*Ni Toleo Maalum la Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania
*Linatumika kuitangaza Tanzania kwa watu mashuhuri
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua jarida la kimataifa la FIRST ambalo
limesheheni taarifa za kuitangaza Tanzania kwa wadau wa nchi mbalimbali
duniani huku likielezea hatua mbalimbali za ustawi kwa miaka 50 tangu
nchi ipate uhuru.
Uzindusi huo ulifanyika kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania jijini
London, Uingereza ambako pia Waziri Mkuu alikabidhiwa nakala ya kwanza
ya toleo la sasa ambayo iliwekwa kwenye jalada jekundu la ngozi (leather
bound red cover).
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema Serikali ya
Tanzania imepata fursa nzuri ya kujinadi kwa watu maarufu na
wafanyabiashara wa kimataifa duniani kupitia jarida hilo na akataka
uwekwe utaratibu wa kujinadi kisekta.
Alimtaka Balozi wa Uingereza, Bw. Peter Kallaghe aweke mkazo na
kusimamia suala hilo ili kuhakikisha matoleo yanayofuata yanakuwa ya
kisekta zaidi. “Balozi hapa umefanya kazi nzuri sana ya kuinadi nchi
yetu, wala usichoke. Tujitahidi sasa kila mwaka waandike kuhusu fursa za
uwekezaji kwa miradi ya kisekta kama utalii, nishati, madini na
kadhalika,” alisema.
Waziri Mkuu alimshukuru Mwenyekiti wa taasisi ya First, Bw. Rupert
Goodman kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa ajili ya Taifa la Tanzania. “Kazi
uliyoifanya ni nzuri lakini katika tolea lijalo tuangalie jinsi ya
kuitangaza miradi ya uwekezaji ambayo inauzika na iende sekta kwa sekta.
Ukisirikiana na Balozo wetu hapa, lazima utapata kitu kizuri,” alisema.
Mapema, akielezea kuhusu jarida hilo la FIRST, Balozi Kallaghe alisema
jarida hilo linasambazwa kwenye mashirika mbalimbali ya ndege kama vile
British Airways, Air Astana, Lufthansa, United Airlines, Gulf Air,
American Airlines, South African Airways, Korean Airways, Etihad
Airways, Qatar Airways na Continental Airlines.
“Siyo tu kwamba linasambazwa katika mashirika haya ya ndege, bali pia
linawekwa kwenye vyumba vya kupumzikia (First Class and Business Class
Lounges) abiria wa daraja la kwanza na la pili wa mashirika haya kwenye
viwanja vingi vya ndege,” alisema.
Alisema hili ni toleo la sita ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano na
ofisi yake (Ubalozi wa Uingereza) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya
Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania lakini pia ikilenga kutangaza fursa za
uwekezaji lakini pia ikitangaza hatua mbalimbali za maendeleo ambazo
nchi hii imepitia.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu
Nchemba; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw.
Mahadhi Maalim na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Charles
Kitwanga. Wengine ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba na
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu ambao pia wamefuatana na
Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, OKTOBA 23, 2014
No comments:
Post a Comment