Wakizungumza na gazeti hili wasomi nchini wamesema mabadiliko ya wakuu
hao huwa na sababu nyingi, lakini sababu ambayo haielezwi huwa ni ile ya
kisiasa.
Katika mabadiliko hayo Rais Kikwete alimpandisha cheo Mkuu wa Wilaya ya
Karatu, Daudi Ntibenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kuwahamisha vituo
vya kazi wakuu wengine sita wa mikoa kuanzia juzi. Ntibenda aliapishwa
jana Ikulu na Rais Kikwete.
Uhamisho huo umekuja ikiwa ni mwezi mmoja kamili tangu Rais Kikwete
alipofanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa mikoa na kuwahamisha sita,
huku wengine watatu wakipangiwa kazi nyingine.
Wakuu wa mikoa wanne wapya ni Dk Ibrahim Msengi (Katavi), Amina Masenza
(Iringa), Halima Dendego (Mtwara) na John Mongella (Kagera).
Akizungumza na gazeti hili Dk Slaa alisema, “Mabadiliko haya ni
viashiria vya Serikali kuchoka na kutokuwa na uhakika kama itabakia
madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu 2015. Ndiyo maana wanawahamisha ili
kuona nani atafaa wapi na kwa malengo gani.”
Alisema kumhamisha mkuu wa mkoa ndani ya mwezi mmoja ni gharama zisizo
na msingi, “Hizi gharama zote za nini? Hivi hawazioni, iweje katika
kipindi hiki kifupi wafanye mabadiliko haya?
“Katika kipindi hiki ambacho nchi inahitaji fedha kwa ajili ya shughuli
nyingi za maendeleo, yanapofanyika mabadiliko kama haya lazima ujiulize
kipaumbele cha Serikali ni nini,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala
alisema: “Binafsi naona mabadiliko haya yanalenga uchaguzi mkuu maana
kila unapokaribia huwa yanafanyika.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Dk Alexander Makulilo alisema: “Suala la gharama haliepukiki. Sababu za
kuhamisha wakuu wa mikoa ni nyingi ila kubwa ni changamoto za mkoa
husika au kupwaya katika utendaji.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema mabadiliko
hayo ni ya kawaida na yametokana na kupewa likizo ya ugonjwa kwa
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti ambaye nafasi yake
imechukuliwa na Elaston Mbwilo aliyetoka Manyara.
“Kunapokuwa na tatizo kama hilo ni lazima Rais ateue watu wengine. Rais
anapoteua anatazama hata changamoto za mkoa husika na uteuzi unazingatia
zaidi utendaji si masuala ya kisiasa. Baadaye utafanyika uteuzi wa
wakuu wa wilaya,” alisema.
Katika uteuzi huo wa juzi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera
anahamia Manyara kutoka Morogoro na nafasi yake inachukuliwa na Dk
Rajabu Rutengwe kutoka Tanga alikokaa kwa mwezi mmoja akitokea Katavi.
Magalula Magalula amehamishiwa Tanga kutoka Lindi ambako naye alikaa kwa
mwezi mmoja akitokea Geita na nafasi yake inazibwa na Mwantumu Mahiza
kutoka Pwani. Mhandisi Evarist Ndiliko amehamishiwa Mkoa wa Pwani kutoka
Arusha alikohamia hivi karibuni akitokea Mwanza. Walioachwa kwa ajili
ya kazi nyingine ni Dk Christine Ishengoma (Iringa), Kanali Fabian
Massawe (Kagera) na Kanali Joseph Simbakalia.
.aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ambaye tayari ameteuliwa kuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo
ya Nje (EPZA).
Akizungumza Ikulu jana mara baada ya kuapishwa, Ntibenda alisema,
“Siendi Arusha kupambana na vurugu, ninakwenda kusimamia masuala ya
maendeleo.”
Alisema changamoto zinazoukabili mkoa huo ni migogoro ya ardhi na
kusisitiza kuwa ataitatua migogoro hiyo kwa kushirikiana na wananchi
pamoja na wakuu wa mikoa.
Chanzo :Mwaananchi
No comments:
Post a Comment