Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) (kulia) akiwa katiika Kiwanja cha Ndege cha Addis Ababa akiwa njiani kuelekea Cairo, Misri katika sherehe za kumuapisha Rais Mteule, Mhe. Abdel Fattah al Sisi. Mwingine katika picha ni Bw, Shelukindo, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia. |
Waziri wa Mambo ya Nje (kulia) akipokea taarifa fupi kutoka kwa Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Misri, Bw. Jestas Nyamanga katika Hoteli aliyofikia Mhe. Waziri ya Fairmont. |
Mhe. Waziri Membe mwenye miwani akiwa amesimama mbele ya Hoteli ili kuingia katika gari maalum kwa ajili ya kumpeleka eneo lililofanyika sherehe za uapisho. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Vincent Kibwana. |
Balozi Kibwana (kushoto) akijadili jambo na Afisa wake, Bw. Celestine Kakere |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) kushoto akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Nabil Fahmy. |
Waziri Membe akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mawaziri wenzake baada ya kushiriki katika chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa heshima yao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri |
Waziri Membe akibadilishana mawazo na watu mbalimbali kabla ya kupata Chakula cha Jioni. |
Sehemu ya mto Nile ambapo kando yake ndiyo kuna Hoteli ambayo Waheshimiwa Mawaziri waliandaliwa chakula cha jioni. Angani ni helikopta ikiwa katika doria kuhakikisha kuwa hakuna mtu anadhurika. |
Waziri Membe akiwa na Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wa Misri, Bi. Fatma. Bi. Fatma ambaye alishawahi kufanya kazi katika Ubalozi wa Misri nchini Tanzania ndio alikuwa Afisa Itifaki anayemuhudumia Mhe. Waziri na ujumbe wake. |
Na Ally Kondo, Cairo
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb)
amemwakilisha Rais Kikwete katika sherehe za kumuapisha Mkuu wa Majeshi
wa zamani, Field Marshal Abdel Fattah al Sisi kuwa Rais mpya wa Misri.
Rais Sisi aliapishwa na Jaji Mkuu katika viwanja vya Mahakama Kuu ya
Misri siku ya Jumapili tarehe 08 Juni, 2014 ambayo ilitangazwa kuwa ni
siku ya mapunziko.
Sherehe
za uapisho zilihudhuriwa na Viongozi wa nchi mbalimbali duniani,
hususan kutoka nchi za Kiarabu na Afrika. Nchi za Kiarabu ziliwakilishwa
vizuri katika sherehe hizo kwa kutuma Viongozi wa ngazi ya Juu
ukilinganisha na nchi za Afrika ambazo nyingi zilituma Mawaziri wa Mambo
ya Nje isipokuwa chache kama vile Somalia, Chadi na Equatorial Guinea
ambazo Marais wao walishiriki wenyewe.
Sherehe
za uapisho zilipambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo gwaride la
kijeshi, hotuba za Rais anayengia madarakani na anayetoka na kila
mwakilishi kupata fursa ya kusalimiana na kufanya mazungumzo ya muda
mfupi na Rais Sisi.
Sherehe
hizo ambazo zilifanyika huku kukiwa na ulinzi mkali zilishuhudiwa pia,
wafuasi wa Rais Sisi wakizunguka katika mitaa ya jiji la Cairo wakiwa
katika magari, pikipiki au kutembea kwa miguu wakiwa wamebeba bendera za
nchi hiyo huku wakifyatua fataki, kupiga mayowe na honi.
Wachambuzi
wa mambo walieleza kuwa Rais mpya wa Misri anatarajiwa kuituliza nchi
hiyo ambayo imekuwa ikikumbwa na machafuko ya kisiasa ya mara kwa mara
tangu mapinduzi ya wananchi yaliyomuondoa madarakani Rais Hosni Mubarak
mwaka 2011.
Hata
hivyo, walikiri kuwa Rais Sisi anakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kufufua uchumi wa nchi hiyo ambao umedorora kwa kiasi
kikubwa kutokana na machafuko hayo. Changamoto nyingine ambayo Rais
Sisi anakabiliwa nayo ni kurejesha mshikamano na umoja wa wananchi wa
Misri ambao kwa kiasi kikubwa wametofautiana mitazamo kutokana na hali
ya mambo inavyokwenda katika nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment