezi
hili kitu ambacho kimesaidia kufanikisha zoezi hili.
Jumla
ya BVR Kits 250 zilitumika katika Uboreshaji huo kwa mgawanyo ufuatao:-
Halmashauri ya Kilombero BVR Kits 80, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele BVR
Kits 80 na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni BVR Kits 90. Vituo
katika Kata zote vilikuwa vinafunguliwa saa 2.00 asubuhi na kufungwa saa
12.00 jioni.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Tume inapenda kuwafahamisha kuwa zoezi hilo la
Majaribio ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika
majimbo matatu yaliyotajwa limefanyika na kukamilika kwa mafanikio
makubwa. Changamoto zilizojitokeza hapa na pale zimetusaidia kupata
ufumbuzi ambao utatusaidia wakati wa Uandikishaji wenyewe nchi nzima.
Tunasema mafanikio makubwa kwa sababu matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa
idadi ya wapiga kura waliojitokeza kujiandikisha ilikuwa kubwa na kuvuka
malengo ya waliokadiriwa kuandikishwa.
Mkoa
wa Dar es salaam, Kata za Bunju Wapiga Kura 15,123 waliandikishwa kati
ya 27,148 na Kata ya Mbweni Wapiga Kura 6,200 waliandikishwa kati ya
8,278. Takwimu hizi za waliondikishwa inatokana na makisio ya watu
tuliyokuwa tumejiwekea kutokana na matokeo ya sensa mwaka 2012. Mkoa wa
Morogoro Kata za Ifakara, Kakingiuka, Ipangala, Mlabani na Viwanja
Sitini Wapiga Kura walioandikishwa ni 19,188 wakati makisio yalikuwa
watu 17,790 na Mkoa wa Katavi Halmashauri ya Mlele kata za Ikuba, Usevya
na Kibaoni Wapiga Kura 11,210 waliandikishwa wakati makisio yalikuwa
watu 11,394. Matokeo haya yanadhihirisha kuwa vifaa vya uandikishaji
vilifanya kazi vizuri na hivyo vinaweza kutumika katika Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa nchi nzima.
Pamoja
na mafanikio hayo, kama ilivyo kawaida katika majaribio yoyote kwani
ndiyo lengo la kufanya majaribio, zilikuwepo changamoto kadhaa wakati wa
utekelezaji wa zoezi hilo. Changamoto hizo zinaweza kuwekwa katika
makundi makubwa matano kama ifuatavyo:- i. Matatizo yaliyotokana na
’Settings’ za BVR Kits; • Baadhi ya ”BVR Kits” zilitumia camera iliyo
katika Laptop badala ya camera iliyowekwa kwa ajili ya kupiga picha. •
Uchukuaji wa alama za vidole (Automatic Process settings) ilisababisha
Mfumo kusimama (Crash). • Tatizo la kuchukua picha iwapo viwango vya
ICAO vya ubora wa Picha havijafikiwa kama •
Unrecognise
face, • Unrecognise eye, • Stretch photo, • Un even light. • Uwepo wa
Majina yenye ”apostrophe”. ii. Matatizo yaliyosababishwa na Software; •
Fingeprint Scanner kusababisha Mfumo wa Uandikishaji kusimama (Crash)
kutokana na SDK na za vifaa finger print scanner. • Kuharibika kwa
baadhi ya file (File Corruption) kutokana na d11 ya finger print
scanner. iii.
Matatizo
ya hardware; • Komputa (Laptop) Kupata Joto kutokana na Bati liliwekwa
kuzuia kuibiwa Laptop kwa urahisi ambapo mahitaji kuwezesha mzunguko wa
hewa ndani ya ”BVR Kit”. • FlashDrive ya pili (Drive G) kutoonekana
hivyo kuhitaji kubadilishwa na kuwa SD card. • Uharaka wa uchukuaji
alama za vidole ambapo ilibidi kufanya mabadiliko. iv. Matatizo ya
lojistiki na matatizo ya Watendaji wa zoezi la Uandikishaji. • ”BVR Kit”
kuchelewa kufikishwa katika Vituo. • Vurugu wakati wa uandikishaji
ambao unahitaji Ulinzi kuwepo. •
Baadhi
ya ”BVR Operator” kutokuwa na uwezo au kuwa makini katika utumiaji wa
”BVR Kits” hivyo kuhitaji elimu zaidi kwa ”BVR Kit Operator”. • ”BVR Kit
Operator” kubadili Kits kwa tatizo dogo linaloweza kutatulika kwa
urahisi. • ”BVR Kit Operators” kutokuwa na uelewa wa matumizi ya ”Solar
Panel” kwani baadhi ziliwekwa chini ya mti au kutogeuzwa kadri muda
ulivyokuwa unakwenda.
