Raha ya kipindi tunachoishi sasa ni wepesi wa mawasiliano.
Mawasiliano ya haraka kwa simu za mkononi, habari kusambaa, mitandao
kutupasha yaliyotokea, ghafla bin vuu.
Hakuna linalofanyika hadharani likapita, vuum,
siku hizi. Iwe umbea au udaku; serikali, mazuri au kashfa, gharika au
tufani; ili mradi...Buum! Hiyo hapo machoni.
Hata mambo ya binafsi ambayo miaka 25 iliyopita
yaliwekwa uvunguni. Ya mtoto kuzaliwa, mtu kuonyesha chakula alichokila,
wanawake kutangaza madoido na urembo wao wa kucheza na kukata viuno,
nk. Tunaishi msimu wa majigambo ya nafsi. Kutaka kuonekana, kusifiwa
kujinadi hadharani; kwa uzuri au ubaya. Kila mtu ajue.
Kiingereza kina neno lake maalumu la kifalsafa.
“Narcissism”....lenye asili Uigiriki. Enzi
Wagiriki wakitawala maendeleo (kama Marekani leo) Narcissus, kijana wa
kiume aliyekuwa na haiba maridadi, alijienzi kiasi ambacho siku moja
Nemesis mwanamke wa kuvutia, akamghilibu ajitazame katika dimbwi la
maji. Narcissus alivyokuwa na huo upendo wa wajihi wake alikaa pale
akijifurahia alivyokuwa mrembo. Kumbe ule wasifu aliouona majini ulikuwa
picha tu. Njozi.
Sasa Narcissus akawa anapotelea ndani ya hiyo
njozi ya wajihi wake, akijifurahia hadi alipojisahau na kuanguka
dimbwini. Akafa. Ndiyo maana ipo nahau ya Kiingereza isemayo “he met his
nemesis” au “she met her nemesis”...yaani, mtu unakutana na Ibilisi au
jambo linalokuweza na kukuangamiza. Nemesis alimtega na kuchangia
kuaangamia kwa Narcissus si kwa ubaya ila kutokana na kujipenda kuzidi
kawaida.
Mantiki ya kisa inatufundisha nini kuhusu lugha, maisha na maudhui?
Tuko ndani ya mazingira ya kupenda umaarufu na
kujitangazia lolote tunalolifanya na kulishirikisha kwa yeyote yule.
Ndani ya mazingira yetu mna hulka ile ya methali ya Kiswahili, “ Hapana
siri ya watu wawili...”
Raha imo, ndiyo. Kufichua mabaya. Polisi weupe wa
Kimarekani sasa hivi wanakosolewa kutokana na vitendo vyao vya kuua watu
weusi waliovunja sheria mitaani bila kuwafikisha mahamakani. Siyo
kwamba ni mambo mapya.
Toka enzi magenge ya weupe yakiwavizia watu weusi
na kuwanyonga hadharani kwa kosa dogo la kutongoza msichana wa Kizungu.
Yalitendeka. Tofauti? Leo huwekwa hadharani kutokana na vifaa kama simu
za mkononi na video zilizozagaa barabarani majuu (CCTV).
Raha ya mablogu ndiyo hiyo.
Ufidhuli na ufisadi wa viongozi wapotofu
unachojolewa soksi, sidiria na kofia. Kama ilivyotokea vuguvugu za
Mashariki ya Kati (Arab Spring): Tunisia, Libya, Misri na kuishia
viongozi waliowatesa wananchi kutolewa madarakani. Kifo katili cha
Kanali Muammar Gadaffi mwaka 2011 mathalan, kiliwekwa wazi. Uanahabari
wa kijamii kilingeni.
Mabloga ni wanahabari huria
Hapa kwetu Tanzania mwanahabari wa TV, Daudi Mwangosi alipouawa
kinyama mwaka 2012, picha ya viungo vyake vya ndani (utumbo na
kadhalika) ziliwekwa wazi wazi mitandaoni. Sasa hivi ukibofya tu Daudi
Mwangosi, vimeselelea mitandaoni.
Wanablogu walikuwa watu wa kwanza kuonyesha
ukatili wa askari walioyateketeza maisha ya Mwangosi akiwa kazini na
kuiacha familia yake ikilia mayowe hadi mtondogoo.
