Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeonyesha dhamira ya dhati Kufanya kazi bega kwa bega na wadau wa maendeleo kuhakikisha uboreshaji wa mfumo wa usimamizi wa mafunzo endelevu wa walimu kazini yaani MEWAKA unaboreshwa na kukamilika kwa wakati na kwa ufanisi ili kuwezesha mahitaji ya walimu wa Sekondari.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha warsha iliyofanyika kwa muda ya siku mbili ya tarehe
28 na 29 Agosti 2025, ya mapitio ya mfumo wa MEWAKA ulioboreshwa Mratibu wa
Mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Lina Rujweka, alitoa shukrani
kwa juhudi na muda uliowekezwa na wadau wote, ikitambua mchango wao muhimu
unaotarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mradi huu hasa
UNESCO na Jamhuri ya Korea kupitia mradi wa ‘’KFIT III wa Transforming
Education through ICT in Africa’’ kwa kuendelea kutoa msaada wa kifedha.
Shirika la UNESCO Dar es Salaam, kwa
kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), inaendelea na juhudi za
uboreshaji mfumo wa MEWAKA ili kuzingatia mahitaji ya walimu wa shule za
sekondari.
Ushirikiano huu ulitokana na tathmini ya
mahitaji iliyoonyesha kuwa mfumo wa sasa ulikuwa umeundwa mahsusi kwa ajili ya
kuwa jukwaa la mafunzo ya maendeleo ya kitaaluma kwa walimu wa shule za msingi.
Hivyo, wadau walikutanishwa ili kupitia
toleo la awali la mfumo wa MEWAKA kwa lengo la kuhakikisha umuhimu, ubora, na
uendelevu wa muda mrefu wa jukwaa hilo.
Wadau hao walikuwa kutoka wizara ya elimu, sayansi na Teknolojia ,
Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Taasisi ya Elimu Tanzania, Tume ya
Kitaifa ya UNESCO na baadhi ya walimu wa shule za sekondari.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, mwakilishi
kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ally Mape alisema majukwaa ya
kidijitali ni nyenzo yenye nguvu ya maendeleo ya kitaaluma, yanayochangia kwa
kiasi kikubwa kuwawezesha walimu kupata ujuzi na kujiamini ili kufanikisha kazi
zao katika Dunia ya sasa.
Kwa upande wake mkuu wa Sekta ya Elimu kutoka Ofisi ya UNESCO Dar es Salaam, Dkt. Faith Shayo, ameeleza kuwa lengo kuu ni kupanua upatikanaji wa mafunzo endelevu ya kitaaluma kupitia majukwaa ya kidijitali, hivyo itasaidia kuboresha matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji kote nchini.
Hata hivyo Dkt. Shayo aliwahimiza wadau
kutoa maoni na mitazamo yao kusaidia kuhakikisha toleo la mwisho la mfumo huu
sio tu kuwa la kisasa bali pia rahisi kutumia na lenye matokeo chanya.
Mpango huu unalingana na juhudi za Serikali
za kuunganisha TEHAMA katika elimu, kama inavyoonekana katika sera na mikakati
muhimu ya kitaifa ikiwemo Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023,
Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali 2025 – 2030, Dira ya Maendeleo ya
2050, Mitaala ya Elimu ya Msingi na ya Ualimu, pamoja na mipango ya kimataifa
kama vile Malengo ya Maendeleo Endelevu hasa lengo namba nne.





No comments:
Post a Comment