Mbali
ya changamoto hizo zilikuwepo pia changamoto nyingine za kimiundombinu
na kibinadamu. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na Hali ya Hewa
hususan katika jiji la Dar es salaam na Morogoro. Mtakubaliana nami kuwa
pamoja na kuwa jiji la Dar es salaam kwa kawaida lina hali ya hewa ya
joto lakini kwa takribani mwezi mmoja hivi uliopita kumekuwa na ongezeko
la joto hali iliyosababisha hata baadhi ya vifaa vya kuandikishia
hususan ’BVR Kits’ wakati mwingine kushindwa kufanya kazi inavyotakiwa
na hivyo kusababisha shughuli za uchapishaji wa Kadi za Kupigia Kura
kuchelewa.
Aidha,
ushirikiano mdogo kutoka kwa Wananchi nao ulikuwa changamoto
iliyosababisha zoezi hilo kwenda taratibu. Baadhi ya wananchi kushindwa
kuzingatia maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na BVR Kit Operators kutokana
na uelewa duni kwani ilibainika pia kuwa bado kuna idadi kubwa ya
wasiojua Kusoma na Kuandika. Hali hiyo ilifanya zoezi la Uchukuaji wa
alama za Vidole (Fingerprint) na Utiaji wa Saini kuwa mgumu.
Kadhalika
kumekuwepo na mwamko mkubwa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili
kujiandikisha. Hivyo, kulikuwepo na watu wengi sana katika vituo vya
Uboreshaji wa Daftari hilo la Kudumu la Wapiga Kura. Changamoto zote
zilizojitokeza kuhusiana na settings tuliweza kwa ushirikiano na
watengenezaji wa vifaa hivyo, kuzipatia suluhisho wakati zoezi
linaendelea. Pia chanagamoto za ’software’ nazo zimekwishapatiwa
suluhisho.
Changamoto
kuhusu hardware zitarekebishwa wakati wa utengenezaji wa BVR Kits 7,750
ambazo zilikuwa hazijaanza kutengenezwa kusubiri matokeo ya zoezi hili
la majaribio.Marekebisho hayo ya hardware pia yatafanywa katika
BVR Kits 250 zilizoletwa kwa ajili ya majaribio. Changamoto kuhusu fedha
na lojistiki zinaendelea kushughulikiwa kwa ushirikiano na Serikali.
Kuhusu changamoto za Watendaji tunaendelea kuzishughulikia kwa
kuhakikisha Watendaji tutakaowatumia wanakuwa na utaalam unaotakiwa
kuziendesha BVR Kits hizo.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Napenda pia niongelee baadhi ya masuala yanayohusu
zoezi la Uboreshaji wa Majaribio kwa ujumla. Kwanza ni vyema ieleweke
wazi kuwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kwa ajili ya Kura
ya Maoni ya Katiba Mpya, Mpiga Kura atatumia Kitambulisho cha Mpiga Kura
alichopatiwa na Tume baada ya kuandikishwa katika mfumo huu tu na si
vinginevyo. Vitambulisho vilivyotolewa katika uboreshaji huu wa
majaribio ni vitambulisho halisi hivyo kila aliyejiandikisha katika
zoezi hili la majaribio ni muhimu atunze kadi yake kwa ajili ya matumizi
yaliyotajwa kwa kuwa taarifa zake tayari zimeingia katika Kanzi data ya
Tume hivyo hataweza tena kujiandikisha kwa mara nyingine hata kama
atabadilisha kituo cha kujiandikishia.