Mabloga ni wanahabari huria
“Houria” ni uhuru kwa Kiarabu. Uhuria huu
uliochipuka mwaka 1990 baada ya kuanguka himaya ya Ukomunisti na
kubomolewa ukuta uliotenganisha Ujerumani ya Mashariki na Magharibi,
mjini Berlin.
Mengi yaliyofuatia hapo yameweka utamaduni wetu
sasa. Kufunguliwa Nelson Mandela toka jela baada ya miaka 26. Akaanzisha
serikali mpya iliyo ahueni na kiini cha safari za Waafrika wengi
kushuka Afrika Kusini.
Wagonjwa wetu kwenda kutibiwa, ushirikiano wa
kibiashara, runinga na vipindi vya TV, nk. Pia kuanzishwa kwa vyama
mbalimbali vya kisiasa barani Afrika. Uhuria huu ulituathiri pia katika
starehe; tuna muziki wa kizazi kipya ...muziki wa Bongo Fleva. Umejenga
ajira kwa vijana wanaojituma, kutegemea muziki.
Kinyume na miaka 35 iliyopita siku hizi tunao
wanamuziki matajiri kuliko enzi za marehemu Patrick Balisidja, Mbaraka
Mwinshehe, Kiko Kids na Marijani Rajab. Tuna vyama vya upinzani na
wanasiasa chipukizi mathalan Zitto Kabwe na January Makamba.
Enzi za Tanu kiongozi kijana alikuwa Chediel
Mgonja aliyeingia baraza la mawaziri akiwa na umri mdogo wa miaka 31-33.
Haikuwa kawaida na siyo wengi wanamjua Mgonja aliyekuwa Waziri wa Elimu
kadhalika. Alipofariki mwaka 2009, mmoja wa watoa maoni ndani ya blog
la Michuzi alisifia:
“Nakumbuka Mgonja alipokuja kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara na magwanda yake ya JKT ya mwanzo kabisa yalikuwa ya kadeti
(mwandishi ana maana mwanafunzi wa kijeshi). Alikuwa kijana machachari
na alikuwa anapendwa na Nyerere. Hata mimi nilimpenda wakati huo niko
shule ya msingi.”
Mtoa maoni mwingine anadai, “hawa wazee walikuwa
very humble” ( wanyenyekevu), na serikali ya sasa ya Tanzania wajiulize
kwa nini viongozi wa sasa hawafuati mfano wa hawa wazee.”
Blogu ni sehemu zenye maoni na malumbano mengi.
Pia, mabloga mashuhuri kama Michuzi huruhusu kiasi fulani cha maoni ya
wananchi ambayo mengine huwa ovyo mengine mazuri mengine makali. Ndiyo
hulka ya uhuru wa kimawazo tuliyo nayo sasa.
Tatizo hata hivyo ni kiwango na mipaka. Kutokana
na haraka ya kuwahi kutoa habari, wanabloga wengi hawafuati kanuni za
uanahabari.
Bloga Mubelwa Bandio (Jicho la Ndani), Mtanzania mkazi wa
Marekani aliwakumbusha mabloga wenzake kuzingatia maadili ya kutangaza
habari:
“Siku za karibuni kumekuwa na matukio mengi mabaya
na ya kutisha nchini Tanzania; mengine yamehusisha matendo ya kikatili
kwa wanajamii. Licha ya shukrani za dhati kwa wanablogu kuweka wazi
matendo haya bado narejesha ombi la kuzingatia maadili katika kuweka
picha na maelezo. Ninaloomba ni kuzingatia utu hata wa marehemu na
kuzingatia heshima ya marehemu na nduguze. Kumekuwa pia na shida ya
kuweka majina na hata picha za watoto wenye umri chini ya miaka 18.”
Ombi hili la mmoja wa wanabloga wenyewe
linaonyesha namna tatizo la uhuru wa kuandika na kutoa maoni ulivyofikia
kilele chake. Hata baada ya Bandio kuweka hoja, bado kuna bloga
alitundika picha ya maiti ya dereva wa polisi aliyefariki na mtoto mdogo
wa miaka minne. Mabloga na wanahabari huria zingatieni maadili na utu.
Huu siyo mchezo wa kitoto, changarawe na gololi!
No comments:
Post a Comment