Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akifungua mafunzo ya siku
27 kwa wakufunzi na wadadisi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
watakaoendesha Utafiti wa Tathmini ya utoaji wa Huduma za Afya nchini
2014/15 mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza na
washiriki wa mafunzo ya Utafiti wa Tathmini ya utoaji wa Huduma za Afya
nchini, mkoani Kilimanjaro.
Mkufunzi
wa mafunzo ya wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Tathmini ya Utoaji
wa Huduma za Afya nchini Bi. Saumu Said akiendelea kutoa mafunzo kwa
washiriki wa utafiti huo mkoani Kilimanjaro.
Washiriki
wa mafunzo ya Wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Tathmini ya Utoaji
wa Huduma za Afya nchini wakiendelea na mafunzo yatakayowawezesha
kufanya utafiti huo mkoani Kilimanjaro.
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akisalimiana na wakufunzi
na wadadisi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watakaoendesha Utafiti wa
Tathmini ya utoaji wa Huduma za Afya nchini 2014/15 walio kwenye mafunzo ,mkoani Kilimanjaro.
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akiwa katika picha ya
pamoja na wakufunzi na wadadisi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
watakaoendesha Utafiti wa Tathmini ya utoaji wa Huduma za Afya nchini
2014/15 mkoani Kilimanjaro.
SERIKALI
imewataka wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa
huduma za Afya nchini mwaka 2014/15 kuzingatia weledi katika utekelezaji
wa majukumu yao na kuepuka kukusanya takwimu zisizo wakati wa utafiti
huo utakaofanyika nchi nzima kuanzia Oktoba 13 mwaka huu.
Aidha,
imewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, madakatari na wafanyakazi wa
vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kutoa ushirikiano kwa
wadadisi watakaoendesha utafiti huo ili waweze kufika kwenye vituo vya
kutolea huduma za afya vilivyopo katika maeneo yao kwa lengo la kupata
taarifa sahihi zitakazofanikisha utafiti huo muhimu kwa maendeleo ya
taifa.
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid akizungumza wakati
akifungua mafunzo ya siku 27 kwa wakufunzi na wadadisi kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar watakaoendesha utafiti huo amesema kuwa wakufunzi,
wadadisi na wataalam hao wanayo nafasi kubwa ya kufanikisha upatikanaji
wa takwimu sahihi zitakazotoa taswira halisi ya utoaji wa huduma ya
afya nchini kwa mwaka 2014/2015.
Amesema
utafiti huo utaiwezesha serikali kutathmini utekelezaji wa mipango
mbalimbali na kufikia malengo iliyojiwekea kitaifa na kimataifa kwa
kuboresha na kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake.
Amesema
Serikali imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za kuboresha huduma za
afya na maisha ya Watanzania kwa kupitia Mikakati ya Kimataifa na
Kitaifa ikiwemo ile ya Malengo ya Milenia ya Mwaka 2015 na Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano (2011 -2016).
Amezitaja
programu nyingine kuwa ni pamoja ile ya Dira ya Maendeleo ya Mwaka
2025, Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA) na Mkakati wa Kupunguza Umaskini
Zanzibar (MKUZA) kwa upande wa Zanzibar.
Dkt.
Seif amesema katika juhudi hizo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
imekuwa na jukumu la kusimamia programu mbalimbali za afya na kufuatilia
utekelezaji na utoaji wa huduma za afya nchini.
Ameeleza
kuwa wakati wa utafiti wa kwanza wa Kutathmini Utoaji wa Huduma za Afya
nchini unafanyika na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2006,Tanzania
ilikuwa na jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 5669, kati ya
hivyo 224 zilikuwa ni hospitali, 541 vikiwa ni vituo vya afya na
zahanati 4904.
Amesema
kumekuwa na maboresho makubwa katika sekta ya afya hadi kufikia mwaka
2013 ambapo takwimu zinaonyesha kuwepo kwa vituo 6767 vya kutolea
huduma ya afya nchini , hospitali 256, vituo vya afya 701 na zahanati
5810.
“Nyote
ni mashahidi kuwa toka kipindi hicho mpaka sasa serikali imeendelea
kusogeza huduma za afya karibu na wananchi wake,sasa tuna huduma ya
kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambayo
inapatikana katika vituo vyote vinavyotoa huduma za mama mjamzito”
Amesisitiza.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina
Chuwa akizungumzia mafunzo hayo amesema kuwa washiriki watakaofaulu na
kukidhi vigezo vilivyowekwa watashiriki katika zoezi la kukusanya
takwimu za utafiti huo kwa kipindi cha miezi minne kuanzia tarehe 13
Oktoba 2014 .
Amesema
utekelezaji wa utafiti huo na mafunzo hayo unafanywa kwa pamoja na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii -
Tanzania Bara, Wizara Afya - Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Shirika la ICF International la
Marekani ambao pia wanatoa ushauri wa kitaalamu katika kufanikisha
utafiti huo.
Dkt.
Chuwa amefafanua kuwa utafiti huo utahusisha ukusanyaji wa takwimu
katika sehemu za kutolea huduma za afya kwa lengo la kufahamu utayari
wa vituo vinavyotoa huduma za afya na huduma bora za afya kwa wananchi.
Aidha
amezitaja huduma zitakazoguswa na utafiti huo kuwa ni pamoja pamoja na
Huduma za Afya ya Uzazi, Afya ya Watoto, Maradhi ya Kuambukiza kama vile
Kifua Kikuu, UKIMWI, Malaria pamoja na Maradhi yasiyo ya kuambukiza
kama vile magonjwa ya Kisukari na Moyo.
Amefafanua
kuwa lengo la kufanyika kwa utafiti huo ni kuiwezesha serikali kujua ni
kwa namna gani vituo vinavyotoa huduma ya afya vimejipanga kutoa huduma
bora ya afya kwa kuangalia upatikanaji wa huduma mbalimbali, vifaa,
dawa, miundombinu na rasilimali watu kwa kada mbalimbali.
Kuhusu
utafiti huo Dkt. Chuwa amesema ni wa pili kwa ngazi ya kitaifa
ukifuatiwa na ule wa kwanza uliofanyika mwaka 2006 na kuongeza kuwa
utahusisha sampuli wakilishi ya vituo vya kutolea huduma vya serikali
,binafsi, mashirika ya umma na vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini
ambavyo vimetayarishwa, hospitali maalum zote, hospitali zote za mikoa ,
wilaya na baadhi ya vituo vya afya na zahanati.
Naye
mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Ibrahimu Msengi
akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa mkoa huo
unaendelea na juhudi za kuboresha huduma za afya zinazotolewa katika
vituo vya afya pamoja kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya wakazi
wa Kilimanjaro na kukuza pato la mkoa huo.
Amesema
mkoa umeweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya afya iliyopo
ili iweze kuakisi ukuaji wa Pato la Mkoa na mahitaji ya wananchi katika
kupata huduma za afya zilizo bora kulingana na ongezeko la idadi ya
Watu.
Amefafanua
kuwa utafiti huo umekuja wakati muafaka ambapo mkoa huo na mikoa
mingine nchini inahitaji kuboresha huduma za afya katika vituo vyote vya
kutolea huduma.
No comments:
Post a Comment