Ndugu
Wanahabari, Pili, ni muhimu wananchi wakapata taarifa hizi kwa usahihi
kwa vile wapo baadhi ya Watu wanaodhani kuwa kwa kuwa hilo lilikuwa ni
zoezi la majaribio basi watakuwa na fursa nyingine ya kujiandikisha
wakati wa zoezi la nchi nzima. Napenda nisisitize hapa kuwa kwa yeyote
aliyejiandikisha katika zoezi hili, hatatakiwa tena kujiandikisha labda
tu kwa yule ambaye atahitaji kubadilisha taarifa zake kutokana na sababu
kama zilivyofafanuliwa na Tume.
Ndugu
Wanahabari. Napenda nisisitize pia kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayo
dhamira ya dhati ya kukuza demokrasia kwa kuandaa na kuendesha chaguzi
zake katika mazingira rafiki na wazi yatakayotoa fursa kwa kila raia wa
Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 kutumia haki yake ya kikatiba ya
kuchagua viongozi wake. Tume itakuwa tayari kupokea maoni na ushauri
kutoka kwa wadau mbalimbali wa Uchaguzi kuhusu namna bora ya kufanikisha
majukumu yake. Aidha, Tume itaendelea kubuni mbinu na mikakati
itakayoboresha utendaji kazi wake.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa
kumalizia, ninapenda tena kuwashukuru wote kwa kuhudhuria Mkutano huu.
Tume mara zote imekuwa ikitambua mchango wa Vyombo vya Habari katika
kufikisha ujumbe kwa jamii inayokusudiwa. Hali kadhalika, katika zoezi
hili la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia BVR
vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kuufahamisha umma wa
watanzania na kuhamasisha wale wote wenye sifa kujitokeza na
kujiandikisha. Tume inatambua na kuthamini mchango wenu huo.
Kwa
mantiki hiyo, na kwa mara nyingine natoa rai kwenu na Wadau wengine wa
Uchaguzi kutoa taarifa zilizo sahihi na kuhamasisha Wananchi kushiriki
katika zoezi hilo kubwa linalotarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Ni mategemeo ya Tume kuwa kwa kupitia kalamu na vipaza sauti vyenu
taarifa hizi zitawafikia Wapiga Kura wetu na hatimaye wataweza
kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha pindi muda huo utakapowadia.
Ndugu Wanahabari,
Nimalizie
pale nilikoanzia, kwamba uandikishaji wa majaribio katika baadhi ya
Kata za Majimbo matatu ya Kawe, Kilombero na Katavi umefanikiwa kwa
kiwango kikubwa licha ya changamoto zilizojitokeza. Kutokana na
changamoto hizo, vifaa vya BVR vitakavyo tumika katika zoezi la
Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini kote vitafanyiwa
marekebisho stahili kwa vile 7,750 ambavyo bado havijafika nchini,
pamoja na vile 250 vilivyotumika katika zoezi la majaribio.
Hivyo,
hapana shaka kwamba, kama mambo yote yataendelea kama ilivyopangwa hadi
sasa, mpango wa kuendesha Kura ya Maoni mwishoni mwa Aprili 2015, na
Uchaguzi Mkuu October, 2015 kwa kutumia Dafti lililoboreshwa na vifaa
vya BVR uko pale pale. Kama kawaida, ili kufanikisha ratiba hiyo,
ushirikiano wa kila Mdau -Vyama vya Siasa, Vyama visivyo vya Kiserikali
NGO’s, CSO’s, Serikali, Wananchi wote, Wapiga Kura na Wafadhili wote,
Tume inaomba uendelee kwa kiwango cha juu. Hili likifanyika, Tume
inaamini kuwa zoezi la Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu Octoba, 2015
utafanikiwa kwa amani na utulivu. Hayati Mwalimu J. K. Nyerere alisema,
Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mwisho
kabisa lakini muhimu sana, kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
naomba kwa msisitizo kwamba zoezi likianza, wanachi nchini kote
wajitokeze kwa wingi kujiandikisha. Hii itawawezesha kwanza kupiga Kura
ya Maoni na baadaye katika Uchaguzi Mkuu, Octoba, 2015. Kukosa kufanya
hivyo ni kujinyima HAKI YAKO YA KIKATIBA YA KUCHAGUA VIONGOZI MNAOWATAKA
No comments:
Post a Comment